Bwana Yesu asifiwe milele!
Leo nataka tujifunze kwa pamoja, “namna ya kuitumia Damu ya Yesu, kusema kwa niaba yako, au kwa ajili yako”
Tunapojifunza hili, ni vizuri na ni muhimu tukaangalia mambo yafuatayo:
Jambo la 1:
Fahamu hili ya kwamba: Damu ya Yesu ina uwezo wa kuongea!
Wazo hili tunalipata tunaposoma Waebrania 12:24 kuwa “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko damu ya Habili”.
Mungu anatumia mstari huu, kutujulisha ya kuwa, damu ina uwezo wa kuongea! Damu ya Yesu na damu ya Habili – zote zina uwezo wa kuongea!
Unaposoma Mwanzo 4:10, damu ya Habili ilipokuwa “inaongea” mbele za Mungu, maneno yake yaliambatana na kilio! Ndiyo maana Mungu alimwambia Kaini ya kuwa “sauti ya damu ya ndugu yako inanililia….”
Jambo la 2:
Fahamu hili ya kuwa: Damu imepewa uhalali na Mungu wa kusema kwa niaba ya mtu!
Ikiwa damu imepewa uhalali na Mungu wa kusema kwa niaba ya mtu; kwa hiyo ni vyema ukajua ya kwamba, vivyo hivyo damu imepewa uhalali na Mungu, wa kusema kwa niaba YAKO, au kwa ajili YAKO, na ikasikilizwa isemacho!
Mungu anasema hivi: “nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu, kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu” (Mambo ya Walawi 17:11).
Haya maneno “nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu …”; ni maneno ya Mungu yanayotoa mamlaka halali kwa damu, ili iwe inasema kwa niaba yetu, yaani “Kwa ajili ya nafsi” zetu na “kwa sababu ya nafsi” zetu!
Unalipata hili? Hii ina maana ya kuwa, na sisi tuna uhalali wa kuitumia damu, ili iweze kusema kwa ajili ya nafsi zetu, na kwa sababu ya nafsi zetu!
Wakati wa agano la kale, damu iliyohalalishwa kusema kwa ajili ya nafsi za watu, ilikuwa ni “damu ya mbuzi na mafahali” (Waebrania 9:13). Lakini wakati huu wa agano jipya, uhalali wa kufanya kazi hii ya kusema kwa ajili ya nafsi zetu, ni damu ya Yesu Kristo (Waebrania 12:24). Kufuatana na Mambo ya Walawi 17:11, kazi mojawapo ya kusema iliyokabidhiwa “kwa damu” ni juu ya “upatanisho” au “kupatanisha”!
Unaposoma Waefeso 2:16, damu ya Yesu ina uwezo halali kutoka kwa Mungu, wa kusema kwa ajili ya nafsi ya mtu, ili aweze kupatanishwa na Mungu! Pamoja na hilo, damu ya Yesu ina uwezo halali toka kwa Mungu, wa kusema kwa ajili ya nafsi ya mtu, ili aweze kupatanishwa na mtu mwingine. Hili unalipata unaposoma Waefeso 2:13, 15 – 17.
Matokeo ya kupewa kile ambacho damu ya Yesu imesema kwa niaba yako ni kule kunakoitwa au kunakojulikana na Warumi 5:9 kama: “Kuhesabiwa haki katika damu yake”!
Kuhesabiwa haki katika damu ya Yesu, kuna maana ya kuwa unachopewa, au unachopokea, si kwa sababu ya kustahili kwako, bali ni kwa sababu Mungu ameheshimu, na kusikia, na kuikubalia damu ya Yesu, juu ya kile ilichosema kwa niaba yako, kwa ajili ya nafsi yako!
Ukiliangalia jambo hili kwa mtazamo huu, utayaelewa zaidi maneno yaliyopo katika Warumi 3:23 – 26 maneno hayo yanasema hivi:
“Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;…
…ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa, apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu”
Tunapoona faida kama hii iliyomo katika damu ya Yesu, ni muhimu tujue kiuhalisia tunaweza kuitumia kwa namna gani!
Musa aliitumiaje aina ya damu iliyohalalishwa wakati wa kipindi chake? Biblia inatupa muhtasari wa jinsi Musa alivyoitumia damu katika maisha yake ya kwamba: “aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote, akisema, hii ni damu ya agano mliloamriwa na Mungu” (Waebrania 9:19, 20)
Biblia inaendelea kusema hivi, juu ya Musa, alivyoitumia damu wakati wa kipindi chake, ya kuwa: “Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada alivinyunyizia damu vivyo hivyo” (Waebrania 9:21)
Nataka ukumbuke ya kuwa, Musa alinyunyiza damu juu ya “Kitabu”; na juu ya “watu wote”, na juu ya “hema”, na juu ya “vyombo vyote”.
Kwa mfano: Ikiwa umeomba kazi mahali, kwa kupeleka barua yako ya kuomba kazi, usisahau kuitumia damu ya Yesu, na “kuiamini kusema” kwa niaba yako, kwa ajili ya nafsi yako, ili upewe hiyo kazi!
Ni muhimu usisahau kunyunyiza damu ya Yesu, juu ya barua yako uliyoiandika ya kuomba kazi, na juu ya vyeti vyako ulivyoambatanisha nayo! Na nyunyiza damu ya Yesu, juu ya “watu wote” watakaohusika na kuipokea, na kuijadili, na kukujibu barua yako, katika kila hatua!
Na ukiitwa kwenye usaili (interview), nyunyiza damu ya Yesu juu ya “Hema”, au katika eneo ambalo usaili huo utafanyika; na juu ya watu wote watakaohusika na usaili huo; na juu ya watu wote watakaohusika na maamuzi ya mwisho, juu ya nani atakayeajiriwa baada ya usaili huo kukamilika!
Kumbuka katika kipindi hiki cha agano jipya, tunanyunyiza damu ya Yesu kwa imani, huku tukisema kile tunachotaka, au tunachoomba kwa Mungu ili atufanyie, kwa msaada wa utendaji wa maneno na sauti ya damu ya Yesu.
Kwa ajili ya hii unaweza – kwa mfano – ukasema – “Nanyunyiza juu ya barua hii damu ya Yesu ya agano jipya, iliyoamriwa na Mungu kusema kwa niaba yangu, na kwa ajili yangu – ili iende ninakoipeleka barua hii, na iweze kusema kwa ajili yangu! Kumbuka hili: Unaposema kwa mamlaka, na kwa imani juu ya hicho usemacho – unatoa mamlaka kwa neno ulilolisema, ili kwamba lipate kudhihirika, au kutokea kama ulivyosema! Hii ni sawa na Marko 11:23, 24.
Unaweza kuitumia damu ya Yesu kwa namna hii, mahali popote ambapo – wewe unajadiliwa, au unasemwa, au unapimwa, au una kesi ya kujibu, au umeshtakiwa – huku ukiamini ya kuwa, damu hii inakutetea, ili wewe ndiwe upate “haki”, sawa na uwakilishi wa damu ya Yesu ulivyo mbele za Mungu kwa ajili yako!
Fanyia mazoezi jambo hili, na naamini utaona Mungu akilithibitisha neno lake, juu ya uwezo wake huo, aliouweka kihalali ndani ya damu ya Yesu kwa ajili yetu.
Na usiache kunishirikisha ushuhuda wa kile ambacho Mungu amekutendea, ulipoweka katika matendo hiki nilichokufundisha leo!
Bado somo hili nitaendelea kukufundisha kwa njia ya “Post” zingine nitakazoendelea kukuwekea kwenye ukurasa wetu huu wa ‘FaceBook’. Christopher & Diana Mwakasege(Mana Ministry)
Tuzidi kuombeana!
Post A Comment:
0 comments so far,add yours