Articles by "BIBLE LESSONS"
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo BIBLE LESSONS. Onyesha machapisho yote



Moja ya dhambi zinazowaangusha wengi ni “kutokusamehe”. Na hii inatokana mara nyingi na kutokuelewa nini maana ya msamaha. Ni rahisi kujilazimisha kusamehe lakini kama msamaha haujatoka ndani basi huo sio msamaha.

Ili kuelewa vizuri, tuchukue mfano una mtoto mdogo labda wa umri wa miaka 6 hivi, ukamkuta siku moja kachukua takataka kaweka ndani ya Friji, kwa namna ya kawaida ni lazima utakasirika na kuamua kumuadhibu ili kwamba siku nyingine asirudie…lakini je! Baada ya kumwadhibu utamwekea kinyongo?..Ni wazi kuwa hutamwekea kwasababu unajua ni mtoto tu! Laiti angefikia umri Fulani wa kujielewa asingefanya hivyo. Kwahiyo unamsamehe tu! Kwasababu unaelewa ni utoto tu ndio ulio ndani yake! Ndio unaomsumbua. Huwezi kwenda huku na kule na kwenda kutangaza kila mahali kwamba mwanao ni mbaya na kuanza kumchukia na kumwekea uadui.

Sasa usingeweza kuamua kumsamehe kabisa kutoka ndani ya moyo wako kama usingeelewa sababu ya kina ya yeye kufanya vile. Na ulipogundua kwamba sababu ni UTOTO ndipo ulipoamua kumsamehe kabisa kabisa.

Kadhalika tunapokuwa wakristo hatuwezi kusamehe watu wanaotuudhi au wanaotufanyia ubaya kutoka ndani ya mioyo yetu,kama hatutaelewa sababu ya wao kutufanyia huo ubaya ni ipi.

Leo tutajifunza sababu kubwa ya watu kutufanyia ubaya, au kutuudhi, au kutuumiza, au kutupangia mabaya, au kutuonea au kutufanyia chochote kile ambacho hakistahili kufanyiwa. Ambayo ukiielewa hiyo itakufanya uweze kumsamehe mtu kutoka ndani ya moyo wako kabisa.

Na sababu hiyo si nyingine zaidi ya DHAMBI ndani ya Mtu.

Mtu yoyote ambaye hajampa Bwana Yesu maisha yake, anakuwa ni milki ya shetani asilimia 100, Na kama anakuwa ni milki ya shetani, tunajua matunda ya shetani ndani ya mtu, ni yapi, Mwovu akiwa ndani ya mtu, Yule mtu lazima atakuwa ni mtu wa chuki, ni lazima atakuwa ni mtu wa kiburi, ni lazima atakuwa ni mtu wa hasira, ni lazima atakuwa ni mtu wa matusi, ni lazima atakuwa mtu wa kujipenda mwenyewe na kujijali nafsi yake, na kujiona yeye ni bora kuliko mwingine,ni lazima atakuwa ni mtu wa mashindano, ni lazima atakuwa mtu wa shari siku zote, mtu wa majivuno na wa dharau, na wakati mwingine atakuwa hata muuaji, n.k Kwa ufupi tabia zote mbaya ambazo zinajulikana zitakuwemo ndani ya huyo mtu ambaye hajampa Kristo maisha yake.

Sasa kama vile mtoto anapokosa, moja kwa moja unaelewa kabisa tatizo la Yule mtoto ni UTOTO uliopo ndani yake na laiti kama angekuwa mtu mzima asingefanya vile, Vivyo hivyo mtu yoyote ambaye hajampa Yesu Kristo maisha yake anapokutendea ubaya, anapokuonea wivu, anapokutukana pasipo sababu, anapokudharau, anapotafuta kukuangusha, anapokutegea mitego ya kila aina ili uanguke, anapokuchukia bure, anapokusengenya huku na huku, anapokuonea hasira, anapokuumiza kwa njia yoyote ile n.k Unapaswa uelewa kwamba tatizo sio yeye bali ni DHAMBI iliyo ndani yake, unapaswa uelewe laiti angekuwa Mkristo kweli kweli kama wewe asingefanya vile, laiti angekuwa amempa Bwana maisha yake asingekuwa na chuki,asingekulaani,asingekutukana, asingekuonea wivu n.k…

hivyo sio yeye bali ni ile dhambi iliyo ndani yake, Kama vile unavyoielewa hali ya mtoto mdogo anapofanya kosa vivyo hivyo unapaswa uielewa hali ya Mtu asiye ndani ya Kristo anapokukosea.

Ndio maana pale Kalvari Bwana Yesu hakutusamehe sisi kwasababu tu aliamua kutusamehe, au alituvumilia,hapana! bali alitusamehe kwasababu alijua hatujui tutendalo, Alijua laiti tungemjua yeye ni nani kwa wakati ule Tusengelimsulibisha pale msalabani. Alijua laiti tungefunguliwa macho yetu tusingefanya yale mambo…Hivyo alitusamehe katoka ndani ya moyo wake kabisa.

Sasa ukishindwa kuelewa haya, utajikuta kila mtu anakuwa adui yako, utashinda kuelewa tofauti ya mtu aliye ndani ya Kristo na mtu asiye ndani ya Kristo, utajikuta unakesha katika maombi ya kuangamiza maadui zako, utajikuta na wewe unaanza kulipiza mabaya badala ya mema. Utajikuta na wewe shetani amekuingia unaanza kuwa na chuki, unaanza kuwa msengenyaji, unaanza kulipiza visasi n.k

Hakuna sababu ya mtu kuwa adui yako, anapokutukana, hakuna sababu ya mtu kuwa adui yako anapokusengenya, hakuna sababu ya mtu kuwa adui yako anapokuchukia, hakuna sababu mtu kuwa adui yako anapokusaliti, hakuna sababu mtu kuwa adui yako anapokutendea ubaya wowote ule, kwasababu unaelewa kabisa kwamba tatizo sio Yule mtu, TATIZO NI DHAMBI ILIYOPO NDANI YAKE, laiti angekuwa mkristo kweli kweli asingefanya vile, hivyo unachopaswa kufanya ni kuchukua hatua ya wewe kumwombea Bwana ampe wokovu ili Dhambi hizo ziondoke ndani yake, lakini sio kushindana naye…Kwasababu ukishindana naye huwezi kumbadilisha kuwa kama wewe, wala hawezi kuvutiwa na kile kilichoko ndani yako. Suluhisho pekee ni kumwombea Rehema na Neema mbele za Mungu.

Ndugu jifunze kusamehe kutoka ndani ya moyo, kwa kuelewa hali ya mtu aliyopo. Kama kuwa na maadui hakuna mtu aliyekuwa na maadui kama Bwana wetu Yesu Kristo, na maadui zake namba moja tulikuwa ni mimi na wewe. Tulimtemea mate…je! wewe katika maisha yako ulishawahi kutemewa mate kama yeye?.. tulimtukana na kumdhihaki, na zaidi ya yote tukampeleka msalabani na kumwaibisha..je! wewe katika maisha yako ulishawahi kuaibishwa hivyo? Lakini yeye hakuwahi kutuita sisi maadui zake.. zaidi sana alisema “Baba wasamehe kwa kuwa hawajui watendalo” na zaidi ya yote akatuita sisi tuliokuja kumwamini baadaye rafiki zake.

Kama Bwana Yesu alitusamehe madeni makubwa kama hayo, unadhani sisi tunapaswa tuwafanyieje wanaotukosea?..tunapaswa tufanye zaidi ya hapo. Bwana alisema mwenyewe kwamba sisi tusipowasamehe waliotukosea hata Baba yetu wa mbinguni hatatusamehe makosa yetu. Ikiwa na maana kuwa kama kuna mtu yoyote ambaye hatujamsamehe kwa dhati kabisa kutoka ndani ya mioyo yetu, na sisi hatutasamehewa dhambi zetu, hivyo ni ziwa la moto litakuwa linatungoja, na Kristo hawezi kuzungumza uongo.

Ndugu yangu, epuka maombi yakupiga maadui zako, epuka kupeleka mashtaka mabaya mbele za Mungu juu ya watu wanaokuudhi, au kukuumiza, usimtaje ndugu yako kwa ubaya mbele za Mungu, wala usimtakie shari, bali mwombee rehema..ili atubu awe mkamilifu, Biblia inasema katika.

Mithali 24: 17 “Usifurahi, adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo; Bwana asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake”. 


Unaona? Hapo Bwana hafurahii, kuanguka kwake mtu mwovu, wala hafurahii mashataka mabaya tunayompelekea dhidi ya watu wengine, maombi tunayopaswa kuomba mbele zake ni Bwana atuepushe na madhara yao lakini sio awapige, au awaue, au awalaani. Adui yetu mkubwa ni shetani na sio watu.

Ni maombi yangu kuwa Bwana atakupa Moyo wa Rehema na Toba dhidi ya ndugu wanaotukosea.

Ubarikiwe sana.


chanzo:https://wingulamashahidi.org/2018/11/20/samehe-kutoka-ndani-ya-moyo-wako/


Bila ya kuwa na maono ya wapi unaelekea ni rahisi kuchukuliwa na upepo na kupelekwa usikokutazamia. Maono yatakufanya ujue ni nini ufanye kwa ajili ya Mungu na maisha yako kwa ujumla.

Mithali 29: 18 

Maono yako kwa ajili ya kazi ya Mungu ni lazima yaendane na agizo kuu alilolitoa Bwana Yesu kwa wote wanaomwamini.

Marko 16:15 Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe.

Ni lazima mara zote agizo hili liwe ndani yako ili unapoendelea na maono yako usijeenda mbali na agizo hili.

Shetani hujaribu kuyafisha maono yako na usipokuwa mwangalifu atayapoteza kabisa. Yeye mara zote hutaka kituzuia kuyafanya mapenzi ya Mungu, anajua akiyaua maono yetu hatutaweza kuifanya kazi ya Mungu kwa ukamilifu.

2Korintho 2:11 Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.

Mambo yafuatayo shetani huyatumia kuua maono yetu:

1. Dhambi ambazo hazijatubiwa
Isaya 59:9-12 Mistari hii inaonyesha kuwa dhambi isipotubiwa hupofusha macho ya rohoni hivyo hutaweza kuyaona maono yako. Dhambi inakuweka mbali na utukufu wa Mungu.

2. Uhusiano uliovinjika katika mwili wa Kristo 
Tunaporuhusu makosa ya ndugu zetu katika Kristo kuzaa uchungu badala ya kusamehe, tunaruhusu shetani kuyafunga macho yetu ya kiroho na hivyo kushindwa kuiona njia ya kuelekea kwenye maono yetu.

3. Tamaa ya mambo yanayoonekana

Zaburi 119:37 Unigeuze macho yangu nisitazame yasiyofaa, unihuishe katika njia yako.

Ukiangalia sana mambo ya dunia na tamaa zake utajikuta unayasahau maono yako na kubaki umefungwa na mambo hayo.

4. Kuangalia sana mambo ya nyuma.

 Unapoacha kutazama mbele unapoelekea na kuweka nguvu na akili yako yote katika mambo ya nyuma yaliyopita, utapoteza kusudi lako na maono yako.

Mwanzo 19:26 Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.

Wafilipi 3:13 Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele.

5. Kutumia muda mwingi kuangalia matatizo

Shetani hujaribu kutufanya tuangalie tu matatizo tuliyonayo na yale yanayoweza kutokea tunapoyafanyia kazi maono yetu hivyo kutuondolea imani ya kuyakamilisha. Biblia katika kitabu cha hesabu inaelezea habari za wapelelezi kumi waliorudi na habari za kukatisha tamaa katika kuiendea nchi ya ahadi maana waliangalia zaidi matatizo na kupoteza maono yao ya kuingia nchi ya ahadi.

Joshua na Kaleb waliona zaidi ya matatizo, waliuona ukuu na uaminifu wa Mungu. Hawakuwa na hofu yoyote hivyo waliweza kuingia nchi ya ahadi (kukamilisha maono yao) maana walimwamini Mungu. Petro alijaribu kutembea juu ya maji lakini alipoona mawimbi akasahau Yesu aliyekuwa mbele yake akimwambia njoo, akaweka akili kwenye mawimbi akaanza kuzama.

Ili tuweze kuyafanikisha maono yetu ni lazima tuwe na uhusiano na ushirika wa karibu na Roho Mtakatifu.

Ubarikiwe na BWANA Yesu.




 chanzo: https://womenofchrist.wordpress.com

Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. —YEREMIA 29:11

Iwapo una picha mbaya binafsi kujihusu, tayari imeathiri vibaya mambo yake ya kale, lakini unaweza kuponywa na kutoruhusu ya kale kujirudia. Ninakuhimiza kusahau yaliyopita hata mambo yoyote hasi ambayo umehisi kujihusu na kujisukuma mbele kuelekea vitu ambavyo Mungu amekuwekea.

Mungu ana mpango mwema na kusudi kwa kila mmoja wetu na njia maalum na wakati mtimilifu wa kuyafanya yatimie, lakini sio sisi wote tunayaona haya. Wakati mwingi tunaishi chini ya kiwango cha maisha ambayo Mungu anakusudia tufurahie.

Kwa miaka mingi sikutumia haki na faida zangu kama mwana wa Mungu. Ingawa nilikuwa Mkristo na kuamini nitaenda mbinguni nitakapofariki, sikujua kwamba kuna jambo ambalo lingefanywa kuhusu maisha yangu yaliyopita, yaliyopo na yajayo. Nilikuwa na picha mbaya kujihusu, na ikaathiri maisha yangu ya kila siku, pamoja na mwono wangu wa siku zijazo.

Leo unaweza kukubali upendo wa Mungu juu yako na uufanye upendo wake msingi wa kujipenda na kujikubali. Pokea hakikisho lake, ukijua kwamba unabadilika na kuwa vile anavyotamani uwe. Halafu uanze kujifurahisha—ulipo—ukiwa njiani kuelekea ukomavu mkamilifu wa kiroho.

Acha Mungu awe Mungu katika maisha yako. Mweke katika kiti cha dereva. Anajua analofanya.

 

Umngoje Bwana, uwe hodari, upige moyo konde, naam umngoje Bwana. —ZABURI 27:14

Tukimngoja Mungu, hatuwi wavivu au kukosa kujishughulisha, lakini kwa kweli tunajishughulisha kabisa kiroho. Huenda tusiwe “tunafanya” kitu, lakini tunamwamini Mungu kufanya yanayohitajika kufanywa. Kwa maneno mengine, tunasema, “Bwana, sitajaribu kufanya haya kwa nguvu zangu. Nitakungoja uniokoe. Na nitaendelea kufurahia maisha yangu huku nikikungoja.”

Shetani anataka tusikitike kutokana na kujaribu kutatua matatizo yetu wenyewe. Anachukia furaha yetu. Anataka kuona kitu kingine lakini si furaha, kwa sababu furaha ya Bwana ni nguvu zetu (Nehemia 8:10). Wasiwasi huiba furaha yetu, lakini furaha hututia nguvu.

Huwa tunajaribiwa kufikiri hatufanyi yanayotupasa kufanya tusipokuwa na wasiwasi au kutafuta jibu la matatizo yetu, lakini hili litazuia wokovu wetu badala ya kuusaidia. 

Si kutowajibika kufurahia maisha huku tukimngoja Mungu na kumtarajia kufanya kile tusichojua kukifanya!

Usihofu kwa kuwa vita si vyako, ni vya Bwana.


Author: Joyce Meyer
Source: https://tv.joycemeyer.org/kiswahili/devotional/kungoja-mungu/
Na Mwl Deborah Lema
UTANGULIZI
Upo umuhimu wa kumjua Mungu, kabla ya kuanza kumwabudu, kabla ya kuanza kumtegemea, kabla ya kuanza kumtumikia, kabla ya kuanza kumuomba, kabla ya kuanza kumtangaza au kutangaza habari zake kwa mataifa.
Kwanza kabisa tutambue Mungu ni ROHO. Sawa na (Yohana 4:24) “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo imewapasa kumwabudu katika roho na kweli”Hivyo usijedanganyika na hao binadamu wanaojiita Mungu. Au wengine huchonga sanamu na Kusema ni Mungu.
Sifa kuu ya Mungu yupo kila mahali Ndio maana lolote unalolifanya liwe jema au baya anakuona, huwezi kumficha chochote au kumkimbia. Kasome kitabu cha (Yona 1:1-). Lakini hufanya makao mahali patakatifu.Hafanyi makao katika mapango ya wanyang’anyi.
Hivyo ukitaka Mungu afanye makao ndani yako dumu katika utakatifu
Baada ya kuangalia MUNGU ni nani, na baadhi ya sifa Zake kwa uchache, pia tutazame Huyu Mungu je, Anajidhihirishaje!? Au anaonekanaje?
Eneo hili ni pana, ntaeleza kwa uchache kadri Mungu atakavyoniwezesha. Nianze kwa njia ya ISHARA. kipindi cha Musa Mungu alijifunua kwa Musa kwa ishara mbalimbali. Tukisoma Kutoka 4:2-3
“BWANA akamwambia, ni nini hiyo uliyonayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo, Akamwambia itupe chini, akaitupa chini, nayo ikawa nyoka, Musa akakimbia mbele Yake” Tukiruka mstari wa 4 twende mstari wa 5 anasemaje?
“Ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, MUNGU wa Ibrahim, MUNGU wa Isaka, MUNGU wa Yakobo AMEKUTOKEA”
Kwa kutokujua njia au namna mbalimbali ambazo Mungu hujidhihirisha au huonekana kwetu tunashindwa kujua au kutenda yatupasayo. Kuna wengine husubiri mpaka aje malaika kavaa nguo nyeupe, au ngurumo kubwa Ndio ajue ni Mungu. Lakini kumbe zipo njia nyingi na nyingine za kawaida lakini katika ukawaida huo MUNGU hujidhihirisha ni yeye anasema nawe, au ni yeye ameruhusu jambo fulan n.k
Hivyo usiwe mtu wa kupuuzia baadhi ya Ishara mbalimbali zinazofunuliwa kwako, wakati mwingine hutasikia Sauti bali kwa ishara Utajua Mungu anasema nini.
Mungu hujidhihirisha kwa sauti ya waziwazi
Kumbe pia Mungu hujidhihirisha kwa sauti ya waziwazi kama vile mtu anavyomsikia mtu akiongea, Mungu Pia anaweza sema nawewe Kwa sauti ya waziwazi.
Tusome 1 Samweli 3:10-11
“BWANA akaja,akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli ! Samweli ! Akasema nena BWANA kwakua mtumishi wako anasikia. BWANA akamwambia Samweli, Angalia nitatenda tendo katika Izraeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha”
Ukisoma 1 Samweli 3:4-9
Mungu alipoanza kumuita Samweli au Kasema nae Samweli hakujua ni Mungu, akadhani ni Eli, mara zote tatu BWANA alipomuita alikimbilia kwa Eli akidhani ndie anayemuita, hadi mara ya tatu Eli alipotambua anayemuita Samweli ni Mungu mwenyewe. Ndipo akamwambia Samwel aseme hivi …Nena BWANA kwakua mtumishi wako anasikia…
Je, Mungu amewahi kusema nawewe Kwa sauti ya waziwazi? Kama ndio ulijuaje ni Mungu? Au kwakua hukumuona anaekuita? . Na kama utajibu hapana, una uhakika? Au hujui yule anayekusemeshaga ndie Mungu? Au ukisikia sauti huoni mtu huwa unakemea? Lakini ni vizuri kuwa mwangalifu tena sana, kwani shetani nae anaweza kusema nawe kwa sauti
MFANYE MUNGU RAFIKI, SEMA NAE MARA KWA MARA UTAJIKUTA SIKU MOJA ANAKUJIBU UNAMSIKIA, ILA UTAKATIFU UNAHITAJIKA.
Tuambatane sote sehemu ijayo…




Na Mwl Deborah Lema
Je, Mungu amewahi kusema nawewe Kwa sauti ya waziwazi? Kama ndio ulijuaje ni Mungu? Au kwakua hukumuona anaekuita?. Na kama utajibu hapana, una uhakika? Au hujui yule anayekusemeshaga ndie Mungu? Au ukisikia sauti huoni mtu huwa unakemea? Lakini ni vizuri kuwa mwangalifu tena sana, kwani shetani nae anaweza kusema nawe kwa sauti. 
 Mungu hujidhihirisha kupitia Neno lake
Biblia imejaa majibu, mwongozo, masahihisho na jumla ya taratibu zote juu ya maisha ya mwanadamu. Yani katika dunia hii hakuna jipya, yote yalishaandikwa. Lakini tutajuaje ikiwa hatusomi neno?
Huwa inatokea mtu anapata wazo, au anasukumwa juu ya jambo fulani lakini anabaki njia panda. Lakini punde asomapo neno au mtumishi wa Mungu akasimama kuhudumia watu anaanza kushangaa imekuaje? Maana Yale yanayonenwa yanagusa maeneo yale yale. Kumbe ni Mungu amejidhihirisha kupitia neno lake. Hakuna neno katika Bíblia lisilo na maana, tusome…
2 Timotheo 3:16

Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadabisha katika haki;

Ni dhahiri Neno la Mungu lina pumzi ya Mungu ndani yake. Linaishi. Halikadhalika katika yote tunayopitia, Mungu hujidhihirisha kupitia neno lake.
Tuamue tu sisi kutoona ama kufumbia macho, lakini majibu yetu hupatikana katika neno lake. Ni jumumu letu kusoma na kuomba Roho Mtakatifu atusaidie kuelewa maana kusoma tu haitakusaidia kama hautaelewa.
Unajua unachotakiwa kufanya unapokutana na jambo lolote? Ni kulijua neno la Mungu.Tazama hapa
Marko 12:24

Yesu akajibu, akawaambia, Je! Hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu?

Mathayo 22:29

Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.

Maandiko hayo yadhihirisha ya kwamba, ikiwa tunayajua maandiko, basi tutakuwa tunajua uweza wa Mungu. Na katika kujua uweza wa Mungu, basi tutaona anavyojidhihirisha kwetu mara zote – kupitia Neno lake.
Jipangie muda kila siku wa kusoma neno la MUNGU kwa msaada wa Roho Mtakatifu.
Baada ya kuona sehemu ya tano vile Mungu anaweza jidhihirisha kupitia neno lake na tukashuhudiwa ndani na nje.
Mungu anavyojidhihirisha kwa kuachilia mzigo ndani unaoleta matokeo chanya nje.
Natamani unielewe na kwa pamoja tumzalie BWANA matunda katika Hili. Wako wengi Sana Mungu anawasukuma kufanya vitu mbalimbali lakini hawavifanyi kwakudhani havitafanikiwa au watachekwa au watawezaje. Tusome habari za Dorkasi katika Matendo 9:36-43
Habari hii kwa wasomaji wa neno si habari geni kwao .Sitasoma mistari yote, Naomba kusoma mstari wa 39 Unasema hivii…
“Petro akaondoka akafuatana nao, Alipofika wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, WAKILIA NA KUMWONYESHA ZILE KANZU NA NGUO ALIZOZISHONA DORKASI wakati ule alipokua pamoja nao”
Sifa kuu ya jambo la ki Mungu halinaga matokeo hasi, labda ukute ulijichanganya mwenyewe katika kulielewa au katika kulitendea kazi. Mungu anaweza kujidhihirisha kuwa ni yeye kupitia matokeo chanya yatakayo kuja baada ya kutendea kazi ule mzigo uliopewa ndani.Dorkasi kazi Yake ilimgusa Mungu, na hata baada ya yeye kufa wajane hawakuona aliyeziba pengo Lake, hivyo hawakua tayari kumzika. Lakini yote ni kwa sababu ya matokeo chanya ya ule mzgo uliokua ndani yake.
Mungu alijidhihirisha Kuwa anatambua thamani yake duniani na ndipo akarudishiwa uhai wake.
Wangapi wanakufa tunakimbilia kuwazika? Je, unadhani ukifa leo watu watagoma kukuzika watake urudi? Kama ndio kwa lipi? Na kwa hilo ni kwa wanadamu au linamgusa Mungu? Hata mimi najaribu kujibu haya maswali maana yananihusu pia.
Nimejaribu kueleza kwa uchache vile Mungu anajidhihirisha ingawa Bado zipo namna nyingi zaidi ambazo Mungu hujidhihirisha ikiwemo kwa njia ya maombi na kadhalika. Tuhitimishe kwa kuona je, MUNGU ANAPATIKANA WAKATI GANI?
Ni kweli Mungu yupo wakati wote lakini Hii zaburi yasemaje hapa?
ZABURI 32:6
“Kwa hiyo kila mtu mtauwa akuombe WAKATI UNAOPATIKANA, hakika maji makuu yafurikapo hayatamfikia yeye”
Kuna wakati unaakili zako Timamu, unaelewa, unasikia na Unajua Kama si kufahamu wajibu wako sahihi mbele za Mungu ambao ukiutekeleza unapokea haki yako. Lakini ubaya tuna tabia ya kusubiri maji yatufike shingoni Mambo hayaendi, kila njia imeshindikana Ndio tunarudi kwa Mungu kwa machozi, lakini kumbe muda wa kumuhusisha Mungu tulikua nao na tukaacha. Lakini tunataka tumtafute Mungu kwa dharura, hicho kitu hakipo.
Wekeza kwa Mungu, tumia hicho kipawa chako kumtumikia Mungu, tumia pesa zako,wakati huu ambao una akili timamu tumika , unaijua kweli, una nguvu ya kumtumikia , unauwezo wa kwenda ibadani, huu Ndio wakati wako au huu Ndio wakati tunaoweza kusema MUNGU ANAPATIKANA KWAKO
USISUBIRI MAMBO YAKUHARIBIKIE, USISUBIRI UWE MAUTIUTI KITANDANI, USISUBIRI UVUNJIKE MIGUU NA MIKONO NDIO UMWENDEE MUNGU KWA MACHOZI BAADA YA SHETANI KUKUCHAKAZA, WAKATI MUNGU ANAPATIKANA KWAKO NI SASA
ASANTE KWA KUWA PAMOJA NAMI KATIKA KUJIFUNZA HAYA



Na Mwalimu Deborah Lema.
delechansie@gmail.com

UTANGULIZI.
Lazima tujue mazingira au ushawishi unaoweza kumsababisha mtu atende dhambi au amkosee Mungu. Si kila mahali au kija jambo linaweza kukutoa katika uwepo wa Mungu, ila yapo mambo au mazingira ambayo humpelekea mtu kutenda dhambi, iwe kwa kudhamiria au kwa nguvu ya ushawishi. Na pia si kila mtu anayetenda dhambi kwamba anafurahia, hata makahaba na walevi wa kupindukia tunaowaona si wote wametaka au wanafurahia hali zao, ila kuna mazingira yanayowapelekea kuwa hivyo walivyo. Katika Warumi 7:15 inasema
“Maana sijui nifanyalo, kwasababu lile nilipendalo, silitendi, bali nilichukialo ndilo ninalolitenda.”
Unaweza ukatamani sana sana kumpendeza Mungu na kukaa uweponi mwake wakati wote, lakini kila ukijitahidi unashindwa, unashangaa mara limetokea hili na lile umemtenda Mungu dhambi. Na yale ambayo hupendi wala huyawazii kuyatenda ndiyo unaanza kuyatenda kila siku, Je, ni kwa nini sasa? Ni mambo gani yanasababisha uwe mtu wa kuanguka dhambini kila mara?
1. Kutokuwa na Msingi wa Neno la Mungu.
Kutokujihusisha na neno la Mungu humaanisha ya kwamba kuna mwongozo mwingine unaotegemea katika maisha yako ambao kwa hakika lazima utaangukia DHAMBINI TU.
Daudi anaandika katika
Zaburi 119:105

Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.
Tunapojikita katika kusoma Neno la Mungu tunapata kufunuliwa mambo kadha wa kadha na kukaa uweponi mwa Mungu, na kinyume chake ni kuyumbishwa katika upepo wa kila namna. Katika Hosea 4:6 Neno linasema
“Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe…”
Neno la Mungu linakutosheleza katika kutimiza mahitaji yako ya kila siku na wakati huo huo kutulia uweponi mwake katika hali ya Utakatifu, Lakini kwa kukosa/kukinai neno tunaangukia dhambini.
2. Hasira.
Hasira imepelekea watu kujiua, kufukuza wake zao au waume zao, kutukana, kufanya vurugu na maovu mengineyo. Na kwakutambua hilo Biblia haikuacha kusema hilo ndio maana katika Waeféso 4:26 inasema
“Mwe na hasira, ila MSITENDE DHAMBI, jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka.”
Ni kweli huwezi ukazuia hasira, na haikwepeki, kuna mambo yanakera kabisa, ikiwemo ya mambo ya kusingiziwa, n.k lakini bado tunapewa onyo HASIRA HIZO ZISITUPELEKEE kumtenda Mungu dhambi. Epuka kufanya jambo au maamuzi yoyote ukiwa na hasira, hyo itakusaidia usitende dhambi.
3. Kuongozwa na mwili.
Maandiko yanasema siku zote nia ya mwili ni mauti, usitegemee hata siku moja mwili wako utakusukuma kumpendeza Mungu. Hujawai ona kuna kitu unasukumwa sana kukifanya ndani lakini mwili wako hautaki kabisa? Je, hatujawahi kusoma kuwa Roho i radhi lakini mwili ni dhaifu? unaweza ona vile mwili unapingana na mapenzi ya Mungu. Katika Wagalatia 5:16 Neno linasema
“Basi nasema, ENENDENI KWA ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.”
Mwili siku zote umejawa na tamaa, pia hapo hapo neno linasema tamaa ni dhambi, tunaweza ona vile ilivyo muhimu kuenenda katika Roho na kuongoza na Roho katika mambo yote.
NA SI ROHO TU, BALI ROHO MTAKATIFU, KWANI KUNA ROHO YA SHETANI PIA.
4. Ushawishi wa wenye dhambi.
Usitegemee mtu aliyezoelea dhambi akakushawishi wewe mazuri ya kumpendeza Mungu, yawezekana wewe kimbilio lako la kwanza ni kutaka ushauri au kuambatana na watenda dhambi, sasa lazima ipo siku watakuangusha dhambini tu. Katika Mithali 1:10 Inasema
“Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, wewe usikubali.”
Mungu anajua kabisa wenye dhambi ni watu wenye kushawishi wengine kuanguka nao dhambini, na kamwe hawawezi kukuelekeza katika njia ya haki, hujawahi ona kama ni mlevi anamshawishi mtu asiyemlevi akimwambia, “onja tu kidogo”? hayo yote ni ushawishi wa wewe kuanguka dhambini. Kuna mazingira ya ushawishi unaweza ukayaepuka, na kama hayaepukiki basi JENGA MSIMAMO UNAPOSHAWISHIWA USIKUBALI.
5. Majaribu.
Majaribu ni kizuizi au kifungo fulani katika maisha ya mtu. Na watu wengi wameshindwa kuwa wavumilivu kusubiri wakati wa Bwana na kuamua kupita njia za mkato. Kuna wengine kwa kukosa kazi muda mrefu, wamekua tayari kuuza miili yao au kutoa rushwa za namna nyingine ili mambo yao yaende vizuri, wakisahau Wanamtenda Mungu dhambi kwa ajili ya mambo ya kitambo. Lakini Neno lasemaje katika Ufunuo 2:10 Inasema
“Usiogope mambo yatakayokupata, tazama, huyo ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakua na dhiki siku kumi, UWE MWAMINIFU HATA KUFA, NAMI NITAKUPA TAJI YA UZIMA.”
Mkazo wangu ni hapo nilipoandika kwa herufi kubwa, ya kwamba tuwe waaminifu katika kumtazama Mungu, haijalishi tunachoka na kuumia kiasi gani, tuwe waaminifu mpaka kufa, wala shida na taabu hizo zisitufanye tumtende Mungu dhambi.
KILA JARIBU UNALOPITIA LINA MLANGO WA KUTOKEA, WALA LISIKUSABABISHE UMTENDE MUNGU DHAMBI.
6. Kuendekeza mizaha.
Mizaha na utani vimesababisha wengi kupigana, kuchomana visu, na vurugu za namna mbalimbali. Wengine wameshindwa kustahimili hasira za mizaha wakaangukia katika matusi na visa. Katika Zaburi 1:1
“Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki, wala hakusimama katika njia ya wakosaji, WALA HAKUKETI BARAZANI PA WENYE MIZAHA.”
Biblia inamuita mtu asiyeketi barazani pa wenye mizaha kuwa HERI kwake. Maana katika mizaha kuna mengi, na shetani hutumia njia hiyo kupoteza wengi, wengine siku ya tar 1/4 wanaiita sikukuu ya wajinga, wanaitumia kudanganyana, hivi mfano Mungu akishuka siku kama hiyo umeshadanganya watu kwa mzaha mzaha hatahesabu uongo huo kama dhambi? Au uongo wa siku hiyo sio dhambi? Msisitizo wangu ni kuwa makini na mizaha, usiipe kipaombele sana, kwani ni mlango wa wazi sana ambao shetani huutumia kupotosha wengi.
7. Kulewa vitu (ulevi wa vitu).
Ulevi si lazima iwe pombe, unaweza ukapata kitu kikakulewesha akili zako zote na mategemeo yako yote yakahamia hapo. Kuna watu walimlilia Mungu kwa ajili ya kazi au kupandishwa vyeo baada ya kupata walivyoomba wakaaza kulewa kwavyo. Na matokeo ya kulewa huko ni kutenda dhambi kuona huitaji kingine chochote uko huku kufanya unachojisikia, ile hofu ya Mungu haipo tena kwani ulikua nayo kipindi cha uhitaji, baada ya kupata ukajisahau. Katika 1 Wafalme 11:4 neno linasema
“Maana ikawa, Sulemani alipokua mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.”
Tunaweza kusema kuwa Sulemani alijichimbia kaburi la uharibifu mwenyewe, alifika mahali akaona anajitosheleza kwa kila kitu,akajitwalia wanawake wengi kadri alivyoweza huo ndio ukawa ulevi wake. Na mwishowe alimtenda Mungu dhambi kwa kuigeukia miungu mingine.
UNYENYEKEVU ULIOKUA NAO WAKATI WA DHIKI ISIFIKE WAKATI UKAJISAHAU UONE UMEFIKA, KUANGUKA KU KARIBU KULIKO KUINUKA.
8. Kukosa Nguvu za Roho Mtakatifu.
Kamwe akili zetu, wala fahamu zetu haziwezi kutusaidia tusimtende Mungu dhambi, ila tukiwa na Nguvu za Roho Mtakatifu sawa na Matendo 1:8tutaweza. Yesu mwenyewe alitambua hatuwezi ndio maana akatuachia msaidizi. Katika Yohana 14:16-17 Inasema
“Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele, ndiye Roho wa kweli, ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui, bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakua ndani yenu.”
Roho Mtakatifu ndiye pekee anayeweza kumsaidia mtu asitende dhambi. Ataachilia hofu ndani yako, (hofu ya kumuhofu Mungu), pia ataongoza hatua za miguu yako yaani uende wapi na usiende wapi, pia atakupa maneno ya kuzungumza au kutamka, ukiwa na nguvu za Roho Mtakatifu hauwezi kuwa mropokaji wa ovyo wala mtukanaji, kwa maana hata maneno ya kinywa chako yataratibiwa naye.
SISEMI KWA HABARI YA ROHO MTAKATIFU, BALI NASEMA KWA HABARI YA NGUVU ZA ROHO MTAKATIFU, MAANA KAMA NI KUJAZWA ROHO MTAKATIFU WENGI WALISHAJAZWA LAKINI BADO WANAENDELEA NA DHAMBI. (Matendo 1:8)
9. Kukosa hazina ya Neno la Mungu moyoni mwako.
Kuna watu au niseme kuna Wakristo ambao hawana Neno kabisa, yaani mtu akisoma Biblia anasoma kama gazeti, hana muda wa kulitafakari, hana muda wakupata mafunuo juu ya neno, hana muda wakulihifadhi yaani yupo tu. Ikatokea umemnyang’anya Biblia basi kwisha habari yake. Lakini mtunzi wa Zaburi 119:11 Anasemaje?
“Moyoni mwangu nimeliweka Neno lako, nisije NIKAKUTENDA DHAMBI.”
Kumbe Neno ndani ya moyo wake ndiyo kinga au kengele ya kumwongoza katika njia zake. Unapokua na Neno la Mungu ndani ya moyo wako unapojaribiwa kutenda dhambi daima litakukumbusha yaliyo mapenzi ya Mungu kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Lakini kama huna Neno utakumbuka nini sasa? Kumbuka hata Yesu alipotoka mlimani baada ya maombi ya siku 40 shetani alipomjaribu hakurudi mlimani kuomba, bali alimshinda KWA NENO, kwa kumwambia Imeandikwa… Hivyo tujizoeze kusoma Neno, kulitafakari na kulihifadhi ndani ya mioyo yetu.
Kuna mambo mengine wala hauitaji kufunga wala kuomba, UKIWA NA HAZINA NZURI YA NENO TAYARI UMESHINDA.
10. Kutokua mwombaji.
Maombi ni silaha moja wapo kati ya nyingi ambazo zinaweza kukusaidia kumpinga shetani. Ukisoma katika Waefeso 5:11 Neno linasema
“Vaeni Silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani.”
Moja ya hila ya shetani kwako ni wewe umtende dhambi. Lakini unapokua mwombaji unaachilia ulinzi wa Mungu katika maisha yako, na shetani hataweza kukuangusha kirahisi, na kuomba huko uombe kwa msingi wa Neno, usiombe tu mradi umeomba. Mfno unaweza kuomba sawa na Zaburi 119:37
“Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, unihuishe katika njia yako.”
Macho nayo yameponza wengi kumtenda Mungu dhambi, ata mwizi aliona kwanza ndipo akaiba. Mzinzi na mwasherati aliona, akatamani kisha akaanguka dhambini. Pia ombea miguu yako, ifungiwe utayari katika kupeleka habari njema za Ufalme, na wala isikumbilie masengenyo wala kupeleka maneno ya uchonganishi na ufitinishi.
11. Kukinai au kukosa makusanyiko ya watakatifu. (Waebrania 10:25)
“Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine, bali tuonyane, na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadri mwonavyo siku ile kuwa imekaribia.”
Katika kukusanyika kama watakatifu, kuna kufundishana, kuonyana, na kutiana moyo katika changamoto mbalimbali ili tuweze kuimarika katika Kristo na kudumu katika UTAKATIFU.
MJUE SANA MUNGU ILI UWE NA AMANI, NA NDIVYO MEMA YATAKAVYOKUJILIA.
Hitimisho
Nipende kusema kuwa si hayo tu bali hayo ni baadhi tu. Yapo mambo mbalimbali na mazingira yanayoweza kukuangusha dhambini, hivyo tia bidii katika kusoma NENO LA MUNGU na kufwatilia Watumishi wa Mungu mbalimbali kwa msaada zaidi. Naomba kuhitimisha katika kitabu cha Yohana 4:34

“Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, NIYATENDE MAPENZI yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.”
Chakula ni kitu muhimu sana katika maisha ya Mwanadamu, huwezi kuishi bila chakula. Yesu akachukulia namna hiyo kwa kusema “Chakula chake ni kuyatenda mapenzi ya baba yake.” Yaani kila siku imempasa kutenda mapenzi ya baba yake, ni bora akose vyote lakini ayatende mapenzi ya baba yake. Kwa maana mapenzi ya Mungu siku zote ni mazuri na makamilifu, hayana dhambi ndani yake, bali yamejaa UTUKUFUU NA THAWABU nyingi. Je, mimi na wewe chakula chetu ni nini? Pia Paulo mtume anatusisitiza haya katika Wafilipi 4:8
“Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli,yoyote yaliyo na staha, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema, ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo.”
“NIKUSHUKURU SANA KWAKUA PAMOJA NAMI KATIKA SOMO HILI, NI OMBI LANGU KWA MUNGU ATUPE NGUVU YA KUISHI MAISHA YA USHINDI DHIDI YA DHAMBI KATIKA KUISHI KWETU HAPA DUNIANI.“