Na Mwalimu Deborah Lema.
delechansie@gmail.com
UTANGULIZI.
Lazima tujue mazingira au ushawishi
unaoweza kumsababisha mtu atende dhambi au amkosee Mungu. Si kila mahali au
kija jambo linaweza kukutoa katika uwepo wa Mungu, ila yapo mambo au mazingira
ambayo humpelekea mtu kutenda dhambi, iwe kwa kudhamiria au kwa nguvu ya
ushawishi. Na pia si kila mtu anayetenda dhambi kwamba anafurahia, hata
makahaba na walevi wa kupindukia tunaowaona si wote wametaka au wanafurahia
hali zao, ila kuna mazingira yanayowapelekea kuwa hivyo walivyo. Katika Warumi 7:15 inasema
“Maana
sijui nifanyalo, kwasababu lile nilipendalo, silitendi, bali nilichukialo ndilo
ninalolitenda.”
Unaweza ukatamani sana sana
kumpendeza Mungu na kukaa uweponi mwake wakati wote, lakini kila ukijitahidi
unashindwa, unashangaa mara limetokea hili na lile umemtenda Mungu dhambi. Na
yale ambayo hupendi wala huyawazii kuyatenda ndiyo unaanza kuyatenda kila siku,
Je, ni kwa nini sasa? Ni mambo gani yanasababisha uwe mtu wa kuanguka dhambini
kila mara?
1. Kutokuwa na Msingi wa Neno la Mungu.
Kutokujihusisha na neno la Mungu
humaanisha ya kwamba kuna mwongozo mwingine unaotegemea katika maisha yako
ambao kwa hakika lazima utaangukia DHAMBINI TU.
Daudi anaandika katika
Zaburi 119:105
Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa
njia yangu.
Tunapojikita katika kusoma Neno la
Mungu tunapata kufunuliwa mambo kadha wa kadha na kukaa uweponi mwa Mungu, na
kinyume chake ni kuyumbishwa katika upepo wa kila namna. Katika Hosea 4:6 Neno
linasema
“Watu
wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi
nami nitakukataa wewe…”
Neno la Mungu linakutosheleza katika
kutimiza mahitaji yako ya kila siku na wakati huo huo kutulia uweponi mwake
katika hali ya Utakatifu, Lakini kwa kukosa/kukinai neno tunaangukia dhambini.
2. Hasira.
Hasira imepelekea watu kujiua,
kufukuza wake zao au waume zao, kutukana, kufanya vurugu na maovu mengineyo. Na
kwakutambua hilo Biblia haikuacha kusema hilo ndio maana katika Waeféso 4:26 inasema
“Mwe
na hasira, ila MSITENDE DHAMBI, jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka.”
Ni kweli huwezi ukazuia hasira, na
haikwepeki, kuna mambo yanakera kabisa, ikiwemo ya mambo ya kusingiziwa, n.k
lakini bado tunapewa onyo HASIRA HIZO ZISITUPELEKEE kumtenda Mungu dhambi. Epuka kufanya jambo au maamuzi yoyote ukiwa
na hasira, hyo itakusaidia usitende dhambi.
3. Kuongozwa na mwili.
Maandiko yanasema siku zote nia ya
mwili ni mauti, usitegemee hata siku moja mwili wako utakusukuma kumpendeza
Mungu. Hujawai ona kuna kitu unasukumwa sana kukifanya ndani lakini mwili wako
hautaki kabisa? Je, hatujawahi kusoma kuwa Roho
i radhi lakini mwili ni dhaifu? unaweza ona vile mwili
unapingana na mapenzi ya Mungu. Katika Wagalatia
5:16 Neno linasema
“Basi
nasema, ENENDENI KWA ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.”
Mwili siku zote umejawa na tamaa,
pia hapo hapo neno linasema tamaa ni dhambi, tunaweza ona vile ilivyo muhimu
kuenenda katika Roho na kuongoza na Roho katika mambo yote.
NA SI ROHO TU, BALI ROHO MTAKATIFU, KWANI KUNA
ROHO YA SHETANI PIA.
4. Ushawishi wa wenye dhambi.
Usitegemee mtu aliyezoelea dhambi
akakushawishi wewe mazuri ya kumpendeza Mungu, yawezekana wewe kimbilio lako la
kwanza ni kutaka ushauri au kuambatana na watenda dhambi, sasa lazima ipo siku
watakuangusha dhambini tu. Katika Mithali
1:10 Inasema
“Mwanangu,
wenye dhambi wakikushawishi, wewe usikubali.”
Mungu anajua kabisa wenye dhambi ni
watu wenye kushawishi wengine kuanguka nao dhambini, na kamwe hawawezi
kukuelekeza katika njia ya haki, hujawahi
ona kama ni mlevi anamshawishi mtu asiyemlevi akimwambia, “onja tu kidogo”? hayo
yote ni ushawishi wa wewe kuanguka dhambini. Kuna
mazingira ya ushawishi unaweza ukayaepuka, na kama hayaepukiki basi JENGA
MSIMAMO UNAPOSHAWISHIWA USIKUBALI.
5. Majaribu.
Majaribu ni kizuizi au kifungo fulani
katika maisha ya mtu. Na watu wengi wameshindwa kuwa wavumilivu kusubiri wakati
wa Bwana na kuamua kupita njia za mkato. Kuna wengine kwa kukosa kazi muda
mrefu, wamekua tayari kuuza miili yao au kutoa rushwa za namna nyingine ili
mambo yao yaende vizuri, wakisahau Wanamtenda
Mungu dhambi kwa ajili ya mambo ya kitambo. Lakini Neno
lasemaje katika Ufunuo 2:10 Inasema
“Usiogope
mambo yatakayokupata, tazama, huyo ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili
mjaribiwe, nanyi mtakua na dhiki siku kumi, UWE MWAMINIFU HATA KUFA, NAMI
NITAKUPA TAJI YA UZIMA.”
Mkazo wangu ni hapo nilipoandika kwa
herufi kubwa, ya kwamba tuwe waaminifu katika kumtazama Mungu, haijalishi
tunachoka na kuumia kiasi gani, tuwe waaminifu mpaka kufa, wala shida na taabu
hizo zisitufanye tumtende Mungu dhambi.
KILA JARIBU UNALOPITIA LINA MLANGO WA KUTOKEA,
WALA LISIKUSABABISHE UMTENDE MUNGU DHAMBI.
6. Kuendekeza mizaha.
Mizaha na utani vimesababisha wengi
kupigana, kuchomana visu, na vurugu za namna mbalimbali. Wengine wameshindwa
kustahimili hasira za mizaha wakaangukia katika matusi na visa. Katika Zaburi 1:1
“Heri
mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki, wala hakusimama katika njia
ya wakosaji, WALA HAKUKETI BARAZANI PA WENYE MIZAHA.”
Biblia inamuita mtu asiyeketi
barazani pa wenye mizaha kuwa HERI kwake. Maana katika mizaha kuna mengi, na
shetani hutumia njia hiyo kupoteza wengi, wengine siku ya tar 1/4 wanaiita
sikukuu ya wajinga, wanaitumia kudanganyana, hivi mfano Mungu akishuka siku
kama hiyo umeshadanganya watu kwa mzaha mzaha hatahesabu uongo huo kama dhambi?
Au uongo wa siku hiyo sio dhambi? Msisitizo
wangu ni kuwa makini na mizaha, usiipe kipaombele sana, kwani ni mlango wa wazi
sana ambao shetani huutumia kupotosha wengi.
7. Kulewa vitu (ulevi wa vitu).
Ulevi si lazima iwe pombe, unaweza
ukapata kitu kikakulewesha akili zako zote na mategemeo yako yote yakahamia
hapo. Kuna watu walimlilia Mungu kwa ajili ya kazi au kupandishwa vyeo baada ya
kupata walivyoomba wakaaza kulewa kwavyo. Na matokeo ya kulewa huko ni kutenda
dhambi kuona huitaji kingine chochote uko huku kufanya unachojisikia, ile hofu
ya Mungu haipo tena kwani ulikua nayo kipindi cha uhitaji, baada ya kupata
ukajisahau. Katika 1 Wafalme 11:4 neno
linasema
“Maana
ikawa, Sulemani alipokua mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu
mingine wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa
Daudi baba yake.”
Tunaweza kusema kuwa Sulemani
alijichimbia kaburi la uharibifu mwenyewe, alifika mahali akaona anajitosheleza
kwa kila kitu,akajitwalia wanawake wengi kadri alivyoweza huo ndio ukawa ulevi wake.
Na mwishowe alimtenda Mungu dhambi kwa kuigeukia miungu mingine.
UNYENYEKEVU ULIOKUA NAO WAKATI WA DHIKI ISIFIKE
WAKATI UKAJISAHAU UONE UMEFIKA, KUANGUKA KU KARIBU KULIKO KUINUKA.
8. Kukosa Nguvu za Roho Mtakatifu.
Kamwe akili zetu, wala fahamu zetu
haziwezi kutusaidia tusimtende Mungu dhambi, ila tukiwa na Nguvu za Roho
Mtakatifu sawa na Matendo 1:8tutaweza. Yesu mwenyewe alitambua hatuwezi ndio maana
akatuachia msaidizi. Katika Yohana
14:16-17 Inasema
“Nami
nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele,
ndiye Roho wa kweli, ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala
haumtambui, bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakua ndani yenu.”
Roho Mtakatifu ndiye pekee anayeweza
kumsaidia mtu asitende dhambi. Ataachilia hofu ndani yako, (hofu ya kumuhofu
Mungu), pia ataongoza hatua za miguu yako yaani uende wapi na usiende wapi, pia
atakupa maneno ya kuzungumza au kutamka, ukiwa na nguvu za Roho Mtakatifu
hauwezi kuwa mropokaji wa ovyo wala mtukanaji, kwa maana hata maneno ya kinywa
chako yataratibiwa naye.
SISEMI KWA HABARI YA ROHO MTAKATIFU, BALI NASEMA
KWA HABARI YA NGUVU ZA ROHO MTAKATIFU, MAANA KAMA NI KUJAZWA ROHO MTAKATIFU
WENGI WALISHAJAZWA LAKINI BADO WANAENDELEA NA DHAMBI. (Matendo 1:8)
9. Kukosa hazina ya Neno la Mungu moyoni mwako.
Kuna watu au niseme kuna Wakristo
ambao hawana Neno kabisa, yaani mtu akisoma Biblia anasoma kama gazeti, hana
muda wa kulitafakari, hana muda wakupata mafunuo juu ya neno, hana muda
wakulihifadhi yaani yupo tu. Ikatokea umemnyang’anya Biblia basi kwisha habari
yake. Lakini mtunzi wa Zaburi 119:11 Anasemaje?
“Moyoni
mwangu nimeliweka Neno lako, nisije NIKAKUTENDA DHAMBI.”
Kumbe Neno ndani ya moyo wake ndiyo
kinga au kengele ya kumwongoza katika njia zake. Unapokua na Neno la Mungu
ndani ya moyo wako unapojaribiwa kutenda dhambi daima litakukumbusha yaliyo
mapenzi ya Mungu kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Lakini kama huna Neno utakumbuka
nini sasa? Kumbuka hata Yesu alipotoka mlimani baada
ya maombi ya siku 40 shetani alipomjaribu hakurudi mlimani kuomba, bali
alimshinda KWA NENO, kwa kumwambia Imeandikwa… Hivyo
tujizoeze kusoma Neno, kulitafakari na kulihifadhi ndani ya mioyo yetu.
Kuna mambo mengine wala hauitaji
kufunga wala kuomba, UKIWA NA HAZINA NZURI YA NENO TAYARI
UMESHINDA.
10. Kutokua mwombaji.
Maombi ni silaha moja wapo kati ya
nyingi ambazo zinaweza kukusaidia kumpinga shetani. Ukisoma katika Waefeso 5:11 Neno
linasema
“Vaeni
Silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani.”
Moja ya hila ya shetani kwako ni
wewe umtende dhambi. Lakini unapokua mwombaji unaachilia ulinzi wa Mungu katika
maisha yako, na shetani hataweza kukuangusha kirahisi, na kuomba huko uombe kwa
msingi wa Neno, usiombe tu mradi umeomba. Mfno unaweza kuomba sawa na Zaburi 119:37
“Unigeuze
macho yangu nisitazame visivyofaa, unihuishe katika njia yako.”
Macho nayo yameponza wengi kumtenda
Mungu dhambi, ata mwizi aliona kwanza ndipo akaiba. Mzinzi na mwasherati
aliona, akatamani kisha akaanguka dhambini. Pia
ombea miguu yako, ifungiwe utayari katika kupeleka habari njema
za Ufalme, na wala isikumbilie masengenyo wala kupeleka maneno ya uchonganishi
na ufitinishi.
11. Kukinai au kukosa makusanyiko ya watakatifu.
(Waebrania 10:25)
“Wala
tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine, bali tuonyane, na
kuzidi kufanya hivyo, kwa kadri mwonavyo siku ile kuwa imekaribia.”
Katika kukusanyika kama watakatifu,
kuna kufundishana, kuonyana, na kutiana moyo katika changamoto mbalimbali ili
tuweze kuimarika katika Kristo na kudumu katika UTAKATIFU.
MJUE SANA MUNGU ILI UWE NA AMANI, NA NDIVYO MEMA
YATAKAVYOKUJILIA.
Hitimisho
Nipende kusema kuwa si hayo tu bali hayo ni baadhi tu. Yapo mambo mbalimbali na
mazingira yanayoweza kukuangusha dhambini, hivyo tia bidii katika kusoma NENO
LA MUNGU na kufwatilia Watumishi wa Mungu mbalimbali kwa msaada
zaidi. Naomba kuhitimisha katika kitabu cha Yohana 4:34
“Yesu
akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, NIYATENDE MAPENZI yake aliyenipeleka,
nikaimalize kazi yake.”
Chakula ni kitu muhimu sana katika
maisha ya Mwanadamu, huwezi kuishi bila chakula. Yesu akachukulia namna hiyo
kwa kusema “Chakula chake ni kuyatenda mapenzi ya baba
yake.” Yaani kila siku imempasa kutenda mapenzi ya baba yake,
ni bora akose vyote lakini ayatende mapenzi ya baba yake. Kwa maana mapenzi ya
Mungu siku zote ni mazuri na makamilifu, hayana dhambi
ndani yake, bali yamejaa UTUKUFUU NA THAWABU nyingi. Je, mimi
na wewe chakula chetu ni nini? Pia Paulo mtume anatusisitiza haya katika Wafilipi 4:8
“Hatimaye,
ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli,yoyote yaliyo na staha, yoyote yaliyo
ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema,
ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo.”
“NIKUSHUKURU SANA KWAKUA PAMOJA NAMI KATIKA SOMO
HILI, NI OMBI LANGU KWA MUNGU ATUPE NGUVU YA KUISHI MAISHA YA USHINDI DHIDI YA
DHAMBI KATIKA KUISHI KWETU HAPA DUNIANI.“
Post A Comment:
0 comments so far,add yours