Hatua ya
kuweka akiba, ni matokeo ya maamuzi. Akiba ni matokeo ya maamuzi ya kuweka vitu
sasa, kwa ajili ya kuvitumia baadaye. Ukiona mtu anaweka akiba, ujue
anatekeleza maamuzi yake, yanayogusa nyakati mbili za Maisha, nyakati ya sasa
na nyakati ya baadaye.
Kwa
hiyo, haina maana ya kwamba, vitu unavyoamua kuviweka akiba sasa, kwa ajili ya
kuvitumia baadaye, huna kazi navyo sasa – la hasha! Lakini sababu ya kutumia
vitu hivyo baadaye, ni kubwa kiumuhimu, kuliko sababu ya kuvitumia sasa!
Hebu
tujifunze zaidi juu ya hekima hii, kwa kuangalia mifano ifuatayo:
Mfano 1:
Sababu zilizomfanya Mfalme Daudi aweka akiba.
Ukisoma
1 Mambo ya Nyakati 29:2 utaona mfalme Daudi akisema hivi: “nimeiwekea akiba
nyumba ya Mungu wangu…”. Sababu yake ya kuiwekea akiba nyumba ya Mungu,
tunaipata tunaposoma alichosema mfalme Daudi kwenye 1 Mambo ya Nyakati 29:3,
aliposema hivi: “Nami tena kwa kuwa nimeiwekea nyumba ya Mungu wangu shauku
yangu…”
Mfalme
Daudi alitaka waliokuwa wanamsikiliza, wajue ya kuwa, vitu alivyoviweka akiba
kwa ajili ya nyumba ya Mungu, aliviweka akiba, si kwamba hakuwa na shida wakati
ule, iliyohitaji matumizi ya vitu vile. La hasha!
Ila
“Shauku” au “Sababu” ya kuona nyumba ya Mungu wake inajengwa, ilikuwa kubwa
kiumuhimu, kuliko kuvitumia wakati ule. Na tena – hakutaka mrithi wake yaani
Sulemani, aliyepewa jukumu la kuijenga nyumba hiyo, aje awe na tatizo katika kupata
vitu vya kuanzia kuijenga nyumba ile.
Mfalme
Daudi alisema “katika shida yangu, nimeiwekea akiba nyumba ya Bwana…” (1 Mambo
ya Nyakati 22:14). Hii inaonyesha ya kuwa alifanya maamuzi ya kuweka akiba
akiwa katika mazingira ya “shida”. Lakini moyoni mwake kulikuwa na Shauku kubwa
ya kuona nyumba ya Mungu wake inajengwa, kiasi cha kuishinda sauti ya “shida”
iliyokuwa “inalia” moyoni mwake, kutaka kutumia vitu vile vile alivyoamua
kuviweka akiba!
Je,
ndani ya moyo wako kuna shida inayolilia kuvitumia vitu ulivyonavyo, ambavyo
pia ulitaka kuviweka akiba kwa ajili ya kuvitumia baadaye? Je, ni sauti ipi
inayoshinda? Ni ile ya kuvitumia katika shida uliyonayo sasa, au ni ile
inayotaka uviweke akiba kwa ajili ya kuvitumia “baadaye”?
Je,
unaweza kuikubali “hekima” hii ya mfalme Daudi? Pamoja na shida aliyokuwa nayo,
wakati ule alipokuwa anaweka akiba, aliona ni vema kuweka akiba, kuliko
kumaliza alichokuwa nacho katika kushughulikia shida aliyokuwa nayo! Unasemaje
katika hili?
Mfano wa
2: Sababu inayomfanya mdudu Chungu kuweka akiba ya chakula wakati wa joto.
Biblia
inasema “Ewe mvivu, mwendee Chungu, zitafakari njia zake upate hekima…hujiwekea
akiba ya chakula wakati wa jua; hukusanya chakula chake wakati wa mavuno”
(Mithali 6:6,8).
“Chungu”
anayetajwa hapa ni aina ya sisimizi, au aina ya siafu. Biblia inatuambia ya
kwamba”hujiwekea akiba ya chakula” wakati wa joto. Kwa nini anafanya hivyo?
Ni kwa
sababu anajua ya kuwa kipindi cha joto ni kipindi cha mavuno ya chakula
anachokula, ambacho hakipatikani wakati wa baridi, kwa kuwa kipindi cha baridi
si kipindi cha mavuno ya chakula chake!
Hii
inatupa kujua ya kuwa, “Sababu” za mdudu Chungu kuweka akiba ya chakula wakati
wa joto, ni kubwa kiumuhimu, kuliko kukila chakula chote wakati alipokuwa
anakikusanya. La sivyo, wakati wa baridi hatakuwa na chakula cha kula, kwa kuwa
hakuna mavuno ya chakula chake wakati wa baridi.
Tungelitazama
jambo hili kimapato, tungejua ya kwamba kipindi cha joto kilikuwa kipindi cha
kupata kipato chake, na kipindi cha baridi ni kipindi ambacho hana kipato.
Uamuzi aliokuwa nao si kutumia kipato chake chote alichokipata wakati wa joto,
bali aliamua baadhi ya kipato chake akiweke akiba, ili aje akitumie wakati hana
kipato – yaani wakati wa kipindi cha baridi!
Je,
maamuzi yako unayofanya juu ya kipato unachopata yakoje? Unatumia kipato chote
kwa matumizi yako ya sasa au kuna baadhi ya kipato unachokiweka akiba kwa ajili
ya matumizi ya baadaye?
Endelea
kufuatana nasi kwenye mfululizo wa somo hili , hapa kwenye ukurasa wetu wa
facebook katika siku chache zijazo.
Mungu aendelee kukubariki
, na tuzidi kuombeana.
Post A Comment:
0 comments so far,add yours