MPANGO WA MUNGU KUHUSU MAWAZO YETU.

Bila mimi hamuwezi

Mawazo yetu ni muhimu sana kwa maisha yetu ya sasa na yale yajayo. Kwa hiyo, Mungu anayo mengi ya kusema kuyahusu. Ametuwekea utaratibu na mwongozo wa kuweza kuvuna baraka zake kwa kupitia kwenye mawazo yetu. Hata hivyo ni muhimu kukumbuka wakati wote kuwa msaada wetu unatoka kwa Bwana. (Zaburi 124:8). Pia Yeye anasema: “Mimi ni mzabibu ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamuwezi kufanya neno lolote.” (Yohana 15:5).

3
Kwa hiyo, hata katika suala la kuwaza au kutafakari, bila msaada wake, hatuwezi kitu. Kama kuwaza tu kwa namna inayofaa hatuwezi, sembuse kuyafanya hayo mawazo yetu yatupatie shauku za mioyo yetu? Agizo la muhimu analotupa Bwana, tunalopaswa kulizingatia ni kuwa, “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe.” (Mithali 3:5).


Bwana anasema nisizitumainie akili zangu! Hili ni jambo la kushangaza kabisa. Kuzitumainia akili maana yake ni kufanya mambo yangu bila kumpa Mungu nafasi. Yaani, nikishawaza jambo tu, ninalitenda. Tena ninakuwa ninajua tu kuwa yale yote ninayoyafanya ni ujanja, uwezo na juhudi zangu mwenyewe.


Mungu anatuonya kuhusu kuzitumainia akili, si kuhusukuzitumia. Tunatumia akili zetu kuchagua wapi pa kutumainia. Biblia inasema, “Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi.” (1Wakorintho 15:34)


JINSI YA KUWA NA MAWAZO YENYE NGUVU

Hivi itakuwaje kama nitaweza, kila siku, kuwa na mawazo ya kushinda, kuweza, kufanikiwa, kupona na mengine ya namna hii hata kama kwa namna ya kibinadamu mambo yanaonekana kuwa ni mabaya? Bila shaka maisha yangu yatabadilika kwa haraka sana kuelekea kwenye ubora. Tunaweza kabisa kuzifunza akili zetu kuwaza mawazo chanya na si mawazo hasi, yaani tunaweza kuwa na imani. Na uzuri ni kwamba yupo Bwana upande wetu ambaye anatusaidia katika kila hatua.


Kutofautisha nia

Ili tuweze kujenga tabia ya kutafakari kwa mafanikio, ni lazima tuwe na uwezo wa kuchunguza na kutambua nia iliyomo ndani mwetu kila wakati.


Ndani mwetu kuna nia za aina mbili. Biblia inasema, “Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani.” (Warumi 8:6). Kwa hiyo, kuna nia ya mwili na nia ya roho. Nia ya mwili ni nia ambayo hujificha sana kiasi kwamba wakati mwingine ni vigumu kuigundua. Bila shaka umeshawahi kukutana na hali zifuatazo:


• Unapotaka kulala unaomba ulinzi wa Mungu uzingire nyumba yako. Lakini, baadaye ukisikia kishindo chochote nje, unaingiwa na hofu kubwa. Kilichokufanya uombe ni nia ya roho, lakini kilicholeta hofu ni nia ya mwili. Hii imekufanya usimwamini Mungu ambaye hapo tu kabla uliomba ulinzi wake.

• Unaposafiri, unalifunika gari kwa damu ya Yesu. Lakini, gari likiyumba kidogo tu njiani, hukumbuki tena maombi uliyofanya. Hofu inaletwa na nia ya mwili.

• Unaweza kuomba Bwana akufungulie milango ya mafanikio, kisha baada ya muda mfupi unaanza kusema hali ni ngumu, maisha ni magumu. Nia ya roho ilikusukuma kuomba lakini nia ya mwili ikakufanya ukiri kutowezekana.

• Watumishi wa Mungu wanaposema kuwa Bwana ametupa mamlaka ya kutoa pepo na kuponya wagonjwa, unashangilia na kupiga makofi. Lakini ukiangalia, hujawahi kumwombea mgonjwa yoyote wala kukemea pepo. Nia ya roho ilikufanya upige makofi ya furaha lakini nia ya mwili inakuzuia kuyatendea kazi mambo hayo.


Mifano hii michache inatuonyesha kuwa, kumbe kwa nje unaweza kuonyesha kuwa uko upande wa Mungu, lakini ndani yako ukawa uko kinyume kabisa. Shida ni kwamba, ile nia ya ndani ambayo iko kinyume na Mungu ndiyo inakuwa na nguvu, na ndiyo inayoshinda. Kibaya zaidi ni kuwa, unakuwa hujitambui kwamba una hali hiyo.


Kuchagua nia sahihi

Ili upate mazao mengi na bora shambani ni lazima ufanye kazi. Lakini, ili upate magugu mengi na mazao yako yaharibiwe, unatakiwa ukae tu bila kufanya chochote. Magugu yatakuja yenyewe tu. Hayahitaji juhudi yoyote. Akili ya mwanadamu ni kama shamba. Mawazo safi ni mazao bora. Mawazo mabaya ni magugu. Usipojibidisha kwa lolote kuhusu mawazo yako, ni lazima utavamiwa na lundo la magugu, yaani mawazo yasiyofaa! Wakati mwingine unaweza usilitambue hilo.


Dalili zinazoonyesha kuwa akili yako ina magugu hayo ni hizi zifuatazo: kusonya kila mara, kunung’unika, kulaumu watu wengine, kukosa raha, kujiinamia, kutikisa kichwa, kushika tama, kukosa usingizi, n.k.


Ili uwe na mawazo bora yatakayozaa matunda mema maishani, ni lazima ufanye kazi ya kung’oa magugu wewe mwenyewe, kwa maana, “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu.” (Mithali 16:1).


Ni lazima kufanya uchaguzi wa makusudi (conscious selection) wa mawazo mema kutoka katika Neno la Mungu, na kuyatafakari hayo muda wote. Kufanya uchaguzi wa makusudi maana yake ni kuwa, usiache tu mawazo yoyote yaingie na kutoka akilini kama yapendavyo. Simama katika mlango wa akili yako kukagua kila wazo linalojitokeza, kisha ruhusu yaingie yaliyo safi na zuia yaliyo magugu.


Ni lazima kuitambua nia ya mwili kila wakati na kuishinda kabisa na kubaki na nia moja tu – ya roho. Unaishinda kwa kukiri neno la Mungu. Kwa mfano, unapoingiwa na hofu, unasema, “Imeandikwa kuwa Mungu hajanipa roho ya woga bali ya nguvu.”


Kitendo cha wewe kusema hivyo kinadhihirisha kuwa umetambua kwamba kuna magugu, yaani nia isiyo sahihi. Kwa njia hiyo tu ndipo utaona nguvu za Mungu zikifanya kazi maishani mwako. Hili ni jambo la muhimu sana! Endapo hufanyi hivyo, uwezekano mkubwa ni kuwa uko katika kundi la wale ambao hawajui kuwa
wamevamiwa na wanaendeshwa na hiyo nia ya mwili.


Kumbuka kuwa, mwanzoni hii itakuwa ni vita kubwa. Utapata upinzani mkubwa. Hili ni jambo la kawaida kabisa. Maana kuhusu adui zetu, Bwana anasema, “Sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja nchi isiwe ukiwa na wanyama wa bara wakaongezeka kukusumbua. Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hata utakapoongezeka wewe, na kuirithi hiyo nchi.” (Kutoka 23:29-30).


Kasi ya kushinda kwako inategemea kuongezeka kwako - katika ufahamu, maarifa na nguvu. Kwa hiyo, Bwana anatutia moyo akisema, “Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.” (Yoshua 1:9).


Ukidumu katika kuyazuia mawazo mabaya kuingia akilini mwako kwa kutafakari mawazo mema kutoka katika neno la Mungu, hakika yake, baada ya muda mfupi utaona unabadilika kabisa! Hakika! Kwa maana, neno hilo ni roho na roho ndiyo itiayo uzima! (Yohana 6:63).


Kwa mfano, unapoumwa, badala ya kutafakari jinsi mwili unavyouma na udhaifu ulio nao, tafakari kwamba, “Kwa kupigwa kwake mimi nimepona; yeye ameyachukua magonjwa yangu. Mimi ni mzima katika Jina la Yesu.” Unapoishiwa fedha, badala ya kutafakari jinsi ambavyo shida uliyonayo ni kubwa kuliko fedha unayopata, tafakari, kwa mfano, “Yote yawezekana kwa imani. Kwa Jina la Yesu naamuru fedha zije kwa ajili ya hitaji hili nililonalo.”


Kwa kufanya hivi, utakuwa unatimiza andiko linalosema, “Linda sana moyo wako maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.” (Mithali 4:23). Uzima haushii kwenye kupona tu magonjwa. Hata kupata fedha, chakula na nguo ni sehemu ya uzima. Ndani ya moyo kuna chemchemi itakayotoa huo uponyaji na hizo fedha ambayo ni mahitaji yako.


Ukiyawaza yale yaliyo kinyume na neno la Mungu, unakuwa katika kundi hili: “Asiyetawala roho yake ni mfano wa mji uliobomolewa, usio na kuta.” (Mithali 25:25). Utaanza tu kukiri udhaifu na kushindwa. Hatimaye, utavamiwa na roho za kuzimu za kila namna, maana hauna ulinzi. Na hizo ndizo zitakazokudidimiza chini zaidi na zaidi ili litimie andiko lisemalo, “Mauti …. huwa katika uwezo wa ulimi.” (Mithali 18:21).


Chagua mawazo ya kutafakari! Usikubali hata kidogo kuwa mtumwa wa mawazo. Usitawaliwe na mawazo, bali uwe mtawala wa mawazo. Yaani, wewe ndiyo uchague nini cha kuwaza na nini cha kutupa nje. Kasha utaona ahadi za Mungu zikitimia maishani mwako
Share To:
Magpress

Calvin Petro

Kwa Moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na Maagizo yako. Moyoni mwangu nimeliweka Neno lako Nisije nikakutenda dhambi. (Zaburi 119:10-11).

Post A Comment:

0 comments so far,add yours