Ikiwa kuna swali kubwa ambalo linawatatanisha wakristo wengi, basi ni swali la kukua kwa imani yao ya kikristo. Wengine wanaita ni kukua kiroho kwa wakristo.
Ukiwauliza wakristo wengi ya kuwa ni
tatizo gani wanaloliona kubwa, linalowakwamisha katika maisha yao ya kikristo;
walio wengi watasema ni tatizo la imani.
Tatizo hili linatokea kati ya watu
wa Mungu, kwa kuwa hawajui imani ni nini, na kwamba inapatikanaje. Na wengine
wamekuwa wakijitahidi kuomba kwa Mungu kwa muda mrefu ili imani zao zikue,
lakini bila mafanikio ya kuridhisha.
Kwani imani maana yake nini?
“Basi imani ni kuwa na hakika ya
mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Waebrania 11:1)
Katika mstari huu tunaona mambo
mawili makubwa.
1. Imani ni kuwa na hakika
ya mambo yatarajiwayo; na 2. Imani ni bayana ya mambo yasiyoonekana.
Imani inakupa uhakika sasa juu ya
mambo ambayo unayoyatarajia. Imani inaweka wazi (bayana) mambo yasiyoonekana.
Chanzo cha imani ndicho pia chanzo
cha uhakika wako katika maisha ya kikristo; pia ni chanzo cha uwazi wa mambo ya
rohoni yasiyoonekana. Chanzo cha imani ndicho pia kinakupa uhakika wa maisha
yako ya wokovu.
Chanzo cha imani ni nini? Imani huwa mtu anaipataje?
Kwa maneno mengine unaweza ukauliza, chanzo cha uhakika ulio nao wa
wokovu na ukristo ni kitu gani?
Mara nyingi watu wa mataifa huwa wanauliza maswali yafuatayo: Mtu
atawezaje kuwa na uhakika wa kuokoka akiwa hapa duniani? Mtu
atawezaje kuwa na uhakika ya kuwa amesamehewa dhambi wakati bado yupo duniani?
Maswali haya huwa yanatokea mara kwa
mara kwa sababu hawajui uhakika wa mambo hayo unatoka wapi. Laiti wangejua,
basi wangekuwa na usemi mwingine midomoni mwao juu ya wokovu.
Biblia inasema wazi kabisa kwamba
yote yawezekana kwake aaminiye (Marko 9:23). Na kama biblia ambayo ni
Neno la Mungu inasema yote yawezekana kwake aaminiye, mwanadamu ni kitu gani
mbele za Mungu hata apinge?
Basi imani ni kuwa na hakika ya
mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.
Imani chanzo chake ni nini?
“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa Neno la Kristo”
(Warumi 10:17)
Mstari huu wa biblia unatufahamisha
kuwa imani chanzo chake ni kusikia Neno la Kristo. Hii ina maana ya kuwa
uhakika wa wokovu, au ukristo na misingi yake unapatikana kutokana na kusikia
Neno la Kristo.
Watu wengi utawasikia wakiomba na
wakati mwingine kwa kufunga na kwa kuomboleza ili Mungu awape imani. Lakini
mabadiliko katika maisha yao hayaonekani.
Biblia inatufahamisha wazi kabisa
kuwa ‘imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa Neno la Kristo.
Imani huja kwa Neno la Kristo. Imani huja kwa kusikia Neno la Kristo!
Watu wengi wamekuwa wakiomba imani
na wanapoona haionekani katika maisha yao, wanaanza kumkemea shetani bila
mafanikio yoyote. Watu wengi wanajikuta wamo katika hali ya kukwama kiroho na
kudumaa kwa sababu hawajawa wasikiaji wa Neno la Kristo.
“Lakini iweni watendaji wa Neno,
wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu” (Yakobo 1:22)
Kwa mstari huu tunapata upeo mkubwa
kidogo juu ya chanzo cha imani. Tunaweza sasa kusema, imani chanzo chake ni
kusikia na kulitenda neno la Kristo.
Imani huja kwa kulisikia na
kulitenda neno la Kristo. Uhakika tulio nao katika Njia hii ya wokovu katika
Kristo unatokana na Neno la Kristo tulilolisikia na kulitenda.
Kuwa msikiaji tu wa Neno la Kristo
haitoshi bila ya kuwa mtendaji wake. Neno la Kristo lililosikiwa na mtu,
lisipowekwa katika matendo haliwezi kuonekana na watu wengine.
Watu wengi sana ni wasikiaji wa Neno
la Kristo, utawakuta makanisani, wakiliskiliza Neno, utawakuta kwenye mikutano
ya kiroho pia utawakuta kwenye semina za Neno la Mungu; lakini watendaji wa
Neno hilo la Kristo wanalolisikiliza ni wachache sana.
Wasomaji wa biblia ni wengi sana,
lakini watendaji wa Neno hilo wanalolisoma ni wachache sana. Na kwa sababu hii
siku hizi ni vigumu sana kuweza kutofautisha kati ya mkristo na mtu wa kawaida,
au mtu aliyeokoka na mtu asiyeokoka, kwa kuwaangalia matendo yao.
Mtu anajiita mkristo au ameokoka
lakini matendo yake yako mbali sana na Neno la Kristo. Huu ni unafiki mkubwa –
unaohitaji kutafutiwa ufumbuzi.
Wakati umefika, na wakati wenyewe
ndiyo huu wa watu kujulikana maisha yao ya kikristo yamesimama katika msingi
upi. Ikiwa msingi huo ni Neno la Kristo, basi neno hilo ni budi lionekane
katika matendo yao ya kila siku.
Imeandikwa; “Lakini iweni
watendaji wa Neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu”.
Kuwa mtendaji wa Neno la Kristo
maana yake nini?
Kuwa mtendaji wa Neno la Kristo maana yake ni kuwa mtumiaji wa Neno la Kristo
ulilolisikia. Kuwa mtendaji wa Neno ni kulitumia Neno na Neno nalo likutumie
wewe.
Wewe unakuwa ndani ya Neno la Kristo
na Neno la Kristo linakuwa ndani yako. Neno la Kristo lililondani yako
unalitumia kuwa utukufu wa Mungu. Na wewe ukiwa ndani ya Neno la Kristo,
unatumiwa na Neno hilo kumtwalia Mungu utukufu.
Ndiyo maana Yesu Kristo alisema;
“Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke
yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi
ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa
sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote. Mtu asipokaa ndani
yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni,
yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu,
ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile
mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu,” (Yohana 15:4-8)
Kwa mistari hii tunaona kuwa imani
ya kikristo ni matokeo ya mtu kuunganishwa na Kristo mwenyewe. Na matokeo ya
matunda mazuri ya kikristo yanategemea jinsi ambavyo mtu anavyolisikia na
kulitenda Neno la Kristo.
Pia, tunaona kuwa matokeo ya maombi
ya mtu aliye mtendaji wa Neno la Kristo ni mazuri na yenye mafanikio kuliko
matokeo ya mtu aliye msikiaji tu wa Neno na wala si mtendaji.
Watu wengi ni wasikiaji wa Neno la
Kristo, lakini hawalitumii wala Neno haliwatumii kabisa. Na wengine ni
wasikiaji na watumiaji wa Neno la Kristo katika sehemu chache tu za maisha yao.
Lakini imeandikwa wazi kabisa kuwa
hao wanajidanganya nafsi zao wenyewe, wala hawamdanganyi Mungu, shetani wala
mtu yeyote, bali wao wenyewe; kwa kuwa wamekuwa wasikiaji wa neno la Kristo
lakini si watendaji.
Na ndiyo maana Roho wa Mungu
aliomboleza kwa kupitia kwenye kinywa cha Nabii Hosea akisema; “Watu wangu
wanaangamizwa kwa kukosa maarifa” (Hosea 4:6)
Na Yesu Kristo, pia, alikuwa na haya
ya kusema juu ya watu wa namna hiyo: “Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko
wala uweza wa Mungu” (Mathayo 22:29)
Ni kweli kabisa kuwa kanisa ambalo
ni mwili wa Kristo, limekuwa katika hali ngumu kiroho kwa sababu ya kukosa
maarifa ya Mungu yanayotokana na kulisikia na kulitenda Neno la Kristo.
Imeandikwa; “Lakini iweni watendaji
wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu
akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu
anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara
akasahau jinsi alivyo.” (Yakobo 1:22-24)
Tunakumbuka wakati fulani tulikuwa
tunaongea na mtu mmoja juu ya maisha yake ya wokovu. Tulimuuliza swali hili; “Ni
kitu gani kinachokutofautisha wewe na mkristo mwingine wa kawaida?”
Akasema; “Ni kwa sababu
nimemwamini Mungu”
Tukasema; “ Hiyo haitoshi
kwa sababu hata wao wanamwamini Mungu. Je! hujasoma ya kuwa mashetani nao
wanaamini na kutetemeka?”
Akauliza; “Sasa kitu gani
kinacholeta tofauti?”
Tukasema; “ Ni maisha yako
mapya yanayopatikana baada ya kumpokea Kristo moyoni mwako”.
Tukamsomea waraka wa pili kwa
Wakorintho Sura ya tano na mstari wa kumi na saba, unaosomeka hivi; “Hata
imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita;
tazama! Yamekuwa mapya”
Unapompokea Kristo (Neno) moyoni
mwako unapewa uzima wa Mungu ndani yako, na tabia mpya inayoongozwa la Neno la
Kristo.
Ni vigumu sana kumtofautisha mtu wa
Mungu na mtu wa kawaida kwa kusikia wanachosema tu peke yake. Ni lazima maisha
mapya ndani ya Kristo, maisha ya wokovu yaandamane na tabia mpya.
Tabia mpya hiyo haionekani siku hizi
kwa sababu, watu hawajawa watendaji wa Neno. Yakobo anauliza:
“Ndugu zangu, yafaa nini, mtu
akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! ile imani yaweza
kumwokoa?…..
“Vivyo hivyo na imani, isipokuwa
ina matendo, imekufa nafsini mwake” (Yakobo 2:14,17)
Hii maana yake mtu asipokuwa
mtumiaji wa Neno la Kristo, anaonekana kama vile si mkristo. Utafahamu ni
mkristo kwa sababu anakwenda kanisani jumapili au jumamosi, lakini si kwa
sababu umeona matendo ya kikristo maishani mwake.
Na hata watu wengi waliookoka
wanaliabisha Jina la Bwana kwa kujiita wao ni watu wa Mungu, watoto wa Mungu,
wana wa mfalme, watumishi wa Bwana; kwa sababu matendo yao hayafanani na maneno
wanayosema.
Yafaa nini basi, mtu kusema ameokoka
wakati bado anatawaliwa na matendo ya dunia? Yafaa nini, basi mtu kusema yeye
ni mkristo, wakati maisha yake yana matendo kama ya mtu asiyemjua Kristo?
“Lakini mtu atasema, wewe unayo
imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami
nitakuonyesha imani yangu KWA NJIA YA MATENDO YANGU”. (Yakobo 2:18)
KWA NJIA YA MATENDO watu watajua kuwa imani yako
ni ipi. Kwa njia ya matendo yako watu watajua ya kuwa wewe in mkristo au La.
Imani yako na ijulikane mbele za
watu kwa njia ya kuwa mtendaji wa Neno.
Umefanyika kuwa kiumbe kipya ndani
ya Kristo, kwa hiyo matendo yako ni mapya, pia, matendo ya kale yamepita. Kwa
matendo yako yaliyosimama ndani ya Neno la Kristo, ulimwengu utajua ya kuwa
umeokoka au La.
“Wewe waamini ya kuwa Mungu ni
mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. Lakini wataka kujua,
wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai?….
“Maana kama vile mwili pasipo
roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa” (Yakobo
2:19,20,26)
Mashetani yanamjua Mungu ya kuwa ni
mmoja, na yanaamini hivyo na kutetemeka. Mashetani yana hofu ya Mungu, lakini
watu wengi hawana hofu ya Mungu ndani yao.
Kwa kutokuwa mtendaji wa Neno,
unajikuta kuwa utamu wa maombi, utamu wa kushuhudia, utamu wa Neno la Mungu
unafifia ndani yako.
Imani haiji kwa kuomba, kukua kwa
imani yako hakutakuja kwa kuomba, bali huja kwa kusikia na kulitenda Neno la
Kristo.
Si kwamba tunadharau sehemu ya
maombi katika maisha ya mkristo, la hasha. Maombi ni muhimu sana kwa mkristo
kama vile petroli ilivyo muhimu kwa ajili ya gari.
Ukijaza petroli kwenye gari haina
faida yoyote hadi hapo utakapoingia ndani ya gari na kuliendesha toka mahali
lilipo na kwenda mahali pengine unapotaka.
Maombi bila kuwa mtendaji wa Neno,
ni bure. Maombi PAMOJA na utendaji wa Neno vinaleta mafanikio
makubwa katika kukua kiroho. Neno ndilo linakuongoza unapotaka kusogea kiroho.
Maombi PAMOJA na
utendaji wa Neno ni muunganiko wenye maana kubwa katika kuifanikisha kazi yetu
tuliyotumwa kuifanya hapa ulimwenguni; kazi ya kuwa wajumbe (mabalozi) kwa
ajili ya Kristo.
Lakini tunajua kuwa “sisi tu
wafanyakazi pamoja na Mungu” (1Wakoritho 3:9). Kuwa mfanyakazi
pamoja na Mungu maana yake ni kuwa mfanyakazi pamoja na Neno, kwa sababu Mungu
ni Neno (Yohana 1:1)
Kuwa mfanyakazi pamoja na Neno maana
yake ni kuwa mtenda kazi pamoja na Neno; ni kuwa mtendaji wa Neno; ni kuwa
mtumiaji wa Neno.
Si
kwamba watu wanapenda kutokuwa watendaji wa Neno, bali wengi hawafahamu ni
namna gani ambavyo watafanya ili neno la Kristo walilolisikia au kulisoma
lionekana katika maisha yao.
Post A Comment:
0 comments so far,add yours