Bwana
Yesu asifiwe sana!
Leo
tuangalie jambo la 3, katika yale ambayo ni vyema ukayafahamu juu ya ndoto, ili
uweze kufanikiwa kimaisha.
Jambo
hilo la 3 ni hili: “Zijue Ishara zitakazokuonyesha ya kuwa ni ndoto ipi
uliyoota inayohitaji ufuatiliaji wa haraka”
Hizi
zifuatazo ni baadhi ya ishara, nilizoweza kukukusanyia toka katika biblia,
zitakazokusaidia kujua ikiwa ndoto uliyoota, inahitaji ufuatiliaji wa haraka,
na wa makini.
Ishara
ya 1: Kuiota ndoto ile ile zaidi ya mara moja! Yusufu alimwambia Farao hivi:
“Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo
Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi”. (Mwanzo 41:32).
Hii
haina maana yaliyomo katika ndoto huwezi kuyabadilisha – la hasha! Ukiota ndoto
ile ile au zinazofana zaidi ya mara moja, ni ili ujue umuhimu wa kuyafuatilia
yaliyomo kwenye ndoto hizo – kwa haraka na kwa makini. Wazo hili unalipata
ukisoma Ayubu 33:14,15.
Ishara
ya 2: Ndoto kukutia hofu – ambayo hata baada ya kuamka hofu hiyo unajikuta bado
unaisikia! Mfalme Nebukadreza aliwahi kusema hivi juu ya ndoto aliyoota: “Nikaota
ndoto iliyonitia hofu ….” (Danieli 4:5).
Kabla
ya kuota ndoto ile, hakuwa na hofu. Ndoto aliyoota ilibeba roho ya hofu –
iliyomwingia Nebukadreza wakati akiiota ndoto ile! Na alipoamka – alijikuta
amejaa hofu kutokana na ndoto aliyoota.
Ishara
ya 3: Kujisikia umefadhaika moyoni baada ya kuota ndoto! Tunasoma katika
Danieli 2:1 ya kuwa: “Nebukadreza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika,
usingizi wake ukamwacha”.
Je,
umewahi kusikia hali ya namna hii, mara tu baada ya kuzinduka usingizini baada
ya kuota ndoto? Ikiwa hali ya namna hii imewahi kukupata – basi ujue ndoto hiyo
ina ujumbe wa muhimu unaohitaji kuufahamu! Soma Danieli 2:28.
Ishara
ya 4: Hali ya kufadhaika iliyoambatana na kitu kingine! Nebukadreza katika
Danieli 2:1 – aliposikia kufadhaika baada ya kuota ndoto aliyoota – kuna hali
nyingine zaidi iliyojitokeza kwake! Biblia inasema ya kwamba: “ na roho yake
ilifadhaika, usingizi wake ukamwacha”!
“Mnyweshaji
na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani” na Yusufu, waliota “ndoto
wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto
yake” (Mwanzo 40:5).
Biblia
inasema, si tu kwamba Yusufu “akawaona wamefadhaika” (Mwanzo 40:6); lakini pia
akawaona mfadhaiko ule waliokuwa nao, uliambatana na “nyuso” zao kukunjamana
(Mwanzo 40:7).
Farao
alipoota ndoto mbili mfululizo katika usiku mmoja, asubuhi yake “roho yake
ilifadhaika” (Mwanzo 41:8). Ule mfadhaiko uliambatana na mahangaiko ya kutaka
kupata tafsiri ya ndoto zile, bila kujali hali za kiroho za wale aliokuwa
anawaulizia tafsiri zake (Mwanzo 41:8).
Mahangaiko
ya Farao yalipokwama kupata tafsiri, ndipo Mungu alipomkumbusha mkuu wa
wanyweshaji wake juu ya Yusufu, na akamkutanisha Farao na Yusufu. Yusufu akampa
Farao tafsiri za ndoto zake, na maelekezo ya kufanya.
Ishara
ya 5: Ndoto zinazosababisha jambo uliloota lijitokeze katika mwili wako!
Unaposoma Ayubu 4:12 – 16, utatambua ya kwamba, Elifazi aliota ndoto iliyomtia
hofu, na mifupa yake yote ilitetemeka. Unapolitafakari jambo hili, unaona
uwezekano mkubwa wa Elifazi kusikia maumivu ya mifupa yake alipoamka, baada ya
kuota ile ndoto.
Kuna
mtu aliyeniandikia ujumbe wa simu mwaka 2016 akiomba nimwombee, ambaye alikuwa
na maumivu katika mwili wake, yalisababishwa na ndoto aliyokuwa ameota. Mwaka
2009 aliota amepigwa risasi kwenye paja lake, na katika ndoto alipokuwa anaota,
alijua risasi ilikuwa imebaki kwenye paja na ilihitaji kutolewa. Lakini aliamka
toka usingizini kabla risasi haijatolewa!
Mwaka
2013 mguu wake ukaanza kuuma, na kuwa na maumivu makali kwenye eneo lile la
paja palipopigwa risasi! Kwa nini? Kwa sababu ile “risasi ya kiroho” iliyompiga
katika ndoto ilikuwa haijaondolewa!
Pia
kuna dada mmoja ambaye alinisimulia ya kuwa aliota akicheza mpira wa miguu na
wenzake. Na alipoupiga mpira kwa mguu wake, mara ule mguu ukaanza kumuuma. Na
mara akaamka toka usingizini.
Lakini
alishangaa alipoona ya kuwa, baada ya kuamka toka usingizini – mguu ule
uliokuwa unauma kwenye ndoto ulikuwa bado unamuuma! Na tokea usiku ule alikuwa
hawezi kutembea bila kuchechemea, kwa kuwa mguu ule uliendelea kumuuma.
Tulipokutana
alipotoka hospitali na aliponieleza shida ile, nilijua tatizo lililompata.
Nikamwombea na akapona muda ule ule nilipomwombea!
Ishara
ya 6: Imani yako kwa Mungu katika Kristo Yesu au/na utumishi wako kwake kuanza
kuyumba na kuhangaika na kupoa – baada ya kuota ndoto!
Tukisoma
Kumbukumbu ya Totati 13: 1 – 4, tutaona ya kuwa, kuna ndoto ambazo lengo lake,
ni kumwondoa mtu kwenye imani aliyonayo, kwa Mungu huyu tunayemwabudu katika
Kristo Yesu.
Tena –
tunaposoma Yeremia 23:25 – 17, tunajulishwa ya kuwa, kuna ndoto ambazo lengo
lake ni kutaka kumsahaulisha mtu jina la Bwana Yesu!
Kwa
hiyo – ukiona baada ya kuota ndoto imani yako, na utumishi wako kwa Mungu
katika Kristo Yesu, vinaanza kupoa na kuyumba – ni ishara ya kuwa unahitaji
kuifuatilia hiyo ndoto kwa haraka, na kwa umakini mkubwa kwa njia ya maombi.
Wengine
waotao ndoto zenye malengo kama hayo; wanajikuta au hawaendi kanisani bila
maelezo yanayoeleweka, au nguvu za maombi zinapotea, au wanajikuta hawana
msukukumo tena hata wa kusoma biblia.
Ushauri
wangu kwako kuhusu ishara hizi:
1. Hizi
ishara zikiwa kubwa (“Strong”), au nzito (“heavy”) moyoni mwako – ina maana
ufuatiliaji ufanyike kwa haraka – maana muda umekaribia wa kutimia yote
uliyoyaona kwenye ndoto, ikiwa utayanyamazia! Labda kama unataka yatimie kama
ulivyoyaona kwenye ndoto uliyoota.
2.
Iandike ndoto unayoona ishara nilizokushirikisha, zinakupa kujua inahitaji
kufuatiliwa. Iandike hiyo ndoto hata kama bado hujui tafsiri yake, wala ujumbe
wake. Soma Habakuki 2:2 na Danieli 7:1
3. Anza
kuiombea hiyo ndoto, na usiache kuiombea, hadi hizo “ishara” zilizokusukuma
kuanza kuomba zimeondoka moyoni mwako au mwilini mwako!
Ni
maombi yangu ya kuwa Mungu atasikia kuomba kwako!
Na
Mungu azidi kukubariki!
Post A Comment:
0 comments so far,add yours