Bwana Yesu asifiwe!

Jambo la 2 tunalojifunza juu ya: “Mambo unayohitaji kuyajua kuhusu ndoto unazoota ili iwe vyepesi kufanikiwa kimaisha” ni hili:

“Ndoto ni mlango wa kiroho ndani ya mtu, unaomwingizia vitu maishani mwake kutoka vyanzo tofauti vya ndoto”

Ndoto ambazo mtu anaota, huwa hazina vyanzo vinavyofanana. Utofauti wa vyanzo vyake, unasababisha ufuatiliaji wake usifanane pia! Ukikosea kukijua chanzo cha ndoto uliyoota, uwe na uhakika wa kukosea pia namna ya kuishughulikia!

Kibiblia – ndoto ambazo mtu anaota, zinaweza kutokana na chanzo kimojawapo kati ya vyanzo vifuatavyo:

1. Ndoto zinazotoka kwa Mungu:
Biblia inasema kwenye kitabu cha Ayubu 33:14, 15 ya kuwa: “Mungu huwa anasema na mtu “mara moja”, na wakati mwingine hata mara mbili, kwa njia ya “ndoto”…usingizi mzito uwajiliapo watu”.

Njia mojawapo ambayo mfalme Sauli alitegemea Mungu angeitumia kujibu maombi yake, ilikuwa ni njia ya “ndoto” (1 Samweli 28:6). Asingetegemea Mungu amjibu maombi yake kwa njia ya ndoto, ikiwa huko nyuma alikuwa hajawahi kuona wala kusikia Mungu akifanya hivyo.

Na tunajulishwa ya kuwa, njia mojawapo ambayo Mungu atakuwa anaitumia kuwaongoza watu, akimtumia Roho Mtakatifu, ni kwa njia ya “ndoto” (Matendo ya Mitume 2:17).

2. Ndoto zinazotoka kwa shetani:
Ndoto hii inayotajwa katika Kumbukumbu ya Torati 13:1 – 4, ni wazi kwamba chanzo chake ni “shetani”. Hii ni kwa sababu maelekezo ya ndoto hiyo, ni kutaka mtu aache kumwabudu Mungu, na badala yake afuate miungu mingine. Hii inatudhihirishia ya kuwa, shetani anaweza akaingiza kitu ndani ya mtu, kwa kutumia njia ya ndoto.

3. Ndoto zinazotokana na mtu kuwa na shughuli nyingi:
Tunalijua hili kwa sababu ya kile tukisomacho kwenye kitabu cha Mhubiri 5:3 ya kuwa: “…ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi….!
Ndoto za namna hii zinaweza kumjia mtu, kwa sababu ya kujikuta amefanya “shughuli” zingine, ambazo hazipo kwenye ratiba ya Mungu – kwa ajili yake siku hiyo!

4. Ndoto zinazotokana na hali ya kiroho ya mahali ambapo mtu amelala:
Ndoto inayokuja kwa namna hii, tunaiona tunaposoma kitabu cha Mwanzo 28:10 – 17. Yakobo aliota ndoto ile, kwa sababu ya hali ya Kiroho ya ardhi ya eneo alilolala usiku ule!
Ndoto ile ilimpa ufahamu Yakobo kujua hali ya kiroho ya eneo lile, na ya ardhi ile. Ndiyo maana alisema: “Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua….hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni” (Mwanzo 28:16,17).

Utofauti huu wa vyanzo vya ndoto ambazo mtu anaweza kuota, unanisukuma moyoni kukushauri na kukuhimiza kujiombea mambo yafuatayo:

Jambo la 1: Jiombee ili Mungu akupe kujua chanzo cha ndoto unazoota ni kipi. Soma Danieli 2:27, 28.

Jambo la 2: Jiombee ili Mungu akiamua kukusemesha kwa njia ya ndoto, upate kusikia na kuelewa ujumbe uliomo ndani yake. Soma Ayubu 33:14, 15.


Jambo la 3: Jiombee na “kuziba” kwa kutumia damu ya Yesu, lango la ndoto ndani yako, ili lisipitishe ndoto za shetani kuja kwako. Kumbuka Mungu aliwaambia wana wa Israeli wanaweza kutumia “damu” kumzuia Shetani asipite kwenye “milango” yao. Soma Kutoka 12:21 – 23 


Share To:
Magpress

Calvin Petro

Kwa Moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na Maagizo yako. Moyoni mwangu nimeliweka Neno lako Nisije nikakutenda dhambi. (Zaburi 119:10-11).

Post A Comment:

0 comments so far,add yours