Kila mara nilipopata habari za watu wa Mungu walioanguka katika
dhambi ya zinaa nilikuwa najikuta najiuliza swali hili, “Hivi wanapataje
ujasiri wa kutenda tendo hilo?”
Akili yangu ilikuwa inakataa kabisa kuamini kuwa mtu aliyeokoka
(na wakati mwingine amejazwa Roho Mtakatifu) anaweza kuanguka kwenye dhambi ya
zinaa. Lakini hata hivyo bado nikawa naendelea kusikia majina ninayoyafahamu ya
watu wa Mungu waliookoka waliokubwa na dhambi ya zinaa.
“Wanafanyaje mpaka wanaanguka katika zinaa”? Hili swali
lilinisumbua kwa muda mrefu. Na siku moja nilikuwa nyumbani kwangu nikijiuliza
swali hili moyoni, nikasikia Roho Mtakatifu akiniuliza ndani ya moyo wangu,
akisema, “ Kwani Daudi aliangukaje? Je! Umesahau ya kuwa naye alikuwa mtu
wangu, mtumishi wangu niliyempaka mafuta?
Niliposikia swali hili, nilichukua biblia na kusoma maneno
yanayoeleza kuanguka kwa Mfalme Daudi katika dhambi ya zinaa na mke wa mmoja wa
askari wake.
Mambo niliyoyasoma yalinifungua macho kuona jinsi ambavyo hata
hivi leo watu wa Mungu wanavyoanguka au wanavyoweza kuanguka katika dhambi ya
zinaa.
Chukua biblia yako na usome habari hizi katika 2 Samweli 11:1-27
na 2 Samweli 12:1-25.
Chanzo cha kuanguka kwa Mfalme Daudi katika dhambi ya Zinaa, ni
KUTOKWENDA VITANI PAMOJA NA ASKARI WAKE.
“Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda
vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote,
wakaangamiza wana wa Amoni, wakakuhusuru Raba. LAKINI DAUDI MWENYEWE AKAKAA
YERUSALEMU”. (2 Samweli 11:1)
Kama kiongozi wao, Daudi alitakiwa kuongozana na watu wake vitani,
lakini yeye aliamua kubaki Yerusalemu asiende vitani, na akamtuma mtu mwingine
amwakilishe. Na jambo hili lilimpa nafasi nzuri sana ibilisi ya kumpa Daudi
kazi nyingine ya kufanya. Ni kazi gani hiyo?
“Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, AKATEMBEA JUU
YA DARI ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke ANAOGA;
naye huyo mwanamke alikuwa MZURI SANA WA KUPENDEZA MACHO”. (2 Samweli 11:2)
Ni kitu gani kilimfanya Mfalme Daudi aamue kutembea juu ya dari ya
jumba lake badala ya kwenda vitani pamoja na watu wake? Na alipomwaona
Bathsbeba, mkewe Uria akioga alishindwa kujizuia, mwisho wake ni kuzini naye na
huyo mama kupata mimba!
Wakristo wengi wamejikuta wameingia katika mtego wa zinaa kwa
sababu ya kutokwenda ‘Vitani’ wakati wanapotakiwa kufanya hivyo. Vita
tunavyovisema, si vita vya kimwili.
“Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya
mwili, maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu
hata kuangusha ngome; tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho
juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo”. (2
Wakorintho 10:3,4)
Na pia imeandikwa; “ Kwa maana kushindani kwetu sisi si juu ya
damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili juu
ya majeshi ya pepo wabaya, katika ulimwengu wa roho”. (Waefeso 6:11)
Ndiyo maana Yesu Kristo alisema; “ Kesheni mwombe msije mkaingia majaribuni;
roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.” (Mathayo 26:41)
Usipovipiga vita katika maombi, inakuwa ni rahisi sana kuangushwa
na majaribu unapokutana nayo. Wakristo wakipoa katika maombi inakuwa rahisi
kuanguka katika dhambi, si katika zinaa peke yake, bali katika mtego wowote
ambao shetani anauweka mbele yao!
Kutokuwa mwombaji, ni sawa na kutokwenda vitani na wenzako, kama
vile Mfalme Daudi alivyofanya.
Kwa hiyo unaona ya kuwa ingawa Mfalme Daudi alikuwa mtu wa Mungu,
mtumishi wake, na mpakwa mafuta wake, alianguka katika zinaa. Na hata hivi leo
kuna wakristo, tena wameokoka, na kupakwa mafuta kwa Roho Mtakatifu, wanaonguka
katika dhambi ya zinaa. Kwa nini? Kwa kuwa hawavipigi vita vya kiroho na
wenzao, na wamepoa katika kumtumikia Bwana.
Je! Lutu aliangukaje?
Hili ni swali ambalo Roho Mtakatifu aliniuliza baada ya kunieleza
habari za Mfalme Daudi. Ingawa Lutu alikuwa mtu wa Mungu, na licha ya kuwa
alikuwa anabebwa kwa maombi ya Ndugu yake Ibrahimu, bado alianguka katika
zinaa.
Roho Mtakatifu alikuwa anaendelea kunijibu swali nililokuwa
najiuliza ya kuwa, watu waliookoka wanaangukaje katika zinaa?
Habari za kuanguka kwa Lutu zimeandikwa katika kitabu cha Mwanzo
19:30-38.
Lutu alizini na watoto wake wawili wa kike baada ya kuleweshwa
mvinyo.
Na ukiisoma habari hii inasikitisha sana. Shetani alipata nafasi
ya kumwangusha Lutu si kwa sababu ya binti zake kumlewesha mvinyo, bali kwa
kuwa MKE WAKE HAKUWA PAMOJA NAYE. Unadhani mke wake angekuwapo hawa watoto
wangepata nafasi ya kumlaghai baba yao? Hapana! Kwa nini?
Kwa maana “ Bwana ameumba jambo jipya duniani, mwanamke atamlinda
mwanaume.” (Yeremia 31:22)
Unaweza kujiuliza ni kwa njia gani mke atalimnda mume wake.
Kumbuka imeandikwa mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana. Kazi moja ya busara
iliyo ndani ya mke ni kumlinda mume kutokana na mashambulizi ya Malaya! Soma
Mithali 2:11-22.
Hata hivi leo ndoa ambazo mume na mke hawakai vizuri, huwa ni
rahisi kwa wao kuanguka katika dhambi ya zinaa hata kama wameokoka. Na huu siyo
ushuhuda mzuri.
Tunamshukuru Mungu kwa wale ambao wamesimama katika ushuhuda
ingawa ndoa zao zina matatizo.
Jambo la kujifunza
zaidi
Roho Mtakatifu alipokuwa anaendelea kunifundisha akasema ndani ya
moyo wangu hivi; “Watu wengi wanadhani zinaa ni tendo la kimwili tu linalofanywa
kati ya mwanaume na mwanamke nje ya ndoa, lakini kuna namna zaidi ya moja
unayoweza kuanguka katika zinaa.”
Niliposikia hivyo moyoni mwangu, niliichukua Biblia na nikaanza
kuisoma upya juu ya zinaa na nikaona kuna namna nne ambazo zinaa inatajwa:-
1.
KATIKA MWILI:
“….Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa
mwili. Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo
vya Kristo na kuvifanya viungo vya Kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye
aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? …. Ikimbieni zinaa, kila dhambi
aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda
dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la
Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu
wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili
yenu.” (1 Wakorintho 6:13-20)
2.
KUTAMANI KWA MACHO. Yesu Kristo alisema;
“Mmesikia kwamba imenenwa Usizini; lakini mimi nawaambia, kila mtu
AMTAZAMAYE MWANAMKE KWA KUMTAMANI, amekwisha KUZINI NAYE MOYONI MWAKE.”
(Mathayo 5:27,28)
3.
KUACHA MKE NA KUOA MWINGINE
Yesu Kristo alisema;
“Kila amwachaye mkewe na kuoa mke mwingine azini ……” (Luka 16:18)
4. KUOA
ALIYEACHWA. Yesu Kristo alisema;
“Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; NAYE AMWOAYE
YEYE ALIYEACHWA NA MUMEWE AZINI.” (Luka 16:18)
Kila mtu na ajipime katika hayo; ikiwa umefanya mambo kama hayo
niliyoyataja, biblia inasema UMEZINI! Je Hakuna waliokoka
wanaofanya mambo ya jinsi hii? Wanaowaacha wake zao halali? – Wanaooa
walioachwa? – na wanaozini katika mwili?
Na Mwl. CHIRSTOPHER MWAKASEGE
SOURCE:http://www.mwakasege.org/
Barikiwa sana baba umenivushaa nakupenda bure sema hujui ❤️❤️❤️🇰🇪
JibuFuta