Utangulizi
SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASIKINI!
(Namna ya mkristo kuishi katika hali ngumu ya
uchumi bila kumkosea Mungu)
Kati
ya mambo yaliyotabiriwa kutokea katika siku hizi za mwisho ni dhiki katika
mataifa, pamoja na hali ngumu ya uchumi. Soma mwenyewe katika Luka 21:25-26 na
Ufunuo wa Yohana 6:5-6.
Pia, tunasoma kutoka katika biblia ya kuwa biashara na uweza wa kuuza na
kununua utafuata mfumo fulani uliojaa dhuluma, ambao utatawaliwa na kundi
fulani ulimwenguni. Watu hawatauza wala kununua bila ya kupatana na watu wa
kundi hilo, na hasa kiongozi wao. Na asomaye na afahamu. Soma kitabu cha
Ufunuo wa Yohana sura yote ya 13.
Si hivyo tu, bali biblia inaeleza wazi kabisa kuwa katika siku hizi za mwisho
kutakuwa na uhusiano mkubwa sana kati ya utajiri na uasherati na pia
kati ya biashara na uasherati. Soma kitabu cha Ufunuo wa Yohana sura za 17 na
18. Lakini pia unaweza kuwa na utajiri na ukafanya biashara bila kujihusisha na
uasherati na mambo mengine yaliyo kinyume na maadili ya Mungu.
Tutawezaje kupona katika hali ya namna hii tusimkosee Mungu
wetu aliyetuita katika utakatifu ndani ya Mwana wake mpendwa Yesu Kristo? Kwa
nini wakristo wengi wanaishi katika hali ngumu kiuchumi kama vile
kuna mtu aliyewawekea vikwazo vya uchumi wasifanikiwe?
Watu wengi wanapenda kuishi maisha matakatifu na wengi pia wanapenda kuokoka na
kudumu ndani ya kristo, lakini swali linalowasumbua ni wafanyeje katika hali
ngumu hii ya uchumi wapate chakula, malazi na mavazi kihalali bila kumkosea
Mungu?
Ni watu wachache wanaofahamu uwezo wa mawazo katika kuongoza maneno na
matendo yao ya kila siku. Ni budi ufahamu ya kuwa maneno yako na
matendo yako ni matokeo ya jinsi unavyowaza. Kwa maneno mengine naweza kusema
ya kuwa maisha ya mtu yanategemea mtazamo wa mawazo yake.
Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba jinsi ulivyo ni matokeo ya
jinsi unavyowaza; kwa kuwa unayowaza ndiyo unayoyasema na kuyafanya.
Watu wengi wamekuwa wakifikiri ya kuwa Mungu ndiye aliyewapangia kuwa maskini.
Na hata wakristo wengine kudiriki hata kuuona umaskini kama sehemu ya
utakatifu na unyenyekevu.
Lakini Biblia haisemi hivyo, wala haifundishi mawazo hayo. Ni lengo langu
kukueleza katika ujumbe huu ya kwamba SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASKINI.
Nataka ufahamu pia ya kuwa nitakapokuwa natumia neno wakristo katika
ujumbe huu, ujue namaanisha wakristo wale wanaomkiri Yesu Kristo ya kuwa Bwana
na Mwokozi wao; ambao pia humwabudu Mungu katika Roho na Kweli.
Ni maombi yangu kwa Mungu katika Jina la Yesu Kristo kuwa atakuwezesha kusoma
na kuelewa somo hili, ili wote tulio wakristo tusimame katika haki zetu zote
zilizopatikana pale msalabani. Nia hasa ni kukupa mafundisho ya msingi ya
kukusaidia uweze kuishi hata katika hali ngumu ya uchumi bila kumkosea Mungu.
Kila wiki nitakuwa nakuwekea sura mojawapo ya mafundisho haya.
Mafundisho ninayotarajia kukufundisha
yatakuwa na mfululizo wa masomo kama yafuatayo:
· Kwa
nini si mapenzi ya Mungu tuwe maskini?
· Mafundisho
manne yasiyo sahihi unayopaswa kuyatambua
· Nani
anaupenda wokovu wa kimaskini?
· Utajiri
wake Kristo usiopimika
· Uchumi
wa ufalme wa mbinguni
· Tofauti
ya zaka na dhabihu
· Ukitoa
tegemea kupokea
· Sadaka
na wokovu
· Natoa
lakini sipokei – nifanyeje?
· Ufanyeje
katika hali ngumu ya uchumi?
Haya ni mafundisho ambayo
nitayaweka kwa namna ambayo yatakupa changamoto ya kuyasoma zaidi wewe binafsi
na kuyaweka katika matendo. Kwa hiyo usitegemee kupata majibu ya maswali yote
uliyonayo juu ya mambo niliyoorodhesha hapa juu, bali tegemea mwongozo wa
changamoto itakayokusaidia katika kujifunza zaidi juu ya utajiri na
mkristo.
KWA NINI SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASKINI?
Napenda kuanza
kukuambia ya kuwa si mapenzi ya Mungu uwe maskini. Kwa sababu tangu kuwekwa
misingi ya ulimwengu huu, Mungu hakupanga kuwa watu wake aliowaumba wawe
maskini; bila kujali rangi, kabila, wala taifa.
Nafahamu ya kuwa katika Mathayo 5:3, Yesu Kristo
alisema; “Heri walio maskini wa roho; maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Watu
wengi wanapousoma mstari huu, wanadhani Yesu Kristo alisema “Heri walio maskini
wa mahitaji ya MWILI; maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Lakini Kristo hakusema
hivyo.
Mtu maskini maana yake ni mtu mhitaji. Yesu Kristo
aliposema “Heri walio maskini wa roho …….” Alikuwa ana maana ya
kusema ‘Heri walio wahitaji wa mambo ya rohoni; maana ufalme wa mbinguni ni
wao. Ndiyo maana aliongeza kusema, “Heri wenye njaa na kiu ya haki; maana
hao watashibishwa" (Mathayo 5:6).
Mtu aliye maskini wa mambo ya mwili ni yule aliye mhitaji wa mambo ya mwili. Na
mambo ya mwilini ninayoyasema ni mavazi, chakula na mahali pa kulala. Yesu
Kristo hakusema heri wale walio na mahitaji ya chakula, mavazi, afya na malazi.
Ninaposema mahitaji ya mwili usije ukachanganya na matendo ya mwili
yaliyoandikwa katika Wagalatia 5:19-21 ambayo ni uasherati, uchafu, ufisadi,
ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
husuda na ulevi. Mimi siyazungumzii hayo ninaposema juu ya mahitaji ya mwili.
Mahitaji ya mwili ninayoyasema ni mavazi, chakula, nyumba na matibabu.
Kwa hiyo si sawa kabisa kwa mtu kuhalalisha umaskini wa mwili, yaani ukosefu wa
chakula, mavazi, matibabu na nyumba, kwa kutumia maneno ya Bwana Yesu Kristo
yaliyo katika Mathayo 5:3:
Nataka kurudia tena; si mapenzi ya Mungu mtu
awe maskini.
Unaweza ukaniuliza na kusema, “Bwana Mwakasege kama si mapenzi ya Mungu mtu awe
maskini, mbona basi kuna matajiri na maskini, je! Mungu hakuwaumba wote?
Ni kweli kwani hata imeandikwa katika Mithali 22:2, kuwa “Tajiri na
maskini hukutana pamoja; Bwana ndiye aliyewaumba wote”. Lakini fahamu ya kuwa
ingawa matajiri na maskini waliopo wote waliumbwa na Mungu; tangu mwanzo wa
uumbaji Mungu hakuyaweka matabaka haya mawili.
Hapo mwanzo Mungu alipomuumba mtu, hakuweka ndani yake utajiri na umaskini
pamoja. Wala hakuumba watu wengine wawe matajiri na wengine wawe maskini.
Tunafahamu ya kuwa mtu aliumbwa kwa mfano wa Mungu na kwa
sura ya Mungu. Na naamini ya kuwa utakubaliana nami nikisema Mungu wetu si
maskini kwa hiyo hatukuumbwa kwa mfano wa kimaskini wala sura ya kimaskini.
Kwa nini nasema na kusisitiza ya
kuwa si mapenzi ya Mungu tuwe maskini?
Ninazo
sababu nne ambazo ningependa kukushirikisha:
Mungu ndiye atupaye nguvu za kupata utajiri
“ Bali utamkumbuka Bwana , Mungu wako, maana
ndiye akupaye NGUVU ZA KUPATA UTAJIRI; ili alifanye imara agano lake
alilowapa baba zako, kama hivi leo” (Kumb. 8:18).
Si mapenzi ya Mungu tuwe maskini kwa
kuwa yeye mwenyewe ndiye atupaye nguvu ili tupate utajiri! Kama basi
Mungu anatupa nguvu za kupata utajiri, ina maana ni wazi kwamba Mungu hapendi
tuwe maskini wa mambo ya mwilini.
Lakini fahamu ya kuwa si matajiri wote waliopo duniani wameupata utajiri
kutokana na nguvu walizopewa na Mungu. Wengi wamepata utajiri kwa njia ya
dhuluma. Na ndiyo maana sehemu nyingi katika Biblia matajiri wa jinsi hiyo
wamekemewa. Soma Amosi 5:11, 12. Kwa sababu hii Mungu hayuko upande wa matajiri
hawa. Hii pia haimaanishi kuwa Mungu yuko upande wa KILA maskini aliopo
duniani. La hasha! Mungu yuko upande wa yule ayafanyaye mapenzi yake awe tajiri
au maskini (Mathayo 7:21)
Watu wengi wametajirika kwa njia ya rushwa na kutokusimamia haki pamoja na
uchoyo. Na hii si sawa hata mbele za Mungu. Ni dhambi zilizo wazi kabisa. Na
wote wafanyayo hayo wanahitaji kutubu!
Ngoja nikueleze jambo muhimu: Mungu anapokupa nguvu za kupata utajiri, anakupa
akiwa na lengo na kusudi muhimu.
Ni lengo gani hilo?
Imeandikwa,
“………. Ili alifanye imara agano lake alilowapa baba
zako, kama hivi leo”
Na Yesu
Kristo alisema, “ ……. Kikombe hiki ni AGANO JIPYA KATIKA DAMU YANGU,
inayomwagika kwa ajili yenu” (Luka 22:20).
Mungu akikupa nguvu za kupata
utajiri ni kwa ajili ya kulifanya imara agano lake katika damu
ya Yesu Kristo. Na hii ina maana utajiri utakaokuwa nao kutoka kwa Mungu ni kwa
kueneza injili! Ni kwa ajili ya kueneza habari njema ya ukombozi kutokana na
dhambi, mauti, magonjwa na umaskini. Habari njema hii inatakiwa kuenezwa
kwa maneno na kwa matendo.
Kwa kuwa tu kuna matajiri wasio wa haki basi haimaanishi kuwa matajiri wa haki
hawapo. Ni budi tuweze kutofautisha utajiri ulio wa haki na utajiri usio wa
haki.
Mungu ndiye atufundishaye kupata faida
Mungu wetu tunayemwabudu na kumtumikia katika
Kristo Yesu si Mungu wa hasara bali Mungu wa faida. Imeandikwa hivi;
“ Bwana, Mkombozi wako, Mtakatifu
wa Israeli, asema hivi;Mimi ni Bwana, Mungu wako,
nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye katika njia ikupasayo
kuifuata” (Isaya 48:17).
Ndiyo maana kila mtu ndani yake ameumbiwa kupenda kufundishwa ili apate faida
katika mambo anayoyafanya. Mungu akikufundisha kupata faida; njia utakayotumia
kupata faida itakuwa njia ya haki. Na faida hiyo haitakuwa kwa ajili yako mwenyewe,
bali utawashirikisha na wengine pia faida hiyo .
Watu wengine kwa kutokuwa wavumilivu, na kutokujali mafundisho ya Mungu;
wameamua kujipatia faida kwa kuwadhulumu, kuwakandamiza na kuwanyonya wengine.
Na inasikitisha jinsi wanavyomshirikisha Mungu katika faida najisi namna hiyo
waposema ya kuwa ni Mungu aliyewasaidia ‘kudhulumu na kunyonya’. Ni wazi ya
kuwa Mungu hakuwasaidia kupata faida kwa njia ya udhalimu.
Si mapenzi ya Mungu tuwe maskini,
ndiyo maana anatufundisha ili tupate faida ya halali. Kwa ajili hiyo
imeandikwa; “Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda
kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia
mhitaji” (Waefeso 4:28).
Je! Si
jambo la kushukuru hili, la kuwa na Mungu ambaye hapendi tupate hasara?
Kama
Mungu asingekuwa anapenda tufanikiwe katika mahitaji yetu ya mwili, basi
ingeandikwa wazi katika Biblia. Lakini badala yake naona maneno kama
yafuatavyo; “Mpenzi, naomba ufanikiwe katika mambo YOTE na kuwa na afya
yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo” (3Yohana 1:2).
Kwa
maneno mengine anatuombea ya kuwa kwa kadri roho inavyofanikiwa basi tufanikiwe
vivyo hivyo katika mahitaji ya mwili – yaani tuwe na chakula, mavazi, n.k.
Vitu vyote vyema ni mali ya Bwana, na vyote
vya Bwana ni vyetu ndani ya Kristo
Katika Zaburi 24:1 imeandikwa;“Nchi na vyote viijazavyo
ni mali ya Bwana; Dunia na wote wakaao ndani yake”
Na pia ukisoma katika Hagai 2:8 unaona imeandikwa hivi “Fedha
ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa
majeshi”
Ngoja nikuulize swali; Je! unadhani vitu vyote hivi Bwana amemwekea nani?
Unadhani alimwekea shetani na watu wanyonyaji wachache?
La hasha!
Mungu aliviweka vitu hvi vyote
na mali hii yote kwa ajili ya watu wake wote, ili itumike katika
usawa. Kwa nini? Kwa kuwa Mungu hapendi watu wake wawe maskini. Ndiyo maana mtu
alipoumbwa aliwekwa awe wakili wa mali yote ya Mungu hapa duniani.
Utajiri uliomo duniani umetawaliwa
na watu wachache na nchi chache siku hizi kwa sababu ya dhambi za uchoyo,
ubinafsi, uonevu,unyonyaji, unyang’anyi na dhuluma zilizoingia ndani ya
mwanadamu.
Na hii imefanya watu wengine kufikiri ya kuwa Mungu ndiye aliyegawa matabaka
haya mawili, ambavyo si kweli. Na si vizuri kumsingizia Mungu katika jambo
ambalo mwanadamu mwenyewe amejiletea uharibufu.
Yesu Kristo alikuwa maskini ili sisi tuwe
matajiri
“ Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi
alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi
mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake” (2 Wakorintho 8:9).
Je! unafahamu kwa nini
Yesu Kristo aliamua kuwa maskini? Ni “…….. ili kwamba ninyi mpate kuwa MATAJIRI
kwa umaskini wake”.
Najua kuna wengine watashangaa
kuusoma mstari huu; lakini ndivyo ilivyo.
Nimewahi kusikia mkristo mmoja akisema: “ Mimi ni maskini kwa kuwa Yesu
Kristo alikuwa maskini”.
Na mwingine alisema; “ Napenda kuwa maskini kwa kuwa Yesu Kristo
alikuwa maskini”.
Nadhani kuwa kuna wakristo wengi ambao wana mawazo kama haya. Ni
kweli kwamba Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alikuwa maskini. Lakini hakuwa
maskini ili sisi tuwe maskini; bali alikuwa maskini ili sisi tuwe matajiri!
Kama alikuwa maskini ili sisi tuwe maskini kama wengine wanavyodhani,
basi kazi hiyo haina faida kwetu. Lakini Yesu Kristo asifiwe kwa kuwa alikuwa
maskini ili sisi tuwe MATAJIRI.
Na
ndiyo maana alisema katika Luka 4:18a ya kuwa; “Roho wa Bwana yu juu
yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri MASKINI habari njema.”
Je!
kuna habari njema kwa maskini zaidi ya kumwondoa katika umaskini wake?
Injili
ni habari njema. Na injili ni uweza wa Mungu uuletao wokovu kwa kila aaminiye
(Warumi 1:16). Kuokoka si kuenda tu mbinguni; bali kuokoka maana yake ni
uokolewe usiende motoni bali uende mbinguni ukifa, PAMOJA na kuokolewa kutoka
kwenye matatizo ukiwa hapa duniani ambayo ni pamoja na umaskini.
Petro
aliposema “Bwana niokoe” alipokuwa anazama katika maji unafikiri alikuwa
anataka wakati huo aokoke aende mbinguni? La hasha! Yeye Petro alitaka aokoke
ASIZAME KATIKA MAJI. Na Yesu akasikia kilio chake akamwokoa. Hivi leo kuna watu
wengi mijini na vijijini wanalia Yesu awaokoe kutokana na njaa, kukosa mavazi,
magonjwa, maonezi, nakadhalika. Kanisa kama mwili wa Kristo linatakiwa kuwa
mstari wa mbele kuwasaidia watu hao, kwa kuwa kazi hii ni sehemu ya utume wake.
Wakristo wengine utawasikia wakisema; hapa
duniani hawahitaji kitu bali thawabu yao wataipata mbinguni. Lakini
matamshi ya namna hii yanaeleza ukweli nusu na usiokamilika. Kuwa mkristo kuna
thawabu duniani na kuna thawabu mbinguni.
Kama hakuna thawabu yoyote
tunayoipata tukiwa hapa duniani kwa kumfuata Yesu Kristo; basi ukristo wetu
hauna maana na hauna msaada wowote kwa mwanadamu. Ukristo usiotatua matatizo ya
mwanadamu ya kila siku, ni ukristo usio na uhai.
Mtume Petro naye aliwahi kusumbuliwa sana na jambo hili, hata ikabidi
amuulize Bwana Yesu.
“Ndipo
Petro akajibu, akamwambia, tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata, TUTAPATA
NINI BASI?” (Mathayo 19:27)
“Yesu akasema, Amini, nawaambiaeni, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu
waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili
yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa MARA MIA SASA WAKATI HUU, nyumba, na
ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia;
na katika ulimwengu ujao uzima wa milele” (Marko 10:29,30).
Majibu haya ya Bwana Yesu, yanazidi kutudhihirishia ya kwamba si mapenzi ya
Mungu tuwe maskini. Yesu Kristo ameeleza wazi kabisa ya kuwa atakayemwamini na
kufuata maagizo hayo atapata MARA MIA SASA WAKATI HUU akiwa bado duniani. Na
kati ya vitu atakavyopewa ni pamoja na nyumba na mashamba!
Ni kweli Bwana Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alikuwa maskini, lakini baada
ya kufufuka alirudishiwa utajiri wake. Ndiyo maana Mtume Paulo anazungumzia juu
ya “….. utajiri wake Kristo usiopimika”. (Waefeso 3:8). Na katika
Wafilipi 4:19 tunasoma hivi; “Na Mungu wangu atawajazeni kila
mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo
Yesu”.
Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua dhambi zetu na magonjwa yetu , na kwa
kupigwa kwake sisi tumepona (Isaya 53:5; Mathayo 8:16,17; 1Petro 2:24). Na kwa
kujua hili kanisa linajihusisha na kuombea wagonjwa na kutoa huduma za afya kwa
wagonjwa.
Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua dhambi zetu na akafanyika dhambi kwa
ajili yetu, “ Ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye” (2Wakorintho
5:21). Na kwa kujua hili kanisa linahubiri habari za ondoleo la dhambi kwa
yeyote atakayemwamini Kristo.
Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alikuwa
maskini, ingawa alikuwa tajiri, ili kwa umaskini wake sisi tupate kuwa matajiri
(2 Wakorintho 8:9). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na miradi mbalimbali
ya kimaendeleo ili mtu aondokane na umaskini.
MAMBO MANNE UNAYOPASWA KUYAJUA
Kuna mafundisho ambayo si sahihi yaliyowafanya wakristo wengi hasa wale
waliookoka kutokujua cha kuamini juu ya uhusiano wa ukristo wao na utajiri. Na
tuangalie maeneo manne yafuatayo ambayo wakati mwingine yamezaa mafundisho yasiyo
sahihi:
TAJIRI NA UFALME WA MUNGU:
Nadhani utakuwa umewahi kusikia watu wakisema; “Matajiri hawataurithi ufalme wa
Mungu” Na wanasema ndivyo Bwana Yesu alivyosema baada ya tajiri aliyetaka uzima
wa milele kukataa kuuza mali yake.
Hata mimi mwanzoni ilikuwa karibu sana nikubaliane na usemi huu. Lakini baada
ya kuyachunguza maandiko niliona ya kuwa Yesu Kristo hakusema hivyo bali
anasingiziwa tu.
Yesu Kristo alisema hivi;“Kwa shida gani wenye mali WATAUINGIA ufalme wa Mungu” (Luka
18:24)
Kwa mstari huu tunajua ya kuwa Yesu Kristo
hakusema ya kuwa wenye mali hawatauingia ufalme wa Mungu; bali
alisema “kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu!”
Na
akaendelea kusema, “ Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la
sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” (Luka 18:25). Na
wale waliosikia wakashtuka na kushangaa, kwa maana waliona itakuwa
vigumu sana kwa tajiri kuokoka, na naona walifikia
mawazo kama waliyonayo wengi siku hizi ya kuwa tajiri hawezi kuingia
katika ufalme wa Mungu. Ndiyo maana wakauliza “Ni nani basi awezaye
kuokoka?” (Luka 18:26).
Yesu Kristo akawajibu akasema;“Yasiyowezekana
kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu” (Luka 18:26).
Kwa maneno mengine alikuwa anasema tajiri
anaweza KUWEZESHWA NA MUNGU kuingia katika ufalme wa Mungu akiiamini injili
inayookoa. Hata hivyo maskini naye anaokolewa kwa neema ya Mungu.
Na kwa kuamini kuwa tajiri hawezi kuurithi
ufalme wa Mungu, wakristo wengi kwa kudhamiria kabisa wameamua kuwa maskini ili
wasije wakaukosa ufalme wa Mungu. Lakini hii si sawa na ni kukwepa wajibu wetu
tulionao kama mawakili wa mali zote za Mungu.
Na ni vizuri
ufahamu ya kuwa umaskini wa kukosa chakula, mavazi na nyumba ya kukaa siyo
tiketi ya kuingia katika ufalme wa Mungu. Na wala umaskini siyo utakatifu –
ingawa kuna maskini walio watakatifu! Na pia utajiri siyo utakatifu ingawa kuna
matajiri walio watakatifu.
Kuna Mkristo
mmoja wa dhehebu fulani alikuwa akinieleza hali iliyowasonga katika dhehebu
lao; alisema;
“Katika kanisa letu Mchungaji akionekana
amevaa vizuri, wakristo wake wanasema amepoa kiroho. Kwao mtu wa
kiroho ni mtu aliye maskini, asiyevaa nguo nzuri wala viatu vizuri.”
Niliposikia maneno hayo nilisikitika sana,
na nikakumbuka maneno ya Mungu aliyosema kwa kutumia kinywa cha nabii Hosea,
yasemayo, “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa ….” (Hosea
4:6) na pia Yesu Kristo aliwahi kusema ya kuwa watu wanapotea kwa
kuwa hawajui maandiko wala uwezo wa Mungu.
Kwa hiyo fungua moyo wako uisikie kweli
ambayo ndiyo neno la Mungu. Na utaifahamu kweli na hiyo kweli itakuweka huru
(Yohana 8:32)
MUNGU NA MALI
Kuna uhusiano gani kati ya Mungu na Mali? Kuna uhusiano gani kati ya Mkristo na
Mali? Kuna uhusiano gani kati ya wokovu na mali?
Je, ni dhambi kwa mkristo kuwa na mali nyingi? Hebu na tuangalie maneno ya Yesu
Kristo juu ya Mungu na Mali.
“Hakuna
mtu awezaye kutumikia mabwana wawili, Kwa maana atamchukia huyu, na
kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia
Mungu na Mali” (Mathayo 6:24)
Neno la kiingereza lililotafsiriwa na
kuandikwa ‘mali’ ni ‘mammon’ Na neno hili ‘mommon’ ni jina
la roho ya ibilisi inayotawala mali. Kwa maneno mengine naweza kusema kuwa
‘mammon’ ni jina la pepo.
Kwa hiyo,
neno ‘mali’ lilivyotumika hapa linamaanisha ‘pepo linaloitwa Mali’ Ndiyo maana
Yesu Kristo alisema; “Hakuna mtu awezaye kutumikia MABWANA wawili ….”
Yesu Kristo asingeliita mali kuwa ni mojawapo ya MABWANA kama hakuwa anasema
juu ya roho inayoitwa mali. Roho hii ya shetani iitwayo Mali imewafanya watu
wengi, hata wakristo waache kumtumikia Mungu aliye hai, na badala yake
waitumikie roho inayowasukuma na kuwatamanisha juu ya mali, ili waitumie kwa uchoyo
na ubinafsi.
Wakristo
wengine wanadhani wanaweza kumtumikia Mungu na vile vile wamtumikie Mali. Yesu
Kristo alisema; “HAKUNA mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana
ATAMCHUKIA HUYU, NA KUMPENDA HUYU: AMA ATASHIKAMANA NA HUYU, NA KUMDHARAU HUYU.
Hamwezi kumtumikia Mungu na Mali.”
Kwa kusema hivi hakuwa anamaanisha kuwa na
vitu vinavyoitwa mali ni vibaya. Kitu anachosema ni kibaya ni KUITUMIKIA MALI!
Biblia inasema katika Zaburi 24:1 kuwa, “Nchi na vyote viijazavyo ni mali
ya Bwana; Dunia na wate wakaao ndani yake.”
Mtu hakuumbwa ili kuitumikia mali. Mtu
aliumbwa kwa ajili ya utukufu wa Mungu na amtumikie Yeye peke yake. Mali ya
dunia iliwekwa kwa ajili ya kumtumikia mtu, na siyo mtu kuitumikia mali! Mtu
aliwekwa juu ya mali yote na aliagizwa kuitawala (Mwanzo 1:28 – 30).
Kuwa na mali siyo vibaya, wala siyo dhambi.
Mali inakuwa kikwazo katika maisha ya ukristo inapoanza kumfanya mtu amsahau
Mungu na mapenzi yake. Ndiyo maana Yesu Kristo alisema; “Kwa shida gani
wenye mali watauingia ufalme wa Mungu” (Luka 18:24) siyo kwamba hawezi
kuuingia ufalme wa Mungu, bali kwa shida wenye mali watauingia ufalme wa Mungu.
Kwa maneno mengine ni kwamba wakimtanguliza na kumtumikia Mungu, mali haitakuwa
kwazo katika maisha yao ya ukristo.
Sasa tuishije katika ushauri wa namna hii?
“Kwa sababu hiyo nawaambieni, msisumbukie maisha yenu, mle
nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula,
na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi,
wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha
hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? NI YUPI KWENU AMBAYE AKIJISUMBUA AWEZA
KUJIONGEZA KIMO CHAKE HATA MKONO MMOJA? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia?
Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala
hayasokoti; nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote
hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani
ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, JE! HATAZIDI SANA KUWAVIKA
NINYI, ENYI WA IMANI HABA? Msisumbuke basi, mkisema, Tule nini? au Tunywe nini?
au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa
mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote” (Mathayo 6:25 – 32)
Kuna
wakristo wengine wameyaelewa vibaya maneno haya ya Bwana Yesu Kristo hata
kufikia kutokufanya kazi kwa kisingizio cha kwamba Yesu Kristo alisema
tusiyasumbukie maisha. Kwao kufanya kazi ina maana kusumbukia maisha. Lakini
napenda kukuambia ya kuwa Yesu Kristo hakuwa ana maana ya kutuambia tusifanye
kazi aliposema tusiyasumbukie maisha.
Nadhani unaamini ya kuwa ni Roho wa Kristo
aliyemwongoza Mtume Paulo kuwaandikia Wathesalonike juu ya mashauri mbali mbali
ya kikristo. Katika 1Wathesalonike 3:10b anasema, “Ikiwa mtu hataki
kufanya kazi, basi, asile chakula.” Ni muhimu kufanya kazi. Kufanya kazi
siyo kusumbuka na maisha. Kusumbuka na maisha siyo kufanya kazi.
Jambo ambalo Bwana Yesu Kristo alitaka
tufahamu wakati alipokuwa akisema tusisumbukie maisha, ni kwamba katika kila
jambo tumshirikishe Mungu na kumtanguliza Yeye. Wakristo wengine wanadhani
wanaweza kula, kunywa na kuvaa bila msaada wa Mungu. Yesu Kristo alisema katika
Yohana 15:5b kuwa; “…… maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya NENO LO
LOTE” (Hili ni pamoja na kula, kunywa na kuvaa) Ndiyo maana katika
Wafilipi 4:13 imeandikwa kuwa “Nayaweza mambo yote katika YEYE anitiaye
nguvu” Yesu Kristo ndiye atutuaye nguvu.
Yesu Kristo alitoa mwongozo mzuri sana wa
jinsi ya kuishi hapa ulimwenguni aliposema;
“Bali utafuteni KWANZA ufalme wake, na haki
yake; na hayo yote mtazidishiwa” (Mathayo 6:33)
Ukiyaangalia maisha ya watu wengi waliookoka
utadhani Yesu Kristo alisema, “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake;
na hayo yote MTAONDOLEWA.” Inahuzunisha kuona ya kuwa watu wengi wakiokoka
maisha yao yanageuka kuwa duni, wanashindwa kula vizuri, wala kuvaa vizuri.
Ngoja nirudie kusema kuwa SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASKINI. SI MAPENZI YA MUNGU
TUKOSE CHAKULA WALA MAVAZI. Ni Mungu yupi ambaye atawapenda ndege akawavika na
kuwalisha, na akawaacha watoto wake aliowaumba kwa mfano wake wakose chakula na
mavazi?
Mungu wetu tunayemwabudu na kumtumikia katika Kristo Yesu, anapenda tuishi
maisha mazuri, tule, tunywe na kuvaa vizuri. Tunachotakiwa kufanya ni kuutafuta
KWANZA ufalme wake, na haki yake, na hayo yote (chakula na mavazi)
TUTAZIDISHIWA na siyo TUTAONDOLEWA.
Ukiona mtu anasema
ameokoka na halafu anajikuta anakosa chakula na mavazi huku anafanya kazi, basi
ujue anafanya kazi na kukusanya vitu hivyo pasipo Bwana; kwa kuwa asiyekusanya
pamoja na Bwana hutapanya.
FEDHA NA KUPENDA FEDHA
Nimewahi kumsikia mhubiri mmoja akisema; “Fedha ni shina la maovu, kwa
hiyo wakristo wajihadhari nazo.” Na wakristo wengi wamekuwa wakisikika
wakisema hivyo, kwa hiyo wanaogopa kuwa na fedha za kutosha.
Lakini ninaposikia watu wakisema hivi, huwa
najiuliza wanaupata wapi usemi huu? Biblia haisemi; “Fedha ni shina la
maovu.”
Badala yake Biblia inasema hivi;“ Maana shina
moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha;ambayo wengine hali wakiitamani
hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi”(1Timotheo 6:10)
Kupenda fedha ni kuwa na tamaa ya fedha; ni
kuzitamani fedha. Na kupenda fedha huku ndiko shina moja la mabaya ya kila
namna.
Kuwa na fedha nyingi au kidogo siyo dhambi,
kwa kuwa fedha ni mali ya Mungu (Hagai 2:8) Lakini kupenda fedha
nyingi au kidogo ni shina moja la maovu.
Tamaa ya fedha ndiyo inayoleta wizi,
ujambazi, mauaji, dhuluma, kutokutosheka, uchoyo, wivu, uasherati; nakadhalika.
Lakini unaweza kuwa na fedha bila ya kufungwa na roho ya kupenda fedha.
Je! Unafahamu ni kwa nini shetani hapendi
wakristo safi wawe na fedha? Maana ni kazi ya shetani kuwapiga vita
wakristo wanaotaka kujipatia fedha kwa njia ya halali. Akishindwa kuwazuia
kupata fedha; atahakikisha zile fedha walizonazo wanazimaliza haraka hata kwa
matumizi ambayo hawakupanga.
Je! Unafahamu ni kwa nini?
Kwa sababu anafahamu mkristo safi akiwa na
fedha za kutosha, atazitumia hizo kumpiga nazo vita kwa kuihubiri injili! Na
shetani anafahamu kuwa Yesu alisema mwisho hautakuja mpaka injili ihubiriwe
katika mataifa yote. Kwa hiyo anajua akiweza kuwakosesha wakristo fedha za
kutosha ili injili ihubiriwe, yeye anapata muda wa kupumua na kupumzika.
Wengi wameshindwa kujenga makanisa kwa sababu
ya ukosefu wa fedha. Watumishi wa kanisa wanalipwa mishahara kidogo, kwa sababu
ya ukosefu wa fedha. Mikutano ya injili na semina za neno la Mungu hazifanyiki
mara kwa mara kwa kukosa fedha. Wainjilisti wanatafuta fedha za kununulia
vipaza sauti wanakosa. Na matokeo yake ni kazi ya Mungu kupoa.
Je! Unadhani ni nani ambaye anaweza kutoa
fedha yake ili ikahubiri injili kama siyo wakristo wenyewe? Na wakristo
watatoaje fedha kama hawana fedha? Na watakuwaje na fedha, kama wanadhani kuwa
na fedha nyingi ni dhambi?
Na shetani ameutumia mwanya huu kuzitumia
fedha ambazo wanazo watu wasiopenda haki kueneza dhambi na uovu. Je, ni haki
kwa nchi nyingine kutumia ma-billioni ya fedha kutengeza silaha ambazo baadaye
wanaziharibu tena, huku mamillioni ya watu wanakufa kwa njaa na maafa mengine?
Kwa hiyo usikubali unaposikia mtu akisema kuwa na fedha ni vibaya; lakini uwe
mtu wa kutokupenda fedha. Kwa kuwa ukizitamani fedha utajikuta unaanza
kuzitafuta hata kwa njia ambazo ni kinyume cha maadili yetu ya Kikristo; na pia
kinyume cha utu wa mwanadamu.
MASKINI NA TAJIRI
Nafahamu ya kuwa si mpango wa Mungu kwa mtu aliye tajiri kumtawala maskini kwa
sababu ya umaskini wake. Na pia nafahamu si mpango wa Mungu kwa nchi zilizo
tajiri kuzitawala nchi maskini kwa sababu ya umaskini wake.
Lakini ni vizuri tufahamu
uhusiano uliopo kati ya matabaka haya mawili:-
Biblia inasema;“Tajiri
humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.” (Mithali
22:7)
Maneno haya ni kweli kabisa, na mtu ye yote
ambaye ni msomaji wa historia na magazeti, anafahamu majadiliano ya muda mrefu
yaliyopo kati ya nchi tajiri na nchi maskini duniani.
Ukoloni mbaya uliopo sasa hivi kati ya nchi
na nchi, ni ukoloni wa kiuchumi. Katika ukoloni huu wa kiuchumi nchi tajiri
zinatumia utajiri wake katika kuzikandamiza nchi maskini. Na kwa njia hii
mamillioni ya watu wamo katika hali mbaya sana kimaisha.
Na njia kuu ambayo nchi hizi tajiri zinatumia
kuzitawala nchi maskini ni kwa njia ya kuzipa mikopo. Na nchi maskini zote
zimejikuta zimeingia katika utummwa mbaya kwa sababu ya mikopo ambayo
haijajulikana kama inaweza kulipwa yote.
Inakisiwa ya kuwa jumla ya madeni yote ya
nchi zinazoendelea ni mabilioni ya dola za Kimarekani na yanazidi kuongezeka.
Ni kweli kabisa kwamba utajiri huu wa nchi
hizo si wote uliopatikana kwa njia ya halali. Na wafuatiliaji wa mambo ya
uchumi duniani, wanafahamu jinsi nchi hizi zilizoendelea zinavyobuni mbinu
mbalimbali kuzinyonya nchi zinazoendelea.
Ingawa si mapenzi ya Mungu tuwe maskini,
lakini pia si mapenzi ya Mungu tuwe matajiri ili kuwatawala wengine kwa sababu
ya umaskini wao. Ole ni kwa matajiri wanaoutumia utajiri wao kuonea na
kuwafanya wenzao kuwa watumwa.
Mungu anapotupa nguvu za kupata utajiri ndani
ya Kristo ni kwa kusudi muhimu la kuimarisha agano lake la kumhudumia mtu mzima
– kiroho na kimwili.
Ni kweli maskini ana shida, maana hata biblia inasema maneno yake hayasikilizwi
(Mhubiri 9:16). Na hii imejionyesha wazi sana katika maoni na
malalamiko ya nchi maskini ambayo yanapuuzwa na kutosikilizwa na nchi tajiri.
Lakini
hali hii si kwa nchi tu, bali hata katikati yetu humu humu makanisani. Sehemu nyingi
kuna wakristo ambao ni matajiri, na mara kwa mara huwa wanatumia utajiri wao
katika kuwatawala viongozi wa kanisa; na hata wakati mwingine kudiriki hata
kutaka kubadilisha maamuzi ya vikao vya kanisa.
Na kwa upande mwingine viongozi wa sharika wanajikuta wameingiwa na hofu na
kushindwa kuwakemea matajiri hao wakati wanapokwenda kinyume na maadili ya
kikristo. Kama siyo ukoloni wa namna yake ulioingia katika kanisa ni nini basi?
Naamini ya kuwa wachungaji na viongozi, wengi wao wangekuwa na hali nzuri
kiuchumi, baadhi ya matajiri wanaotaka kutawala viongozi wengine wangeshindwa
katika mbinu zao. Au wewe unasemaje?
Shetani amekuwa akijitahidi sana kuwakandamiza wakristo wasiwe matajiri kwa
kutumia njia mbali mbali kwa kutegemea mazingira yalivyo. Mahali pengine
ametumia mifumo na vyombo vya fedha kama mabenki; pengine ametumia serikali,
pengine ametumia mafundisho mabaya kwa wakristo, nakadhalika.
Na shabaha yake ya kufanya hivyo ni:-
(a)
Maneno ya wakristo yasisikilizwe wanapohubiri, kwa kuwa imeaandikwa; “….Walakini
hekima ya maskini hudharauliwa wala maneno yake hayasikilizwi” (Mhubiri 9:19b).
Kwa lugha nyingine maana yake “hayatiliwi maanani.”
(b)
Wakristo waendelee kuwa watumwa ingawa wanadai ya kuwa wamewekwa huru. Kumbuka
imeandikwa hivi; “Tajiri humtawala maskini. Naye akopaye ni mtumwa wake
akopeshaye” (Mithali 22;7)
Na
maneno haya ni kweli kabisa. Hebu nieleze ni nani atakayesikiliza na kuyaamini
maneno ya mchungaji au mwinjilisti au mtumishi yoyote wa Mungu anayesema
mtegemee Yesu katika kila kitu wakati yeye mwenyewe ana nguo yenye viraka!
Jambo la kwanza ambalo msikilizaji atajiuliza ni kwamba kama huyu Yesu
ameshindwa kumpa mtumishi wake nguo nzuri, atawezaje kunisaidia mimi mkristo wa
kawaida?
Kwa hiyo lazima tuwe
waangalifu ili tunayosema yawe sawa na tunavyoishi. Na tuishi sawa sawa na
ahadi za Mungu tunazozisimamia.
Siku moja nilimsikia
mchungaji mmoja mwanafunzi wa chuo kimoja cha biblia akisema hivi; “Kuna mtu
mmoja alikuja kutufundisha kuwa sisi kama wachungaji tusisikitike tunapoona
hatuna nguo nzuri, wala chakula kizuri, wala sabuni nzuri za kuogea kwa sababu
IKO SIKU MOJA VITU HIVI TUTAVITAWALA NA BWANA MBINGUNI”.
Mara moja
nikamkatisha na nikasema; “ Hayo mafundisho si sawa. Unadhani Mungu
aliweka hivi vitu duniani (chakula, mavazi, sabuni) kwa ajili ya shetani na
watu wake? Unadhani mbinguni tukifika tutahitaji tena chakula, mavazi na
sabuni? Hivi vitu Mungu aliviweka kwa ajili yetu tuvitumie wakati huu.”
NANI ANAUPENDA WOKOVU WA KIMASIKINI?
“Nani
anaupenda wokovu wa Ukristo wa kimaskini?” Ukiona mtu amefika hali ya
kujiuliza swali la jinsi hii, ujue ana hali ngumu sana kiuchumi.
Hili swali
nilijikuta najiuliza mwenyewe baada ya kuwa na hali
ngumu sana kimaisha baada kuokoka. Kuna wakati fulani baada ya
kuokoka mimi na mke wangu tulijikuta tumefika mahali pa kukosa hata dawa ya
mswaki, nguo, viatu, na chakula kizuri. Licha ya shida hizi zote bado zilifuata
zingine baada ya ndugu zetu wawili tuliokuwa tunawalipia
masomo yao kufukuzwa na kurudi nyumbani kwa kukosa ada. Na waliambiwa
wasirudi shuleni bila nusu ya ada!
Unadhani
tulikuwa na furaha tena? Ingawa tulikuwa tunasema tumeokoka, na mtu akituambia
‘Bwana asifiwe’ tuliitika ‘Amina’ ndani ya mioyo yetu tulikuwa na vita vikali
na maswali mengi.
Ni vigumu
kuieleza hali hiyo tuliyoipitia ilivyokuwa ngumu kwa maneno. Lakini utaelewa
mtu mwenye familia anavyojisikia anapoona anakosa hata fedha za kuwanunulia mke
na watoto wake chakula licha ya mavazi. Wakati huo tulikuwa na mtoto mmoja.
Hali
ilivyozidi kuwa ngumu, ndivyo nilivyozidi kusongwa na mawazo. Ilifika wakati
ambapo nilikuwa naona aibu hata kukaa sebuleni, maana niliogopa hata
kuwaangalia wale vijana waliofukuzwa shule, nikijua kuwa wataniangalia kwa
macho ya huruma ili niwape ada warudi shule. Lakini si kwamba nilikuwa siwahurumii,
bali sikuwa na fedha za kuwapa.
Ningeanzaje
kuwaambia kuwa sina fedha, wakati wanajua nafanya kazi, na pia waliona nilikuwa
na fedha nyingi kabla sijaokoka? Jambo hili lilinifanya niwaze sana.
Inakuwaje kabla sijaokoka nilikuwa na fedha nyingi na baada ya kuokoka najikuta
nimefilisika? Ingawa ni kweli kwamba kabla ya kuokoka fedha zingine nilizipata
kwa njia zilizo kinyume cha ukristo lakini nilikuwa nazo. Na baada ya kuokoka
ilibidi niziache njia hizo – na matokeo yake nilijikuta nimefilisika.
Lakini
nilikuwa nimesoma katika Hagai 2:8 kuwa fedha na dhahabu ni mali ya
Mungu. Na pia nilijua kuwa vyote vya Mungu ni vyangu nikiwa ndani ya Kristo.
Kwa hiyo ilikuwa vigumu kuelewa kwa nini Mungu aseme fedha
ni mali yake, halafu mimi niliye mtoto wake nisiwe nazo.
Ningewezaje
kusema wokovu ni mzuri wakati baada ya kuokoka nimejikuta sina fedha za kutosha
kununua chakula, nguo, dawa ya mswaki na hata kukosa ada za watoto! Je ndivyo
Mungu anavyotaka tuwe baada ya kuokoka?
Wakati huo
ndipo nilipoelewa kwa nini wana wa Israeli waliyakumbuka masufuria ya nyama ya
Misri, ingawa walikula nyama hizo wakiwa utumwani. Ni rahisi sana mtu
aliyeokoka kurudia njia au maisha mabaya ya kutafuta fedha kwa njia zilizo kinyume
cha ukristo anapokuta anabanwa na matatizo ya kiuchumi maishani mwake. Na hata
wakati mwingine unakesha katika maombi ili kumlilia Mungu akupe chakula na
mavazi unaona kama vile hasikii.
Nilipokuwa
nasumbuliwa na hali hii ndipo nilipojikuta najiuliza mwenyewe; “ Nani anaupenda
wokovu wa kimaskini?” Nilijikuta siupendi kabisa. Ni wokovu gani huu ambao
haunisaidii hata kutunza familia yangu?
Siku moja
nilimuuliza mke wangu; nikasema; “Je! wewe unaupenda wokovu wa kimaskini?”
Akajibu;
“Hapa, siupendi!”
Nikasema;
“Naona tuna mawazo yanayofanana. Kwa hiyo naona ni muhimu tumuulize Mungu
katika maombi kwa nini tulipokuwa kwa shetani tulikuwa na fedha za kutosha,
lakini baada ya kuokoka na kuja kwake tunajikuta hatuna fedha hata za kununulia
vitu muhimu?”
Baada ya
kukubaliana hayo, mimi na mke wangu tulianza kumwomba Mungu kwa mfululizo wa
siku tatu juu ya jambo moja hilo hilo. Namshukuru Mungu kwa kunipa
mke ambaye aliweza kusimama pamoja nami katika maombi juu ya jambo hili. Sijui
ningekuwa na hali gani kama angelalamika. Namshukuru Mungu mke wangu
hakulalamika bali ALIOMBA PAMOJA NAMI.
Mungu
alitujibu maombi na akaanza kutufundisha mambo mengi ambayo mengine
nawashirikisha katika ujumbe huu.
Tulijua
hakika kuwa hayakuwa MAPENZI YA MUNGU tuwe na hali ngumu ya kimaisha namna hiyo
– kukosa fedha za kutosha kununulia nguo, chakula na vitu vingine muhimu. Na
baada ya kuyaweka katika matendo yale tuliyoambiwa na Bwana yaliyo katika neno
lake, hali yetu ilibadilika. Na matatizo tuliyokuwa nayo wakati ule yakaisha.
Tukaanza kuona furaha tena katika maisha haya ya wokovu.
Ni vizuri
kujua kuwa Mungu wetu hapendi tuwe maskini. Wala hapendi wokovu wa kimaskini!
Ndiyo maana alimtuma Mwana wake wa Pekee, Yesu Kristo kutukomboa.
Kwa
kukumbusha tu, Yesu Kristo aliyafanya yafuatayo kwa kufa na kufufuka kwake:
"Yesu
Kristo alifanyika dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tuhesabiwe haki bure ndani
yake ya kusimama tena mbele ya Mungu"
(2Wakorintho 5:21)
"Yesu
Kristo aliuchukua udhaifu wetu, ili katika mambo yote tuzitegemee nguvu
zake" (Mathayo 8:17; Wafilipi 4:13)
Yesu Kristo
aliyachukua magonjwa yetu, ili tusitawaliwe na magonjwa tena na kwa kupigwa
kwake tumepona (Isaya 53:4,5; Mathayo 8:17; 1 Petro 2:24)
Yesu Kristo aliyachukua masikitiko na huzuni zetu, ili tukae katika amani yake
ipitayo fahamu zote (Isaya 53:34; Wafilipi 4:6,7)
Yesu Kristo
alikuwa maskini kwa ajili yetu ingawa alikuwa tajiri, ili sisi tupate kuwa
matajiri katika Yeye (2 Wakorintho 8:9)
Ndiyo maana matunga Zaburi 23 aliandika hivi:
“Bwana ndiye mchungaji wangu, SITAPUNGUKIWA NA KITU.Katika malisho ya majani
mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi
yangu; na kuniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake …. Hakika
WEMA
NA FADHILI zitanifuata siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani
mwa Bwana milele”.
Ni
rahisi sana kusema. “Bwana ndiye mchungaji wangu, SITAPUNGUKIWA NA
KITU, lakini je! Ni kweli hujapungukiwa na kitu? Je! Zaburi hii ni ya kweli, au
ni maneno mazuri tu ya kutungia nyimbo?
Lakini
napenda kukutia moyo kuwa maneno haya ni ya kweli, ukikaa ndani ya Kristo
hutapungukiwa na kitu. Ndiyo maana Mungu alimwambia Yoshua ya kuwa atii maagizo
yake yote na kuyafanya HATAMPUNGUKIA WALA KUMUACHA (Yoshua 1:5)
Kwa kuwa
maneno haya ni ya kweli, mbona basi wakristo wengi WAMEPUNGUKIWA NA VITU?
Tatizo haliko kwa Mungu, bali kwetu sisi. Na tuwe watendaji wa neno na tutaona
mafanikio.
WAJIBU WA WAKRISTO:
Ni wajibu wa
wakristo (a) kusaidiana sisi wenyewe kiuchumi; na (b) Kuwasaidia kiuchumi watu
wengine wasio wakristo. Kuna wakati fulani mtu mmoja alikuja kwangu kuomba
ushauri.
Nikamuuliza.
“Una tatizo gani linalokukabili?”
Akasema; “
Baada ya kuokoka ilibidi niache njia fulani fulani ambazo zilikuwa zinanisaidia
kupata fedha kwa kuwa zilikuwa ni kinyume cha maadili ya kikristo. Lakini sasa
naona napata shida, sina fedha za chakula, wala sijui kodi ya nyumba
mwezi huu nitapata wapi. Licha ya hayo, wale niliowakopa fedha kufanyia
biashara hizo nilizoziacha wananidai fedha zao. Hata naogopa kukutana nao. Hebu
nisaidie mawazo, najua nimeokoka kweli, lakini NITAISHIJE KATIKA HALI HII?”
Unadhani
swali lilikuwa jepesi kujibu? Si swala la kumwambia tuombe halafu umwache aende
zake! Yeye anachotaka baada ya kuomba aone msaada unamjia. La sivyo maombi hayo
yanakosa maana kwake.
Swali hili
“Nitaishije katika hali hii?” Linawasumbua walio wakristo wengi siku hizi. Na
umefika wakati wa kulijibu.
Ngoja
nikuulize swali jingine. Unadhani mwanamke ambaye anafanya uasherati ili kupata
fedha za kuwalishia watoto wake hajui kuwa uasherati ni dhambi? Nina uhakika
anajua kwa kuwa kuna mwingine hata kama anafanya hayo hakosi kila
jumapili kanisani, na wakati mwingine hutoa sadaka kwa fedha hiyo hiyo.
Unadhani hajui kuwa uasherati ni dhambi? Unadhani hamwelewi mchungaji anaposema
acheni dhambi? Unadhani haogopi magonjwa ya zinaa? Unadhani anapenda kufanya
hivyo? Nina hakika walio wengi hawapendi kufanya hivyo. Lakini jambo
linalomsumbua, akiacha uasherati atapata wapi fedha za kuwatunza watoto wake?
Nina uhakika akijibiwa swali hili ni rahisi kuacha tabia hiyo chafu.
Wasichana
wengi mashuleni wamejikuta wamebeba mimba na kuharibu usichana wao kwa
kudanganywa na fedha wanazozihitaji kwa ajili ya kununulia mafuta ya kupaka,
nguo, na kutengeneza mitindo ya nywele.
Vijana wengi
wa kiume wamejikuta wamejiingiza katika biashara haramu kwa sababu ya kutaka
utajiri wa haraka haraka.
Kwa sababu
ya kutokujua la kufanya wakristo wengi wamepoteza ushuhuda wao kwa sababu ya
matatizo ya kiuchumi.
Wakristo
wenzetu walifanyaje? Tusome kitabu cha Matendo ya Mitume 4:32,34,35.
“Na jamii ya
watu waliamini (Wakristo) walikuwa na MOYO MMOJA NA ROHO MOJA; wala hapana mmoja
aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake
mwenyewe; bali walikuwa na VITU VYOTE SHIRIKA. WALA HAPAKUWA NA
MTU MMOJA MIONGONI MWAO MWENYE MAHITAJI; kwa sababu watu wote
waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu
vile vilivyouzwa; wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa KWA
KADRI YA ALIVYOHITAJI”
Utaona
katika habari hii ya kuwa kwa sababu ya Ukarimu na kutokuwa na ubinafsi
wakristo hao waliweza kupambana na tatizo la umaskini katikati yao. Ndiyo
maana ikandikwa kuwa; “WALA HAPAKUWA NA MTU MMOJA MIONGONI MWAO MWENYE
MAHITAJI”. Jina la Bwana libarikiwe!
Matokeo ya
usharika namna hii ni haya; “Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu
kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote” (Matendo ya
Mitume 4:33)
Je! Siku
hizi hakuna wakristo wenye mahitaji kati yetu? Na tunafanya nini ili
kuwasaidia? Je! Kuwaombea tu kunatosha? Je! Unashangaa kwa nini ushuhuda wa
kufufuka kwake Yesu hautangazwi kwa nguvu na wakristo? Nadhani wakristo wengi
wanatumia muda wao mwingi sana kujitafutia
mahitaji yao kiasi ambacho muda unaobaki hautoshi kufanya kazi ya
kushuhudia.
Wenzetu
walisaidiana, na sisi tusaidiane. Wazazi mara nyingi huwa wanawasaidia vijana wao
waliowaoza kuanza maisha mapya. Na fahamu kuwa wokovu ni maisha mapya.
Tunawajibika sana kuwasaidia wale wanaookoka kiroho na kimwili kuanza
maisha mapya ndani ya Kristo. Kwa kukosa msaada wa kiuchumi, wengi wamepoa na
kurudi nyuma.
Niliwahi
kushirikishwa ushuhuda mmoja ambao naamini utakusaidia kukuelewesha jambo hili
ninalokuambia.
Kuna mtu
mmoja aliokoka baada ya muda mrefu kuwa mganga wa kienyeji na mchawi. Baada ya
kuokoka ilibidi aache uchawi na uganga wa kienyeji, shughuli hizi ndizo
zilizokuwa zinamsaidia kupata fedha ya matumizi.
Baada ya
kukaa miezi michache katika wokovu, bila ya kuwa na njia nyingine ya kupata
fedha, ilibidi atumie akiba yote aliyokuwa nayo. Baada ya hiyo akiba kuisha
akaanza kupata shida namna ya kuishi.
Akiwa katika
mahangaiko hayo, wakaja watu nyumbani kwake wakiomba msaada wa kutibiwa
magonjwa yao. Hao watu walisikia kuwa yeye ni mganga wa kienyeji, wala
hawakujua kuwa alikuwa ameokoka na kuacha uganga huo.
Kwa sababu
ya kukosa fedha, huyo mtu aliyeokoka akawaza moyoni mwake; “Hawa watu hawajui
kuwa nimeokoka, kwa hiyo hakuna haja ya kuwaambia, kwani kuna ubaya gani
nikienda kuwachimbia dawa ninazozifahamu halafu wanipe fedha inisaidie?”
Kwa hiyo akaenda
akawachimbia hizo dawa akawapa. Na hao watu wakaondoka baada ya kumlipa fedha.
Lakini usiku, huyo aliyeokoka alipokuwa amelala aliona katika maono. Katika
maono hayo akayaona majini mawili yaliyokuwa yanamsaidia katika uchawi zamani
kabla ya hajaokoka. Hayo majini yakasema; “Tulikwaambia hutafanikiwa katika
wokovu, sisi ndiyo tumekufilisi mali yako. Na pia sisi ndiyo
tuliowatuma wale wagonjwa waje kwako. Ulipochima zile dawa ukatuita tulikokuwa.
Sasa tumekuja, mwache Yesu njoo kwetu nasi tutakutajirisha”.
Huyo mtu
aliyeokoka aliposikia hayo, akatambua kosa lake, na mara hiyo akalikumbuka jina
la Yesu Kristo. Kwa hiyo akayakemea yale majini nayo yakatoweka. Akamka akiwa
anatetemeka.
Kama asingelikumbuka
uwezo wa jina la Yesu Kristo, angefanya nini? Naamini kama angepata msaada wa
mahitaji yake toka kwa wakristo wenzake, asingebanwa na mtego huo. Wakristo
naomba kuwakumbusha kusaidiana. Ni muhimu sana kwa maisha yetu ya
kila siku.
Ndiyo
maana Mtume Paulo aliongozwa na Roho Mtakatifu kuandika hivi:
“Kwa
habari za kuwahudumia watakatifu (Wakristo) sina haja ya kuwaandikia.
Maana najua utayari wenu, ninaojisifia kwa ajili yenu kwa Wamakedonia,
kwamba Akaya ilikuwa tayari tangu mwaka mzima; na bidii yenu imewatia moyo
wengi wao ……. Maana utumishi wa huduma hii hauwatimizii watakatifu
(Wakristo) riziki walizopungukiwa tu, bali huzidi sana kuwa na faida kwa
shukrani nyingi apewazo Mungu, kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo,
wanamtukuza Mungu kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili
ya Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote” (2Wakorintho
9:1,2,12 – 15)
Ndiyo maana
pia katika makanisa kuna mgawanyiko wa huduma. Kuna wengine
kazi yao ni kuhubiri na kuwaambia watu waache dhambi kama,
uasherati na wizi. Ni wajibu wa wale wanaoshughulika na mambo ya miradi ya
maendeleo katika kanisa ni kusaidiana na wahubiri hao kuwaongoza watu waishije
baada ya kuacha uasherati na wizi.
Napenda
kukuhimiza hata wewe unayeyasoma haya kuwa, ukiona mwenzako ni mhitaji wa kitu
fulani ambacho unacho, usisite kumsaidia. Kumbuka huduma hii ina thawabu
yake kama Mtume Paulo anavyosema.
Hebu jibu
swali hili; “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake
ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake
huyo?" (1Yohana 3:17)
Mzee Yohana
anatushauri anasema, “Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi,
bali kwa tendo na kweli” (1Yohana 3:18).
Ni kweli
Bwana Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alikuwa maskini, lakini baada ya
kufufuka alirudishiwa utajiri wake. Ndiyo maana Mtume Paulo anazungumzia juu
ya “……… utajiri wake Kristo usiopimika” (Waefeso 3:8). Na katika
Wafilipi 4:19 tunasoma hivi; “Na Mungu wangu atawajazeni kila
mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo
Yesu”.
Kumbuka ya
kuwa; Yesu Kristo alichukua madhaifu yetu na magonjwa yetu yote, na kwa kupigwa
kwake sisi tumepona (Isaya 53:5; Mathayo 8:16, 17; 1Petro 2:24). Na kwa kujua
hili kanisa linajihusisha na kuombea wagonjwa na kutoa huduma za afya kwa
wagonjwa.
Kumbuka ya
kuwa; Yesu Kristo alichukua dhambi zetu na akafanyika dhambi kwa ajili
yetu, “Ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye” (2
Wakorintho 5:21). Na kwa kujua hili kanisa linahubiri habari za ondoleo la
dhambi kwa ye yote atakayemwamini Kristo.
Kumbuka ya
kuwa; Yesu Kristo alikuwa maskini, ingawa alikuwa tajiri, ili kwa umaskini
wake sisi tupate kuwa matajiri (2Wakorintho 5:21). Na kwa kujua hili
kanisa linajihusisha na miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili mtu aondokane na
umaskini. Wakristo binafsi pia wanashauriwa kuwa na miradi isiyovunja maadili
ya kikristo, ili waondokane na umaskini.
SADAKA NA WOKOVU
“Palikuwa na mtu Kaisaria jina lake Kornelio, akida wa
kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake
yote, naye alikuwa akiwapa watu SADAKA NYINGI, na kumwomba Mungu daima. Akaona
katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu,
akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, kuna
nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na SADAKA ZAKO zimefika juu na kuwa
ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye
Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa
ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani; ATAKUAMBIA YAKUPASAYO KUTENDA” (Matendo
ya Mitume 10:1 – 6).
Tabia hii ya Kornelio ya kuwa mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake
yote, na pia tabia ya utoaji wa sadaka na kumwomba Mungu daima, inaonyesha wazi
kuwa Kornelio alimpenda Mungu sana na alikuwa anatafuta namna
yakukubalika mbele zake na namna ya kumpendeza Yeye.
Tungezungumza kwa lugha nyepesi zaidi, ni kwamba alitaka kwa MATENDO YAKE aende
mbinguni na kuurithi Uzima wa Milele baada ya kufa kwake . Kwa kifupi
alimtafuta Mungu kwa njia ya Matendo.
Hii ina maana ya kuwa Kornelio alitaka kuvuna baraka za Agano Jipya
katika damu Yesu, wa kutumia njia za kupendeza Mungu zilizomo katika Agano la
Kale.
Tena ingawa yeye hakuwa Myahudi kwa kuzaliwa, alitaka sana kuvuna
baraka ambazo Mungu aliahidi juu ya Wayahudi.
Mpaka hivi leo kuna watu wengi wanataka kuvuna baraka toka kwa Mungu bila
kutumia utaratibu aliouweka Mungu wa kuzipokea. Ni
vigumu sana kupokea ahadi za Mungu nje ya mpango wake.
Huwezi kupokea ahadi za agano la kale kwa kutumia mbini za agano la kale na
huku sasa hivi tumo katika kipindi cha agano jipya.
Baraka zote zilizomo katika agano la kale aliahidiwa Ibrahimu na uzao wake
MILELE. Soma mwenyewe Mwanzo sura ya 17 na 22. Kwa hiyo ukitaka kupokea baraka
za agano la kale lililofungwa kati ya Mungu na Ibrahimu, inabidi uwe mzao au
mtoto wa Ibrahim. - Kornelio hakufahamu hili; hata leo hii wengi hawafahamu.
Baraka zote zilizomo katika agano jipya zimeahidiwa wale walio ndani ya Kristo
– waliotoa maisha yao kwa Yesu kama vile Yesu Kristo alivyotoa maisha
yake kwa ajili yao.
Ni vigumu kupokea baraka za ahadi za agano la kale na zile za agano jipya NJE
YA YESU KRISTO. Imeandikwa hivi katika Wagalatia 3:13,14,29;
“Kristo alitukomboa katika laana ya torati,
kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, baraka ya Ibrahimu
IWAFIKILIE MATAIFA KATIKA YESU KRISTO, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya
imani…… Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na
warithi sawasawa na ahadi. "
Ndiyo maana Mungu alimtuma Malaika
wake ili amwambie Kornelio kuwa amwite Simon Petro ili awaeleze habari za Yesu
Kristo – ili baraka ya Ibrahimu iwafikie na wapate kupokea ahadi ya Roho kwa
njia ya imani – SIYO KWA MATENDO PEKE YAKE.
Jambo ambalo
Mungu alitaka Kornelio ajue na sisi pia tujue ni kuwa matendo mema, maombi na
SADAKA bila “kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani” yaani kuzaliwa
mara ya pili kwa Roho au kuokoka – haitoshi kumpendeza Mungu, wala
kukubalika mbele zake au kuhesabiwa haki.
Ndiyo maana
Yesu Kristo alimwambia Nikodemo, yule Farisayo kuwa “Mtu asipozaliwa mara
ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu ….. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia,
HAMNA BUDI kuzaliwa mara ya pili”(Yohana 3:3,7).
Haya maneno “Hamna Budi” maana yake ni “lazima” kwa hiyo
Yesu Kristo alikuwa anasema “…… LAZIMA kuzaliwa mara ya pili”.
Yesu Kristo alikuwa anasisitiza kwa Nikodemo, na hata kwetu sote tunaotaka
kuurithi ufalme wa Mungu, kuwa hakuna njia nyingine isipokuwa LAZIMA kuzaliwa
mara ya pili kwa Roho (au kwa maneno mengine) LAZIMA Kuokoka!
IMANI NA MATENDO
Matendo peke yake hayatoshi kukupa
ufalme wa Mungu. Kuna watu wengi sana ambao ni
waaminifu sana katika kusali na kumtolea Mungu sadaka, lakini hawakubaliani
na jambo kuokoka. Wanaona kuwa wao tayari wameokoka kwa sababu tu wanasali,
wanatoa sadaka na kujitahidi kuishi katika matendo mema. Hebu soma
maneno ya mistari hii uone yanavyopingana na msimamo huu;
“Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya
imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; WALA SI KWA
MATENDO, mtu awaye yote asije akajisifu” (Waefeso 2:8,9)
Tunaokoka kwa njia ya imani itendayo kazi katika Yesu Kristo, “Wala si kwa
matendo, mtu awaye yote asije akajisifu”. Matendo yana faida zaidi kwa mtu
baada ya kuokoka. Na pia imani bila matendo, imani hiyo imekufa nafsini mwake.
Biblia inasema hivi:
“Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana
matendo? Je! ile imani yaweza kumwokoa?…. Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina
matendo, imekufa nafsini mwake. Lakini mtu atasema, wewe unayo imani, nami
ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha IMANI
YANGU KWA NJIA YA MATENDO YANGU …….. Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa,
vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa” (Yakobo 2:14,17,18,26).
Jambo ambalo Yakobo alikuwa
anasisitiza hapa ni kutaka kuwaonya watu kuwa kusema wewe ni mkristo na huku
matendo yako hayalingani na ushuhuda wa mdomo wako ni bure. Wokovu uonekane
katika maisha yetu kila siku – la sivyo imani tuliyo nayo inakosa kuzaa matunda
ya uzima wa milele. Ndiyo maana Yesu Kristo aliwahi kuzungumza juu ya kukatwa
kwa tawi (Mkristo) lisilo zaa, soma Yohana 15:1-8 ili upate picha zaidi juu ya
jambo hili.
CHUKUA HATUA LEO
Malaika alimwambia Kornelio atume watu wakamwite Simoni aitwaye Petro ili
AMWAMBIE YAMPASAYO KUTENDA. Mungu kwa uweza wa Roho wake Mtakatifu amekuletea
maneno haya mkononi mwako ili UFAHAMU YAKUPASAYO KUTENDA.
Kama hujaokoka
na unadhani unaweza kuokoka kwa kutoa sadaka nyingi NAKUSHAURI KWA JINA LA YESU
KRISTO WA NAZARETI uombe sala hii kwa sauti, ili utubu na kumpa Yesu Kristo
maisha yako leo. HALAFU endelea kutoa sadaka nyingi ukiwa ndani ya Yesu Kristo.
Omba sala hii kwa sauti; “Mungu Baba, unisamehe dhambi zangu zote
nilizokukosea katika maisha yangu. Ninatubu kwako. Nitakase kwa damu ya Yesu
Kristo. Bwana Yesu Kristo nimefungua moyo wangu nakukaribisha uingie ndani
yangu, kwa uwezo wa Roho wako. Uwe Bwana na Mwokozi wa maisha yangu – sasa na
hata milele. Asante kwa kunisamehe dhambi na kuniokoa. Amina”.
Ikiwa umeisema sala hii kwa uaminifu, basi umefanyika kiumbe kipya – umezaliwa
mara ya pili na Mungu hakumbuki dhambi zako tena. Soma 2Wakorintho 5:17,
Waebrania 8:12. Karibu sana katika ufalme wa Mungu kwa jina la Yesu
Kristo!
Hili ndilo lililotokea kwa Kornelio na jamaa yake, Simoni Petro alipofika kwao
aliwaambia habari za Yesu Kristo – walisikia maneno hayo wakamwamini Yesu na
kujazwa na nguvu za Roho Mtakatifu wakati huo huo.
UCHUMI WA UFALME WA MBINGUNI
Mama mmoja aliyekuwa na watoto sita (lakini
alikuwa hajaolewa), alipelekwa na mwenzake kwa Askofu wa dhehebu lao ili wapate
msaada kwa kuwa walikuwa na maisha ya shida sana. Yule mama pamoja na watoto
wake sita walikuwa wanakaa katika nyumba ya makaratasi, na hawakuwa na chakula
cha kutosha.
Askofu alimuuliza yule mama amewapateje wale
watoto wote sita na huku alikuwa hajaolewa.
Yule mama akajibu akasema; "Mtoto wa
kwanza nilimpata kwa kuwa nilikuwa nataka mtoto, niliona nazeeka bila ya
kuolewa nikaona nizae mtoto, Lakini mtoto wa pili nilimpata wakati nilipokuwa
natafuta chakula cha mtoto wa kwanza. Mtoto wa tatu nilimpata nilipokuwa
natafuta chakula cha watoto wawili niliokuwa nao. Na hali hii imeendelea mpaka
sasa nina watoto sita – na sijui nitaendelea na hali hii mpaka lini".
Ni wazi kabisa si mapenzi ya Mungu huyu mama
aishi maisha ya namna hiyo. Vikwazo vya uchumi ambavyo vilimzunguka yule mama
na watoto wake vilitoka kwa ibilisi.
"Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa
maarifa ……." (Hosea 4:6). Maneno haya yaliyosemwa na Mungu kwa kinywa
cha Nabii Hosea yana ukweli ndani yake hata hivi leo. Watu
wengi sana siku hizi wanaangamizwa, wanadhulumiwa, wanahuzunishwa na
maisha kwa sababu tu wamekosa kuyajua maarifa ya Mungu yaliyomo katika Neno
lake.
Wakati fulani nilikuwa nafundisha katika
semina moja juu ya uhusiano wa maendeleo ya mtu na Wokovu, na wakati wa kipindi
cha majadiliano Mchungaji mmoja akatueleza habari iliyotufikirisha sana.
Akasema ya kuwa katika kanisa alilokuwa
analihudumia miaka ya nyuma aliwahi kufuatwa na mama mmoja wa usharika huo
ambaye alikisema ya kuwa yeye alikuwa mmoja wa wakina mama thelathini ambao
hawashiriki chakula cha Bwana kwa kuwa walikuwa wanaishi hapo mjini kwa njia za
umalaya. Ombi lao kwa mchungaji wao lilikuwa ni kwamba akiweza kuwasaidia
kupata kazi za halali waache umalaya. Wao wametafuta kazi bila ya mafanikio, na
wanafanya umalaya si kwa sababu wanapenda, bali kwa kuwa hawakuwa na njia
nyingine ya kupatia fedha.
Ni jambo la kumshukuru Mungu, ya kuwa
mchungaji yule aliweza kuwatafutia kazi wale wakina mama wote katika kiwanda
kimoja, na maisha yao yakabadilika wakaacha umalaya, na kuishi maisha
ya kikristo yenye ushuhuda.
Ni watu wangapi ambo wanaishi
maisha yao kinyume na maadili ya kikristo ili kupata fedha za
kuwasaidia kila siku? – Ni wazi kuwa ni wengi. Je! hawawezi wakapata
riziki yao bila kudhulumu au kuiba au kudanganya au kuzini? – Ni wazi
kuwa wanaweza. Sasa, ni kwa nini wanaishi kwa jinsi hiyo?
Jambo ambalo watu wanahitaji kujua ni kuwa
baba wa uongo yaani shetani amewadanganya kwenye mawazo ya kuwa hakuna njia
nyingine ya halali ya kupatia fedha isipokuwa hizo. Na shetani anausimamia
uongo huo ili uonekane kuwa ni kweli kwa kuwawekea watu hasa wakristo vikwazo
vigumu vya kiuchumi.
Unaweza ukawa unajiuliza vikwazo hivyo ni
vipi? Vikwazo hivi vinatofautiana katika watu mbalimbali na mahali mbalimbali.
Kuna watu wengine wataona hakuna mradi wa halali wanaoufanya unaofanikiwa.
Mwingine miradi yake inafanikiwa, lakini fedha yote inaishia kutafutia matibabu
ya magonjwa yaliyomo ndani ya nyumba yake ambayo hayaishi.
Mwingine anapata magari mengi, lakini
hayaishi kupata pancha na kuharibika au kuanguka. Mara nyingi utawasikia watu
wa jinsi hii wanasema wana mkosi. Kwa kweli si mkosi bali vikwazo vya kiuchumi
toka kwa shetani ili ushindwe maisha na UANZE KUTAFUTA MAISHA MAZURI KWA NJIA
ZILIZO KINYUME NA MAADILI YA KIKRISTO YALIYO MATAKATIFU.
Jambo ambalo wakristo wengi hawalifahamu
Mimi na mke wangu miaka ya mwanzo tulipookoka
hasa mwaka 1984 na 1985 tulikumbana na vikwazo vigumu sana vya
kiuchumi. Tuliona jinsi maisha yalivyokuwa yanarudi nyuma – fedha tuliishiwa,
chakula tuliishiwa, nguo tuliishiwa, vitu ndani vilianza kuharibika na hatukuwa
na fedha za kuvitengenezea. Tulijaribu kulima bustani za mboga, hazikufanikiwa.
Tulijaribu kupika chapati za kuuza, hazikununuliwa zikaharibika tukazitupa.
Kwa kifupi tuliona maisha ya wokovu kuwa ni
magumu, ya shida na ya kimaskini sana. Tulishindwa hata namna ya
kuwasaidia ndugu zetu vizuri. Hali hii ilitutia uchungu sana. Watu
hawakufahamu ya kuwa hali hii ilikuwa inatunyima amani ya kweli ya wokovu – kwa
kuwa tulijitahidi kuwachangamkia wote ili kuficha mapambano tuliyokuwa nayo
kimaisha.
Ilikuwa ni vigumu sana kuishi
maisha ya ushuhuda mzuri wa kikristo katikati ya mahitaji
makubwa kama hayo tuliyokuwa nayo.
Tulijua kuwa Zaburi 23:1 inasema, "Bwana
ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu". Lakini tulikuwa
tumepungukiwa na vitu vingi vya lazima katika maisha. Hatukufahamu kwa nini
sisi kama kondoo wa Kristo tulikuwa tumepungukiwa namna hiyo!
Tulikuwa tunasoma lakini tunashindwa
kumwelewa Mtume Paulo alipokuwa anasema katika Wafilipi 4:12 kuwa; "najua
kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote,
nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa".
Tuliona ya kuwa Mtume Paulo aliweza kuwa na
amani na ushindi katika hali yo yote aliyokuwa nayo – hata katika upungufu.
Sisi tulikosa amani tulipokuwa tumepungukiwa! Na hili jambo
lilitusumbua sana.
Tulikuwa tunafurahi tunaposoma mstari kama ufuatao; "
…..vyote ni vyenu …. Vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni
vyenu, nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu" (Wakorintho
3:21,22). Tulikuwa tunafurahi kwa kuwa maneno haya yanatupa uhalali wa kumiliki
vitu vilivyo vya Mungu. Kwa mfano Hagai 2:8 inasema "Fedha
ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa
Majeshi." Pia, Zaburi 24:1 inasema "Nchi na vyote
viijazavyo ni mali ya Bwana …" Lakini jambo lililotusumbua
ni kwamba ingawa mistari hiyo ilitupa umilikaji juu ya fedha, dhahabu na vyote
viijazavyo nchi ili tuvitumie – SISI HATUKUWA NAVYO WALA HATUKUJUA
TUTAVIPATAJE!
Tulifahamu ya kuwa ni mapenzi ya Mungu
tufanikiwe katika mahitaji ya kiroho na mahitaji ya mavazi, chakula, na malazi;
soma kitabu cha 3 Yohana 1:2. Kwa hiyo tulikuwa na hamu kubwa ya kufanikiwa.
Tulitamani sana kuona maneno ya
Wafilipi 4:19 yanatimia kwetu – nayo yanasema hivi;
"Na Mungu wangu atawajazeni kila
mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo
Yesu".
Hali hii ilitufanya tuingie katika maombi
mazito, ili kumuuliza Mungu njia na namna ya kuondokana na hali tuliyokuwa
nayo.
Mambo makubwa matatu yafuatayo, Roho wa Mungu
alituambia kuwa ni chanzo cha matatizo yaliyokuwa yanatukabili: Alituambia
yafuatayo:
Kuwa, ingawa tumezaliwa mara ya pili na
kuingizwa katika ufalme wa Mungu – tulikuwa bado tunategemea utaratibu wa
uchumi wa duniani badala ya kutumia na kutegemea utaratibu wa uchumi wa
mbinguni;
Kuwa, tulikuwa tunapenda kupokea bila ya kuwa
watoaji, na pia tulitaka kuvuna tusichokipanda. Roho Mtakatifu aliuliza swali,
Je! unaweza kwenda kwenye bustani yako kuchuma nyanya huku ukijua kuwa hujawahi
kupanda nyanya? Ni wazi kuwa jibu lilikuwa ni hapana.
Kuwa, hatujafahamu ya kuwa adui yetu ibilisi
ndiye chanzo cha mahangaiko na mafadhaiko yaliyoambatana na kupungukiwa
mahitaji katika maisha. Na pia tulikuwa hatutumii silaha tulizopewa ili
kuzivunja kazi za ibilisi katika maisha yetu.
Baada ya kupokea majibu hayo kutoka kwa
Mungu, tulitubu na kuomba msamaha. Tuliendelea kumwomba Mungu atufundishe na
atuongoze katika kuishi maisha ya kutumia na kutegemea utaratibu wa uchumi wa
ufalme wa mbinguni.
Mafundisho tuliyoyapata yalituondoa katika
mahangaiko ya kupungukiwa na kutuingiza katika furaha na amani ya mafanikio
NDANI YA KRISTO.
Ndiyo maana tumechukua hatua hii chini ya
uongozi wa Roho Mtakatifu kukushirikisha baadhi ya mafundisho hayo ili ikiwa
umo katika hali ya mahangaiko ya kupungukiwa na mahitaji muhimu ya maisha upate
msaada wa kuondokana nayo.
Kumbuka ni mapenzi ya Mungu ndani ya Kristo
kuwa ufanikiwe na uishi maisha ya ushindi katika maeneo yote ya maisha yako na
katika siku zote utakazoishi juu ya nchi.
Mwenye haki ataishi kwa imani
Nabii Habakuki aliishi katika kipindi
kilichokuwa kigumu sana kiuchumi. Hali hii iliwafanya watu wengi
kuingia katika dhuluma, udanganyifu na mambo mengine maovu ili tu waweze
kuishi.
Lakini kilichoumiza moyo wa Nabii Habakuki ni
kuona kuwa kulikuwa na watu wachache ambao hawakufuata mambo maovu – lakini
waliishi maisha magumu na kuonewa na matajiri wa wakati huo. Hali hii ilimfanya
Nabii Habakuki aingie katika maombi ya kumlalamikia Mungu, huku akihitaji kujua
mpango wa Mungu juu ya watu waliosimama upande wake. Soma kitabu cha Habakuki
sura ya 1 na 2.
Kati ya jibu ambalo Mungu alimpa Nabii
Habakuki juu ya maisha ya watu wake katikati ya hali ngumu ya uchumi ni maneno
haya;
"….mwenye haki ataishi kwa imani
yake" (Habakuki 2:4)
Huu ndio uliokuwa mpango wake kwa watu wake
wakati ule ili uwasaidie kuishi katikati ya dhuluma na maovu yanayotokana na
hali ngumu ya uchumi.
Katika siku hizi za mwisho, kumetabiriwa
kutokea tena hali ngumu ya uchumi inayoambatana na dhuluma pamoja na maovu
mbalimbali. Mungu amekwisha andaa mpango mzuri kwa ajili ya wote watakaoipokea
na kuikiri injili ya Kristo inayookoa. Na mpango huu ni sawa na ule aliopewa
Nabii Habakuki.
Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Mtume Paulo
alisema maneno muhimu yafuatayo:
" Kwa maana siionei haya Injili; kwa
sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza,
na kwa Myunani pia. Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka
imani hata imani; kama ilivyoandikwa , MWENYE HAKI ATAISHI KWA IMANI"
(Warumi 1:16-17).
Huu ndio mpango wa Mungu kwa watu wote
wanoipokea Injili ya Kristo na kuokolewa. Katikati ya dhuluma,wizi, uasherati
na maovu mbalimbali yanayoambatana na hali ngumu ya uchumi iliyopo sasa na ile
itakayotokea miaka si mingi iliyo mbele yetu kuanzia sasa – Mungu anawataka
watu waishi kwa kufuata mpango wake – WAISHI KWA IMANI.
Kuishi kwa Imani ndiyo utaratibu wa uchumi wa
mbinguni ambao kila mkristo anatakiwa kuufuata akitaka kuishi maisha ya
mafanikio na matakatifu katikati ya hali ngumu ya uchumi – badala ya kujikuta
amewezwa na masumbufu ya maisha haya.
Inasikitisha kuona kuwa wakristo wengi
wameyatafsiri na kuyatumia vibaya maneno haya "kuishi kwa Imani". Na
kwa ajili hiyo mpango wa Mungu uliomo ndani ya maneno haya haujaeleweka na
wengi.
Wakristo wengine wanafikiri kuishi kwa imani
ni kuacha kazi wanazozifanya na kuanza kuishi maisha ya omba omba na ya
kubahatisha. Wamesahau kuwa biblia inasema mtu asipofanya kazi asile – soma
2Wathesalonike 3:6 – 12.
Ingawa kuna wakristo ambao wamelifanya neno
hili "kuishi kwa Imani" lisieleweke vizuri; hali hii haiwezi wala
haitaweza kubadilisha mpango wa Mungu uliomo ndani yake.
Mawazo yetu siyo mawazo ya Mungu; njia zetu
si njia za Mungu; na mipango yetu si mipango ya Mungu. Hakuna njia ya mkato kwa
mkristo safi ya kufanikiwa katika maisha, isipokuwa ni kwa kuishi
ndani ya mpango wa Mungu uliofunuliwa katika Kristo Yesu.
"Mwenye haki ataishi kwa imani" maana
yake nini? "Mwenye haki" maana yake Mkristo, au Mtakatifu,
au Mwongofu, au Mteule, au Aliyeokoka. Kwa hiyo tunaweza kusema Mkristo ataishi
kwa imani.
Pia tunasoma katika Waebrania 11:1 ya kuwa:"Basi
imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo
yasiyoonekana"
Tena imeandikwa katika Warumi 10:17 ya kuwa;"Basi
imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo".
Tena imeandikwa katika Yakobo 2:26 ya kuwa;"Maana
kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo
imekufa".
Kwa mistari hiyo michache na mingine mingi
iliyomo katika Biblia inatusaidia kujua ya kuwa "Mwenye haki ataishi
kwa imani" maana yake kila mkristo anatakiwa kuishi kwa kuwa mtendaji
wa Neno la Kristo na siyo msikiaji tu – kila wakati na katika kila eneo la
maisha yake.
Roho Mtakatifu alipokuwa anatufundisha haya
mimi na mke wangu, tulijua hakika ya kuwa tunatakiwa kutumia muda mwingi
kulisoma na kulitafakari Neno la Kristo, ili tuweze kulitenda Neno hilo katika
maisha haya. Tulianza kusoma Neno la Mungu na vitabu mbalimbali vilivyoandikwa
na watumishi wa Mungu na bado tunaendelea kufanya hivi hata leo, na tumeona
mabadiliko makubwa katika maisha yetu – maana mahangaiko tuliyokuwa nayo
yametoweka kwa jina la Yesu Kristo! Sasa tunaishi katika maisha ya ushindi na
amani ndani yake Kristo.
Tatizo ambalo mtu analipata anapookoka, ni
namna ya kuishi katika maisha mapya ya wokovu (2Wakorintho 5:17)
Biblia inatuambia ya kuwa sisi ni raia wa
nyumbani mwake Mungu (Waefeso 2:19). Pia inatuambia kuwa sisi si wa ulimwengu
huu (Yohana 17:14). Kwa hiyo maisha yetu hayatakiwi kuongozwa na utaratibu wa
hapa duniani.
Kuna tofauti kati ya utaratibu wa uchumi wa
duniani na utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni. Ingawa sisi tulio wake
Kristo tumo humu ulimwenguni hatutakiwi kuishi kwa kutegemea utaratibu wa
uchumi wa dunia hii unaoyumba, bali tutegemee utaratibu wa uchumi wa ufalme wa
mbinguni – usioyumba wala kubadilikabadilika kwa kuwa umejengwa juu ya mwamba
imara – Neno la Kristo.
Wakristo wengi kwa kutokujua hili wamejikuta
wakipata shida ya kutaka kuwatumikia mabwana wawili – yaani Mungu na Mali
ambapo Yesu Kristo alikwishasema haiwezekani. Matokeo yake ni kupoteza ushuhuda
wa kikristo na kuishi maisha ya mahangaiko.
Kutegemea utaratibu wa uchumi wa dunia hii
kuna shida sana kwa kuwa uchumi huo ukiyumba kidogo, na wewe unayumba
kimaisha. Lakini ukiutegemea utaratibu wa uchumi wa ufalme wa mbinguni huwezi
kuyumba wakati uchumi wa dunia ukiyumba – kwa kuwa tumaini lako halimo mikononi
mwa dunia na wanadamu – bali ndani ya Kristo Yesu ambaye ni mwamba imara
usiotikisika.
Katika sura zifuatazo nitaelezea mambo mbali
mbali muhimu yaliyomo katika utaratibu au mfumo wa uchumi wa ufalme wa
mbinguni. Kwa hiyo usiache kusoma mfululizo wa somo hili katika sura
zinazofuata baada ya kila wiki.
TOFAUTI YA ZAKA NA DHABIHU
Kutokutoa zaka na dhabihu ni
kumwibia Mungu. Mtu aliye mkristo asipotoa zaka na dhabihu anaitwa mwizi. Kuna
wakristo ambao ni wezi lakini wao hawajui yakuwa ni wezi. Wamemwibia Mungu zaka
na dhabihu. Mungu anasema hivi:
“Je! mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi
mwasema, tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia ZAKA na DHABIHU” (Malaki
3:8)
Kati ya amri tulizopewa na Mungu ni kwamba tusiibe. Kuiba ni dhambi. Na dhambi
ina adhabu yake. Popote palipo na dhambi, laana hutokeza. Kwa wale wanaomwibia
Mungu kwa kutokutoa zaka na dhabihu, wamefunikwa na laana. Ndiyo maana Mungu
alisema hivi:
“…..
Mmeniibia Zaka na Dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana
mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote (Malaki 3:8b, 9).
Laana maana yake ni kutokufanikiwa, kutofaulu, kutokustawi, kukosa furaha,
kukosa amani, na kukosa mwelekeo sahihi. Ni wazi kuwa wakristo wengi hawana
furaha, hawana amani na hawafanikiwi katika maisha yao ya kila siku,
kwa sababu hawamtolei Mungu zaka na dhabihu.
Unapokosa kumtolea Mungu ili ujenzi wa nyumba yake – kanisa uendelee, Hagai 1:6
anatuambia Mungu anasema hivi;
“Mmepanda
mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini
hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye
apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka”.
Zaka ni kitu gani?
Zaka ni fungu la kumi la pato lako. Hebu isome na kuitafakari mistari
ifuatayo;
“Tena
zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya
Bwana, ni takatifu kwa Bwana ….Tena zaka yote ya ng’ombe, au ya kondoo, kila
apitaye chini ya fimbo; SEHEMU YA KUMI watakuwa ni watakatifu kwa Bwana” (Mambo
ya Walawi 27:30 –32).
“…Toa
fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako;
na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na
mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na
kushiba; ili kwamba Bwana, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya
mkono wako uifanyayo”(Kumbukumbu la Torati 14:28-29).
Zaka ni fungu la kumi la pato toka mshahara wako ofisini, shambani au kwenye
mifugo. Tena zaka hii ni ya Bwana na ni Takatifu.
Mtu asipoitoa zaka hii anamwibia
Mungu. Zaka si yako hustahili kukaa nayo wala kuitumia nje ya utaratibu wa
Mungu.
Lakini Malaki 3:10a anasema; “Leteni
zaka KAMILI ….” Maana yake nini maneno haya? Maana yake ni hii; ikiwa kwa
mfano mshahara wako kwa mwezi ni shilingi 2,000/= ( kabla ya makato) – fungu la
kumi au zaka unayotakiwa kutoa ni shilingi 200/= ambayo ndiyo zaka kamili ya
mshahara wako. Ukileta pungufu yake hiyo si zaka kamili.
Tena
kwa mfano umevuna magunia 10 ya mahindi toka shambani mwako – zaka kamili
unayotakiwa kutoa ni gunia moja bila kupungua. Kumbuka mzaliwa wa kwanza wa
mifugo yako ni wa Bwana.
Unaweza
ukasema habari za kutoa zaka ni za agano la kale na siyo za agano jipya.
Waebrania 7:5-10 inatuambia wazi ya kuwa Ibrahimu alitoa fungu la kumi. Kama
Ibrahimu alitoa sehemu ya kumi, Je! si zaidi sana kwetu sisi tulio
uzao wake kwa imani ndani yake Kristo? Maana imeandikwa hivi;
“Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu na warithi sawasawa
na ahadi” (Wagalitia 3:29). Soma pia Wagalitia 3:13,14).
Dhabihu ni kitu gani?
Dhabihu ni matoleo yanayotolewa baada ya kutoa sehemu ya kumi ya pato lako. Kwa
mfano, kama mshahara wako kwa mwezi ni shilingi 2,000/=, basi sehemu
ya kumi (zaka) ni shilingi 200/=. Kiasi cho chote utakachotoa ju ya shilingi
200/= ndiyo matoleo yako. Kwa mfano ukitoa shilingi 210/= toka kwenye mshahara
wako wa shilingi 2000/=, Basi, shilingi 200/= ni zaka; na shilingi 10/= ni
dhabihu au matoleo au sadaka ya kawaida.
Kiasi utakachotoa katika dhabihu/matoleo, ndicho kitakachokuwa kipimo
kitakachoweka kiwango chako cha kupokea. Imeandikwa hivi:
“Lakini
nasema neno hili, APANDAYE HABA ATAVUNA HABA; APANDAYE KWA UKARIMU ATAVUNA KWA
UKARIMU. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni,
wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na
Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, MKIWA NA RIZIKI ZA
KILA NAMNASIKUZOTE,mpatekuzidisanakatikakilatendojema;kamailivyoandikwa,
Ametapanya, amewapa maskini, haki yake yakaa milele. Na yeye ampaye mbegu
mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha,
naye ATAYAONGEZA MAZAO YA HAKI YENU, MKITAJIRISHWA KATIKA VITU VYOTE MPATE KUWA
NA UKARIMU WOTE; umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu. Maana utumishi wa
huduma hii HAUWATIMIZII WATAKATIFU RIZIKI WALIZOPUNGUKIWA TU, Bali huzidi sana
kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu; kwa kuwa mkijaribiwa kwa
utumishi huo, WANAMTUKUZA MUNGU kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya
Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote” (2Wakorintho
9:6-13)
Soma tena mistari hiyo hapo juu, lakini sasa tafakari zaidi maneno
niliyoyaandika kwa herufi kubwa. Utaona kuwa usipokuwa mwaminifu katika utoaji,
wewe mwenyewe unakosa kufanikiwa, na pia unamkosesha Mungu shukrani na utukufu
ambao angepata kwa utoaji wako.
Zaka na dhabihu zitolewe wapi?
Hili jambo linahitaji uongozi wa Roho Mtakatifu, ili upate ufahamu Mungu
anataka upeleke wapi zaka na matoleo uliyo nayo.
Hili ni muhimu kwa kuwa
Biblia inazungumza juu ya kupeleka kanisani (Malaki 3:10-11), kwa watakatifu
(2Wakorintho 9:12), kwa maskini (2Wakorintho 9:8-9), kwa watumishi wa Mungu
(1Wafalme 17:10-24; 1Wakorintho 9:7-14); kwa wajane, - na kadhalika.
Muombe Mungu akuongoze mahali pa kupeleka. Amani ya
Kristo na iamue moyoni mwako.
Baraka Tele!
Kuna baraka tele za mafanikio kwa mkristo aliye mwaminifu katika kumtolea Mungu
zaka na matoleo.
Katika Malaki 3:10 imeandikwa hivi; “Leteni zaka kamili ghalani, ili
kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo (YA UTOAJI) asema
Bwana wa Majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na
KUWAMWAGIENI BARAKA, HATA ISIWEPO NAFASI YA KUTOSHA AU LA”.
Je! umewahi kukutana na mkristo ambaye anashuhudia kuwa Mungu amempa
baraka nyingi hata HANA MAHALI PA KUZIWEKA? Ni wazi kuwa ahadi hii haijatimia
kwa kuwa hatujawa watendaji na Neno kikamilifu katika utoaji.
Soma mistari hii hapa chini uone baraka zingine zinazotokana na utoaji; “Azaria
Kuhani Mkuu, wa nyumba ya Sadoki, akamjibu, akasema, Tangu watu walipoanza
kuleta matoleo nyumbani kwa Bwana, tumekula na KUSHIBA NA KUSAZA TELE; kwa
kuwa Bwana amewabariki watu wake; na kilichosalia ndiyo akiba hii kubwa.
Ndiko Hezekia akaamuru kutengeneza vyumba nyumbani mwa Bwana; wakavitengeneza.
Wakayaingiza MATOLEO na ZAKA na vitu vilivyowekwa wakfu, kwa uaminifu ….” (2Mambo
ya Nyakati 31:10-12).
Kwa nini wakristo wengine wanapungukiwa vyakula, wakati tuna nafasi ya
kumruhusu Mungu kutubariki kwa vyakula tele? Mpe Mungu nafasi ya kukubariki kwa
kumtolea zaka na matoleo!
Anza Sasa!
Nakushauri ya kuwa kama ulikuwa hutoi sehemu ya kumi au zaka pamoja
na matoleo ya kutosha – anza sasa.
Jambo la kwanza, kumbuka kutubu kwa Mungu katika Jina la Yesu Kristo kwa kuwa
ulimwibia zaka na dhabihu kwa kutokumtolea.
Halafu mwombe Mungu akuwezeshe kusimama katika uaminifu wa kumtolea zaka na
dhabihu ili apate nafasi ya kukubariki zaidi kama tulivyoona,
na kama alivyoahidi.
UKITOA TEGEMEA KUPOKEA
Sehemu nyingi nilizotembelea nimeona na kufahamu ya kuwa watu wengi
wanatoa sadaka – fedha taslimu au vitu au wanyama kwa Mungu BILA KUTEGEMEA
KUPOKEA KUTOKA KWA MUNGU.
Furaha ya utoaji inatokana na kufahamu matokeo ya utoaji huu. Ndiyo maana
mkristo yuko tayari kuweka shilingi 10,000/= katika mradi utakaompa faida
kuliko kutoa kanisani ambako anafikiri sadaka hiyo haina faida kwake binafsi.
Kwa hiyo siku zote atatoa sadaka kidogo kanisani au kwenye kazi ya Mungu.
Bila ya mkristo kujua kwamba anajua na kuwa na uhakika moyoni mwake kuwa akitoa
sadaka anastahili kupokea ZAIDI YA KIWANGO ALICHOTOA KUTOKA KWA MUNGU –
utoaji wake utakuwa chini siku zote.
Wakristo wengi wanafikiri wakimtolea Mungu kitu, watazidi kupungukiwa na
kufilisikia. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba ukimtolea Mungu ulicho nacho
UNAFUNGUA MLANGO WA KUFANIKIWA kwa ulivyo navyo. Unapomtolea
Mungu hufilisiki bali unatajirika!
Tunapokuwa ndani ya Kristo, tunachukua na kubeba tabia ya Mungu ndani
yetu. Imeandikwa hivi:
“ Bali wote waliompokea(Kristo) aliwapa UWEZO
wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake” (Yohana 1:12) “
Kwa kuwa UWEZA wake wa UUNGU umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa,
kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe” (1Petro
1:13)
Ni
vizuri ufahamu ya kuwa mojawapo ya tabia ya Uungu tuliyo nayo ndani yetu katika
Kristo ni tabia ya kutoa HUKU UKITEGEMEA KUPOKEA. Mungu akitoa kitu anategemea
kupokea.
Tabia ya Mungu ya Utoaji
Mungu
alipokuwa anamtoa mwana wake wa pekee, alimtoa huku akitegemea kupata watoto
wengi wa kiroho. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanae
pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohana
3:16)
Mungu
alipokuwa anamtuma Roho Mtakatifu juu ya wanafunzi wake, alimtoa huku
akitegemea kupata mashahidi wengi watakaosimama upande wake na kulitetea jina lake hapa duniani.
“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi
mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalem, na katika Uyahudi wote, na Samaria,
na hata mwisho wa nchi” (Matendo ya Mtume 1:8)
Mungu
anapotoa utajiri kwa watu wake, anautoa huku akitegemea kupata agano lililo
imara kati yake na wanadamu. “ Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye
akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba
zako,kama hivi leo” (Kumbukumbu la Torati 8:18).
Hii ndiyo
tabia tuliyo nayo ndani ya Kristo, kutoa huku tukitegemea kupokea. Hili jambo
la kutoa na kupokea wakati mwingine linajulikana kama KUPANDA na
KUVUNA.
Hakuna
mkulima anayepanda mbegu shambani bila kutegemea kuvuna. Kama hana tegemeo la
kuvuna, basi hata haja na hamu ya kupanda inapotea – inakuwa haina maana
kupanda maana hatapata kitu.
Katika mambo
ya kiroho ni vivyo hivyo. Utakachotoa ndicho utakachopata. Utakachopanda ndicho
utakachovuna. Ukipanda fedha utavuna fedha. Ukipanda upendo utavuna upendo.
Ukipanda ng’ombe utavuna ng’ombe. Ukitoa vitabu utapokea vitabu. Imeandikwa
hivi; “ Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho
mtu, ndicho atakachovuna” (Wagalatia 6:7).
Hivi ndivyo
ilivyo, utakachopanda ndicho utakachovuna. Kwa maneno mengine, ni kwamba
ukipanda tegemea kuvuna.
Tumia tabia ya Mungu iliyo ndani yako
Ikiwa
wewe unakaa ndani ya Kristo na Kristo anakaa ndani yako, basi uwe na uhakika ya
kuwa tabia ya Uungu ya kutoa na kupokea, kupanda na kuvuna imo ndani yako.
Inaonekana
wazi ya kuwa wakristo wa kanisa la Korintho na Filipi katika nyakati za huduma
ya Mtume Paulo – walishiriki sana katika habari hii ya kutoa na
kupokea. Siyo kutoa bila kupokea bali kutoa na kupokea. Hii ni tabia
iliyoonekana wazi katika ukristo wao. Hebu soma maneno yafuatayo juu ya habari
hii katika kitabu cha Wafilipi katika nyakati za huduma ya Mtume Paulo –
walishiriki sana katika habari hii ya kutoa na kupokea. Siyo kutoa bila
kupokea bali kutoa na kupokea. Hii ni tabia iliyoonekana wazi katika ukristo
wao. Hebu soma maneno yafuatayo juu ya habari hii katika kitabu cha Wafilipi
4:10-14;
“
Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikra
zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa
mkinifikiri hali yangu; lakini mkupata nafasi. Si kwamba nasema haya kwa
kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote
niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na
katika mambo yo yote, nimefudishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na
kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. LAKINI MLIFANYA
VEMA, mliposhiriki nami katika dhiki yangu”.
Mtume
Paulo hapa anawaambia Wafilipi wazi kuwa maisha yake yote na katika mambo yote
na katika hali yo yote tumaini lake na ushindi wake ni katika UWEZA WA KRISTO
amtiaye nguvu – na wala si katika uweza wake Paulo au huruma za wanadamu. Hata
hivyo aliwaambia “MLIFANYA VEMA MLIPOSHIRIKI NAMI KATIKA DHIKI YANGU”. Katika
maneno yanayofuata aneleza kwa nini walifanya vema kumhudumia katika dhiki
yake.
“Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika
mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine
lililoshirikiana nami katika habari hii ya
KUTOA
NA KUPOKEA, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike
mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja. Si kwamba
nakitamani kile kipawa, bali NAYATAMANI MAZAO YANAYOZIDI KUWA MENGI, katika
HESABU YENU” (Wafilipi 4:15 – 17).
Ni
wazi kabisa ya kuwa kwa sababu ya kushiriki katika habari ya KUTOA NA KUPOKEA –
Wafilipi hawakufilisika wala kupungukiwa bali MAZAO YALIZIDI KUWA MENGI KATIKA HESABU YAO.
Huyu Mungu aliyewafanikisha Wafilipi, ndiye atakayekufanikisha wewe na kuongeza
mazao mengi katika habari hii ya KUTOA na KUPOKEA.
Kumbuka siku zote kuishi kwa kuitumia na kutegemea tabia ya Mungu iliyo
ndani yako katika Kristo. Tabia hii itakusaidia kutoa na kutegemea kupokea –
kupanda na kutegemea kuvuna. Imeandikwa hivi
“Wapeni
watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa – sukwa
hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu” (Luka 6:38)
SADAKA NA WOKOVU
“Palikuwa na mtu Kaisaria jina lake Kornelio, akida wa
kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake
yote, naye alikuwa akiwapa watu SADAKA NYINGI, na kumwomba Mungu daima. Akaona
katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu,
akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, kuna
nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na SADAKA ZAKO zimefika juu na kuwa
ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye
Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa
ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani; ATAKUAMBIA YAKUPASAYO KUTENDA” (Matendo
ya Mitume 10:1 – 6).
Tabia hii ya Kornelio ya kuwa mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake
yote, na pia tabia ya utoaji wa sadaka na kumwomba Mungu daima, inaonyesha wazi
kuwa Kornelio alimpenda Mungu sana na alikuwa anatafuta namna
yakukubalika mbele zake na namna ya kumpendeza Yeye.
Tungezungumza kwa lugha nyepesi zaidi, ni kwamba alitaka kwa MATENDO YAKE aende
mbinguni na kuurithi Uzima wa Milele baada ya kufa kwake . Kwa kifupi
alimtafuta Mungu kwa njia ya Matendo.
Hii ina maana ya kuwa Kornelio alitaka kuvuna baraka za Agano Jipya
katika damu Yesu, wa kutumia njia za kupendeza Mungu zilizomo katika Agano la
Kale.
Tena ingawa yeye hakuwa Myahudi kwa kuzaliwa, alitaka sana kuvuna
baraka ambazo Mungu aliahidi juu ya Wayahudi.
Mpaka hivi leo kuna watu wengi wanataka kuvuna baraka toka kwa Mungu bila
kutumia utaratibu aliouweka Mungu wa kuzipokea. Ni vigumu sana kupokea
ahadi za Mungu nje ya mpango wake.
Huwezi kupokea ahadi za agano la kale kwa kutumia mbini za agano la kale na
huku sasa hivi tumo katika kipindi cha agano jipya.
Baraka zote zilizomo katika agano la kale aliahidiwa Ibrahimu na uzao wake
MILELE. Soma mwenyewe Mwanzo sura ya 17 na 22. Kwa hiyo ukitaka kupokea baraka
za agano la kale lililofungwa kati ya Mungu na Ibrahimu, inabidi uwe mzao au
mtoto wa Ibrahim. - Kornelio hakufahamu hili; hata leo hii wengi hawafahamu.
Baraka zote zilizomo katika agano jipya zimeahidiwa wale walio ndani ya Kristo
– waliotoa maisha yao kwa Yesu kama vile Yesu Kristo alivyotoa maisha
yake kwa ajili yao.
Ni vigumu kupokea baraka za ahadi za agano la kale na zile za agano jipya NJE
YA YESU KRISTO. Imeandikwa hivi katika Wagalatia 3:13,14,29;
“Kristo alitukomboa katika laana ya torati,
kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, baraka ya Ibrahimu
IWAFIKILIE MATAIFA KATIKA YESU KRISTO, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya
imani…… Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na
warithi sawasawa na ahadi. "
Ndiyo maana Mungu alimtuma Malaika
wake ili amwambie Kornelio kuwa amwite Simon Petro ili awaeleze habari za Yesu
Kristo – ili baraka ya Ibrahimu iwafikie na wapate kupokea ahadi ya Roho kwa
njia ya imani – SIYO KWA MATENDO PEKE YAKE.
Jambo ambalo
Mungu alitaka Kornelio ajue na sisi pia tujue ni kuwa matendo mema, maombi na
SADAKA bila “kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani” yaani kuzaliwa
mara ya pili kwa Roho au kuokoka – haitoshi kumpendeza Mungu, wala
kukubalika mbele zake au kuhesabiwa haki.
Ndiyo maana
Yesu Kristo alimwambia Nikodemo, yule Farisayo kuwa “Mtu asipozaliwa mara
ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu ….. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia,
HAMNA BUDI kuzaliwa mara ya pili”(Yohana 3:3,7).
Haya maneno “Hamna Budi” maana yake ni “lazima” kwa hiyo
Yesu Kristo alikuwa anasema “…… LAZIMA kuzaliwa mara ya pili”.
Yesu Kristo alikuwa anasisitiza kwa Nikodemo, na hata kwetu sote tunaotaka
kuurithi ufalme wa Mungu, kuwa hakuna njia nyingine isipokuwa LAZIMA kuzaliwa
mara ya pili kwa Roho (au kwa maneno mengine) LAZIMA Kuokoka!
IMANI NA MATENDO
Matendo peke yake hayatoshi kukupa
ufalme wa Mungu. Kuna watu wengi sana ambao ni
waaminifu sana katika kusali na kumtolea Mungu sadaka, lakini
hawakubaliani na jambo kuokoka. Wanaona kuwa wao tayari wameokoka kwa sababu tu
wanasali, wanatoa sadaka na kujitahidi kuishi katika matendo mema. Hebu
soma maneno ya mistari hii uone yanavyopingana na msimamo huu;
“Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya
imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; WALA SI KWA
MATENDO, mtu awaye yote asije akajisifu” (Waefeso 2:8,9)
Tunaokoka kwa njia ya imani itendayo kazi katika Yesu Kristo, “Wala si kwa
matendo, mtu awaye yote asije akajisifu”. Matendo yana faida zaidi kwa mtu
baada ya kuokoka. Na pia imani bila matendo, imani hiyo imekufa nafsini mwake.
Biblia inasema hivi:
“Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana
matendo? Je! ile imani yaweza kumwokoa?…. Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina
matendo, imekufa nafsini mwake. Lakini mtu atasema, wewe unayo imani, nami
ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha IMANI
YANGU KWA NJIA YA MATENDO YANGU …….. Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa,
vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa” (Yakobo 2:14,17,18,26).
Jambo ambalo Yakobo alikuwa
anasisitiza hapa ni kutaka kuwaonya watu kuwa kusema wewe ni mkristo na huku
matendo yako hayalingani na ushuhuda wa mdomo wako ni bure. Wokovu uonekane
katika maisha yetu kila siku – la sivyo imani tuliyo nayo inakosa kuzaa matunda
ya uzima wa milele. Ndiyo maana Yesu Kristo aliwahi kuzungumza juu ya kukatwa
kwa tawi (Mkristo) lisilo zaa, soma Yohana 15:1-8 ili upate picha zaidi juu ya
jambo hili.
CHUKUA HATUA LEO
Malaika alimwambia Kornelio atume watu wakamwite Simoni aitwaye Petro ili
AMWAMBIE YAMPASAYO KUTENDA. Mungu kwa uweza wa Roho wake Mtakatifu amekuletea
maneno haya mkononi mwako ili UFAHAMU YAKUPASAYO KUTENDA.
Kama hujaokoka
na unadhani unaweza kuokoka kwa kutoa sadaka nyingi NAKUSHAURI KWA JINA LA YESU
KRISTO WA NAZARETI uombe sala hii kwa sauti, ili utubu na kumpa Yesu Kristo
maisha yako leo. HALAFU endelea kutoa sadaka nyingi ukiwa ndani ya Yesu Kristo.
Omba sala hii kwa sauti; “Mungu Baba, unisamehe dhambi zangu zote
nilizokukosea katika maisha yangu. Ninatubu kwako. Nitakase kwa damu ya Yesu
Kristo. Bwana Yesu Kristo nimefungua moyo wangu nakukaribisha uingie ndani
yangu, kwa uwezo wa Roho wako. Uwe Bwana na Mwokozi wa maisha yangu – sasa na
hata milele. Asante kwa kunisamehe dhambi na kuniokoa. Amina”.
Ikiwa umeisema sala hii kwa uaminifu, basi umefanyika kiumbe kipya – umezaliwa
mara ya pili na Mungu hakumbuki dhambi zako tena. Soma 2Wakorintho 5:17,
Waebrania 8:12. Karibu sana katika ufalme wa Mungu kwa jina la Yesu
Kristo!
Hili ndilo lililotokea kwa Kornelio na jamaa yake, Simoni Petro alipofika kwao
aliwaambia habari za Yesu Kristo – walisikia maneno hayo wakamwamini Yesu na
kujazwa na nguvu za Roho Mtakatifu wakati huo huo.
NATOA LAKINI SIPOKEI – NIFANYEJE?
Kuna
wakati fulani, mtu mmoja alinifuata baada ya kipindi nilichokuwa nafundisha
Neno la Mungu juu ya utoaji, na akaniuliza hivi; “Kwa nini mimi nimekuwa natoa zaka
na sadaka nyingi lakini sipokei? Hata miradi niliyo nayo haifanikiwi
nilivyokusudia – ni kwa nini iwe hivyo.
Inawezekana na wewe unayesoma ujumbe huu sasa una maswali kama haya.
Hayo ni maswali ya msingi na ni muhimu tupate ufumbuzi wake. Hata mkulima
ambaye alipanda mbegu katika shamba, na asipate kitu au apate mavuno machache,
atajiuliza maswali kumetokea kitu gani.
Tukumbuke ya kuwa si mapenzi ya Mungu tuwe maskini – tuwe na hali ngumu
kimavazi, chakula na kiafya. Pia, tukumbuke ya kuwa ni tabia ya kiuungu mtu
kutoa na kutegemea kupokea. Ingawa si lazima upate toka kwa mtu huyo huyo
uliyempa, - maana Mungu anaweza kumgusa mtu mwingine akupe – lakini utaratibu
wa Mungu unabaki pale pale, ukitoa tegemea kupokea.
Ni kitu gani kinasababisha mtu asipokee na huku amekuwa akijitahidi kutoa?
Biblia inatuambia ya kuwa tukiwa waaminifu katika utoaji, Mungu atatumwagia
baraka, “hata isiwepo nafasi ya kutosha ya kuziweka” – Je! umewahi kumsikia
mkristo yo yote akisema amepata baraka nyingi mno hata amekosa mahali pa
kuziweka?
Sababu zifuatazo zitatusaidia kujua ni kwa
nini hatufanikiwi katika utoaji wetu – na hata
hatupokei kama tulivyotegemea na kutarajia;
1. KUVUNJA MIIKO AU UTARATIBU WA UTOAJI
Kila jambo
lina utaratibu wake – usipoufuata usitegemee mavuno mazuri. Kilimo cha mahindi
kina utaratibu wake wa upandaji na palizi tofauti na kilimo cha ngano au cha
kabichi. Ndiyo maana wataalamu wa kilimo, walianzisha kampeni za kuwafundisha
wakulima juu ya “kilimo cha kisasa” ili kiwasaidie wakulima kupata “mavuno”
zaidi toka katika mashamba yao.
Hata katika “kupanda na kuvuna” au “kutoa na kupokea” katika mambo ya Mungu
kuna utaratibu wake. Ukienda kinyume na utaratibu huo, usitegemee mavuno ya
kuridhisha toka katika utoaji wako
Kwa mfano hebu soma na kutafakari maneno haya
yafuatayo:
“Lakini
nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa
ukarimu. Kila mtu na atende kama ilivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni,
wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa
ukunjufu” (2Wakorintho 9:6,7).
“….wala si kama kitu kitolewacho
kwa unyimivu” (2Wakorintho 9:5).
Utaona katika mistari hiyo Mungu ametueleza kwa kiasi fulani utaratibu ambao
anataka ufuatwe mtu akitaka kuvuna katika utoaji wake. Je! unafuata utaratibu
huu katika utoaji wako?
Utaratibu
huoni huu; utoaji wako uwe si haba (au kidogo) bali uwe kwa ukarimu. Ukitoa
kidogoutapata kidogo – bali ukitoa vingi utapata vingi. Ndiyo maanaimeandikwa;
“Wapeni
watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa
hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. KWA KUWA KIPIMO KILE
KILE MPIMACHO NDICHO MTAKACHOPIMIWA” (Luka 6:38)
Kama unataka kutoa sadaka tu “ kama ulivyokusudia moyoni
mwako”. Kama ulikusudia kutoa shilingi 100/= toa shilingi 100/=.
Fanya hivi siku zote na utafanikiwa.
Tena,
utoajiunatakiwa ufanyike “si kwa huzuni; wala si kwa lazima; maana Mungu
humpenda yeyeatoaye kwa moyo wa ukunjufu “… na walasi kwa unyimivu”.
Michango mingi iliyomo makanisani siku hizi wakati mwingine inafanyika kwa
kulazimishana.Mtu anatakiwa atoe kwa kupenda kwake toka moyoni mwake – SI KWA
LAZIMA.Kumlazimisha mtu kutoa ni kwenda kinyume cha utaratibu wa utoaji.
Wakristo
wengiwamekosa baraka au mafanikio katika utoaji kwa sababu wanatoa huku
WANAHUZUNIKAAU WANALALAMIKA! Wengi wanawanung’unikiaviongozi wa
makanisa yao kuwa wanatumiafedha au vitu vibaya. Kama una
wasiwasi na matumizi ya matoleo yako – yaombeekwa Mungu ayalinde yatumike kwa
utukufu wake kuliko kulalamika.
Wengine
wanahuzunika na kulalamika kuwa michango imezidi. Je! umewahi kumsikia mkulima
akihuzunika au kulalamika kwa kuwa ameongezewa shamba la kulima na kupanda?
Hakuna. Mkulima halalamiki bali anafurahi kwa kuwa amepata eneo kubwa zaidi la
kupanda umeongezewa eneo la KUPANDA ili AVUNE ZAIDI. Ni eneo la kukusaidia
kutoa zaidi ili UPOKEE ZAIDI!
2. IBILISI AMEZUIA BARAKA ZAKO;
Kati ya baraka
ambazo zinapatikana kutokana na mtu kuwa mwaminifu katika utoaji wa zaka (fungu
la kumi) na dhabihu (matoleo mbalimbali) na kuzidiwa wakati wa matatizo, Mungu
alisema hivi;
“Nami kwa ajili yenu
nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu
wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba ….” (Malaki
3:11).
Ni wazi kuwa
aliye nyuma ya kuharibika kwa mazao shambani au biashara ni yule ‘alaye’ ambaye
ni Ibilisi. (Hii ni kama mkulima au mfanya biashara amefanya anachotakiwa
kukifanya kilicho ndani ya uwezo wake).
Kinyume cha jambo hili ni kwamba usipokuwa mwaminifu kutoa fungu la kumi toka
katika mazao ya shamba lako, usitegemee Mungu akupiganie wakati mharibu
anapoingilia mimea yako na kuiharibu. Vile vile usipokuwa mwaminifu kutoa fungu
la kumi toka katika mapato ya biashara yako, usitegemee Mungu akusaidie wakati
mharibu anapoingilia biashara yako na kuiharibu.
Inawezekana unatoa sadaka, na huoni baraka zozote zinazotokana na kutoa kwako –
hebu angalia na jichunguze kama umekuwa mwaminifu katika kutoa ZAKA KAMILI.
Kwa mfano kama fungu la kumi la pato lako ni shilingi 2,000 – toa zaka kamili
yaani shilingi 200/=. Usitoe pungufu ya hiyo maana haitakuwa zaka KAMILI.
Ikiwa umekuwa mwaminifu katika kutoa Zaka kamili na dhabihu halafu
huoni matokeo yake basi, tumia mamlaka ya Jina la Yesu Kristo – mfunge na
kumkemea ibilisi ambaye ndiye mharibu wa mali yako aondoe mikono yake juu ya
mali yako.
Kumbuka Yesu Kristo alisema;
“Nami
nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalofunga duniani,
litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa
limefunguliwa mbinguni” (Mathayo 16:19).
Kuna mtumishi mmoja wa
Mungu ambaye anasimulia jinsi ambavyo mkulima mmoja wa pamba alivyosaidika na
uwezo wa jina la Yesu Kristo.
Huyo Mkulima alikuwa
mwaminifu katika kumtolea Mungu fungu la kumi la mapato ya shamba lake kila
mwaka, na alikuwa haelewi kwa nini pamba yake ilikuwa haifunguki ingawa muda wa
kufunguka na kuchanua ulikuwa umefika. Wataalamu wa kilimo cha pamba walikuja
kuliangalia shamba hilo lakini hawakuweza kumsaidia mkulima huyo kutatua tatizo
hilo.
Mtumishi wa Mungu huyo
alifika hapo, na alisikia habari ya mahangaiko ya mkulima huyo. Baada ya
kufahamu ya kuwa mkulima huyo alikuwa mwaminifu katika kutoa fungu la kumi –
alimwambia waende shambani ili waombe.
Huyo mtumishi wa Mungu
wakiwa shambani na mkulima huyo; - akimkumbusha Mungu juu ya ahadi yake ya
Malaki 3:7-11. Na mwishoni akamwamuru ibilisi aondoke kwenye pamba hiyo. Mara
tu baada ya kumaliza sala hiyo – pamba ilianza kufunguka na kuchanua! Bwana
asifiwe sana kwa uwezo huu ulivyo wa ajabu.
Usibaki unalalamika na kuhangaika kama vile mtu asiyejua ahadi za Mungu.
Simamia haki zako ndani ya Kristo kwa kuwa mtendaji wa neno na utafanikiwa.
3. KUTOKUPANDA KATIKA UDONGO MZURI
Utoaji ni sawasawa
na upandaji. Mtu akipanda anategemea kuvuna pia. Kwa hiyo mtu akitoa anategemea
kupokea.
Mkulima yo yote akitaka
mavuno mazuri toka shambani mwake kati ya vitu anavyoviangalia ni aina ya mbegu
na aina ya udongo. Siku zote atapanda kwenye udongo mzuri wenye rutuba.
Mfanya
biashara siku zote anataka aweke mtaji wake katika vitu vitakavyomletea faida
kibiashara na siyo hasara.
Lakini,
inasikitisha kuona kuwa inapofika wakati wa utoaji – wakristo wanatoa tu bila
kuangalia kwanza “udongo mzuri” ni upi ili utoaji wao uwaletee matokeo mazuri.
Biblia inatuambia katika
mfano wa mpanzi ya kuwa mbegu zingine“…. Zikaanguka penye udongo ulio mzuri,
zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na
moja mia” (Mathayo 4:8).
Je,
“udongo mzuri” unaoleta faida nzuri ni upi? Sehemu za kutoa zenye matokeo au
mavuno mazuri ni hizi zifuatazo;
(a) Katika
nyumba ya Mungu – kanisani ili kuendeleza kazi ya Mungu – soma Malaki 3:10-11;
na Kumbukumbu ya Torati 8:18.
(b) Kuwasaidia
watumishi wa Mungu na watakatifu wake kwa vitu/mali ulizo nazo. Soma 1Wafalme
17:10-24 na 2Wakorintho 9:10-13.
(c) Kuwasaidia
maskini kwa vitu/mali ulizo nazo. Soma 2Wakorintho 9:8-9.
Angalia upandaji wako
katika utoaji – je! umepanda kwenye udongo ulio mzuri?
4. KUKATA TAMAA
Wagalatia 6:9
inasema hivi; “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa
wakati wake, tusipozimia roho”.
Tafsiri iliyo nyepesi inasema, “maana tutavuna kwa wakati wake tusipokata
tamaa”.
Wakristo
wengi wanatoa lakini hawana uvumilivu. Mkulima asipokuwa mvumilivu kusubiri
mazao ya shamba lake yanayokuja kwa wakati wake – hawezi kuvuna
alichopanda.
Vile vile
mtoaji asiyejifunza kumvumilia Mungu ili amletee matokeo ya utoaji huo kwa
WAKATI WAKE – hawezi kuvuna alichopanda.
Mungu si
mwongo! Wala ahadi zake hazijui kusema uongo. Alichoahidi atatenda. Ukitoa
utapokea KWA WAKATI WAKE USIPOKATA TAMAA.
Usianze
kutafuta njia za mkato ili ufanikiwe – uwe mvumilivu ulichopanda kwenye udongo
mzuri utavuna.
Mkumbuke
Ibrahimu alivyovumilia. Biblia inasema hivi;
“Lakini
akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani,
akimtukuza Mungu; huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale
aliyoahidi” (Warumi 4:20-21).
5.KUTOA KWA MAJIVUNO NA KUTAFUTA KUSIFIWA NA
WATU
“Angalieni
msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana
mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.
Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo
katika masinagogi na njiani, ili WATUKUZWE NA WATU. Amin,
nawaambieni,wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata
mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa
siri; na BABA YAKO AONAYE SIRINI ATAKUJAZI” (Mathayo 6:1- 4
UFANYEJE KATIKA HALI NGUMU YA UCHUMI?
Matatizo ya ugumu wa uchumi katika dunia hii
siyo mapya. Tangu baada ya mwanadamu kuanguka katika dhambi – amekuwa mara kwa
mara akisumbuliwa na matatizo ya uchumi. Ukisoma habari za Isaka na za Yakobo
utaona jinsi hali hii ilivyojitokeza.
Lakini biblia inaeleza wazi kuwa siku hizi ni
mwisho. Katika siku hizi za mwisho, biblia pia inasema wazi kabisa kuwa dunia
itapita kwenye vipindi vigumu vya uchumi
Kwa Mfano: Katika Mathayo 24:7 na Ufunuo
wa Yohana 6:3-6 tunaona ya kuwa katika siku hizi za mwisho kutatokea njaa – au
upungufu wa chakula. Sababu ya kuja kwa njaa hiyo ni vita vitakavyokuwa
vinatokea katika nchi mbalimbali. Ni wazi kabisa kuwa palipo na vita au palipo
na ugomvi, panakuwa na matatizo ya ulimaji mashamba na usafiri wa kuleta
chakula toka sehemu zingine. Matokeo ni hilo eneo au nchi kukosa chakula, haya
mambo yaliyotabiriwa kutokea siku hizi za mwisho wa dunia.
Ukisoma katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana
sura za 17 na 18 utaona ya kuwa hali ngumu ya kibiashara imetabiriwa kutokea
katika siku hizi za mwisho. Kuuza au kununua kutafanyika kwa vibali. Watu
watapenda fedha sana kuliko kumpenda Mungu. Kutakuwa na uhusiano mkubwa sana
kati ya utajiri na biashara na uasherati. Wafanya biashara wa siku hizi za
mwisho watakuwa na sehemu kubwa katika utawala wa miji au vijiji wanavyokaa –
hata wakati mwingine katika maongozi ya nchi au mataifa mbalimbali.
Matokeo ya hali namna hii inawafanya watu
watafute njia au mbinu za kuweza kuishi katika vipindi vya namna hiyo. Lakini
ni wazi kuwa si mbinu zote au njia zote ambazo wanadamu wanazitumia katika
kuishi wakati wa hali ngumu ya uchumi zinampendeza Mungu.
Kunapotokea hali ngumu ya uchumi, tabia za
watu zinabadilika. Mara kwa mara mambo yafuatayo hutokea;
Kubana matumizi Kununua vitu kwa wingi na
kuvirundika Uchoyo – kupunguza tabia ya utoaji na ukarimu Watu huacha
kumtumikia Mungu na badala yake mtu huitumikia mali Rushwa, wizi na dhuluma
huwa ni vitu vya kawaida Miradi ya kila namna huibuka kuanzia kwa watoto hadi
watu wazima.
Jambo linalowafanya watu wawe na tabia hizi,
ni lile la kutaka kutafuta namna ya kuishi katika kipindi kigumu cha uchumi.
Je!mkristo afanye nini ili aishi katika kipindi hiki kigumu cha uchumi bila
kufanya mambo yatakayomkosea Mungu?
Wakristo wengine wamefika mahali pa
kuhalalisha miradi ya kuwapatia fedha ambayo ni kinyume na ushuhuda wa kikristo
– Je! hii ni sawa?
Wengine wamefika hata mahali pa kufunga nira
na wasioamini (wasio wakristo) KWA JINSI ISIYO SAWASAWA (yaani isiyokubalika)
na neno la Mungu ili waweze kupata fedha kutokana na mradi wanaofanya pamoja.
IKO "jinsi iliyo sawasawa" na utaifahamu ikiwa utakuwa mtendaji wa
neno la Mungu.
Wakristo si wa ulimwengu huu
Ndugu au Dada unayesoma sasa mambo haya –
sikiliza! Sisi kama wakristo si wa ulimwengu huu ingawa tunaishi hapa
ulimwenguni. Fahamu na kumbuka hili kila wakati. Yesu Kristo alisema hivi;
"Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu
umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi
siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa
ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako
ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo
naliwatuma hao ulimwenguni" (Yohana 17:14-18).
Je! unafikiri Yesu Kristo anaweza kututuma
hapa duniani bila kutuandaa kuishi kiushindi katika majaribu yaliyomo ndani
yake na hali ngumu ya uchumi?
Je! unadhani Yesu Kristo anaweza kukuokoa
halafu asikutunze kiuchumi katika maisha mapya ya wokovu? Nafahamu kuna
wakristo wengi walioanguka kiroho kwa sababu ya kutafuta njia za kujisaidia
kimaisha.
Biblia inatuambia ya kuwa Yesu Kristo
huwalisha na kuwatunza watu wake ili ajiletee kanisa (wakristo) walio
watakatifu. Soma Waefeso 5:25-33.
Katika vipindi vyote vya matatizo ya uchumi,
Mungu ameweza kuwalisha na kuwatunza watu wake. Wamekula na kuvaa na kulala
ndani ya mpango wake bila kumkosea.
Katika siku hizi za mwisho, Kristo
anazungumza na kulikumbusha kanisa (wakristo) juu ya njia au mbinu za kuchukua
wakati wa hali ngumu ya uchumi mahali walipo.
Mashauri muhimu ya kufanya
Fuata maongozi ya Mungu na siyo ya dunia: Ni
rahisi sana kusikia na kufuata ushauri wa wanadamu kuliko ushauri wa
Mungu hasa mtu anapobanwa na shida. Lakini kwa mkristo nakushauri siku zote
kuwe na shida au kusiwe na shida, fuata ushauri wa Mungu kama vile
anavyokuongoza kwa Roho Mtakatifu katika neno lake. Tuangalie jinsi Isaka
alivyofanya alipokumbwa na hali ya njaa.
"Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na
njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki,
mfalme wa Wafilisti, huko Gerari. Bwana akamtokea, akasema, usishuke kwenda
Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia …. Nami nitakuwa pamoja nawe, na
kukubariki …" (Mwanzo 25:1-3).
Njaa ilipotokea huko Gerari, watu walianza
kuondoka huko na kwenda Misri, ili kutafuta chakula. Ni wazi ya kuwa hata Isaka
alitaka kufanya hivyo. Bwana akamzuia akamwambia asiondoke bali akae katika
nchi aliyomwambia na katika nchi hiyo atakuwa pamoja naye na kumbariki au
kumfanikisha.
Nataka kukukumbusha ya kuwa baraka za Mungu
kwetu hazitegemei jinsi hali ya hewa na uchumi wa dunia hii unavyokwenda bali
zinategemea NENO LA KRISTO.
Isaka akatii, hakuondoka bali alibaki katika
nchi hiyo ambayo watu walikuwa hawapati chakula wakilima.
"Isaka akapanda mbegu katika nchi ile,
akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, Bwana akambariki" (Mwanzo
26:12).
Siku zote kaa na kufanya kazi mahali ambapo
Mungu amekuongoza kukaa. Usihame mahali au kuacha kazi, bila uongozi wa Mungu.
Kufanikiwa kwako hakutegemei mipango yako bali kunategemea mpango wa Mungu.
Ukiwa ndani ya Kristo utafanikiwa mahali po
pote pale ambapo Mungu atakapokuweka hata kama mazingira yake
kibinadamu si mazuri kwa kufanikiwa. Ukiwa ndani ya Kristo, "Utabarikiwa
mjini, utabarikiwa na mashambani … utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa utokapo ….
Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia
mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako" (Kumbukumbu
ya Torati 28:3,6,8).
Endelea kutoa hata wakati wa upungufu
Katika hali ya kibinadamu upungufu unapotokea
mahali watu wanabana matumizi – na hali ya ukarimu na utoaji huwa inafifia sana
hata wakati mwingine kupokea kabisa. Wakristo wengi pia wamekumbwa na hali hii
– wanasema wamepunguza utoaji kwa kuwa wamepungukiwa na hali ya uchumi ni
ngumu. Je! hii ni sawa?
Wakati wa ukame ulipotokea wakati wa maisha
ya Nabii Eliya Mtishbi; Bwana alimwambia Eliya, "Ondoka, uende
Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa
huko akulishe" (1Wafalme 17:9).
Unakumbuka jinsi yule mama alivyojitetea
wakati Eliya alipofika kwake ili alishwe? Yule mama alijitetea kama watu
wengine wanavyojitetea siku hizi wakitakiwa kutoa au kuchanga walivyo navyo kwa
ajili ya kazi ya Mungu. Naye yule Mjane akasema;
"Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina
mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami
ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tule
tukafe" (1Wafalme 17:12).
Kwa jinsi ya kibinadamu, Eliya angeweza
kumwonea huruma yule mama, asile chakula chake; na aondoke na aende kwa
matajiri wa siku zile kupata chakula. Lakini Eliya hakufanya hivyo- bali ALITII
MAAGIZO YA MUNGU. Eliya akamwambia yule mjane hivi;
"Usiogope;enenda ukafanye kama
ulivyosema; lakini unifanyie KWANZA mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie
nafsi yako na mwanao" (1Wafalme 17:13).
Ndivyo yule mama alivyofanya – alimpa KWANZA
MUNGU kwa kupitia mtumishi wake. Mungu akambariki yule mama kwa ukarimu na
utoaji wake wakati alipokuwa na upungufu. "Lile pipa la unga
HALIKUPUNGUKA, wala ile chupa ya mafuta HAIKUISHA sawasawa na NENO LA BWANA
alilolinena kwa kinywa cha Eliya" (1Wafalme 17:16).
Katika hali ya upungufu ulionao, usiwe mchoyo
bali endelea kumtolea Mungu, naye atakubariki na kukufanikisha. Na hii
itaonyesha ni kwa kiasi gani unamtegemea Mungu wako na Neno lake.
Lazima ufahamu ya kuwa Yesu Kristo anaangalia
sana jinsi tutoavyo. Siku moja akiangalia jinsi watu watoavyo fedha; "Akawaita
wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi
kuliko wote wanaotia katika sanduku la Hazina; maana hao wote walitia baadhi ya
mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo,
ndiyo riziki yake yote pia" (Marko 12:43-44). Soma na
kuyatafakari tena maneno hayo ya Yesu Kristo, halafu jiangalie jinsi utoavyo.
Huyu mjane hakuwa na mali ya kutosha alikuwa maskini, lakini bado aliendelea
kumtolea Mungu! Je wewe una la kujitetea katika kutomtolea Mungu wakati wa
upungufu wako?
|
Weka hazina yako mbinguni
Yesu Kristo alisema;"Msijiwekee hazina
duniani, nondo na kutu viharibupo,na wezi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni
hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wezi hawavunji
wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako" (Mathayo
6:19 – 21).
Utoaji wako utaonyesha kama moyo
wako uko kwa Yesu au unaitegemea dunia. Moyo wako
ukimtegemea sana Yesu, utatoa zaidi kwa ajili ya kazi ya Mungu kuliko
mahali pengine. Mkristo anapopoa kiroho, utoaji wake HASA kwa kazi ya kuhubiri
injili nao unapungua. Hata hivyo Biblia inatuambia katika siku za mwisho upendo
wa wengi utapoa.
Mtolee Mungu zaka na dhabihu (matoleo) bila
kuchoka, nawe utakuwa umeweka hazina yako mbinguni – mikononi mwa Mungu –
ambamo wezi hawawezi kukuibia. Naye Bwana atakurudishia mara nyingi zaidi.
Mradi mzuri na wenye uhakika wa mavuno kwa Mungu na kwako wakati wa hali ngumu
ya uchumi ni mradi wa kuhubiri injili. Kwa hiyo siku zote hakikisha umeweka
kiasi fulani katika mradi wa kuhubiri injili.
Dumu katika maombi
Hili ni muhimu sana. Kwa kuwa wakristo wengi
wakiwa katika hali ya ugumu wa maisha na uchumi, wanapoa katika maombi – na
wanakumbwa na majaribu ambayo mara nyingi yanachafua ushuhuda wao. Soma Luka
21:36, Mathayo 24:42 – 51 na Mathayo 26:41. Kwa hiyo dumu katika maombi,
usikate tamaa, hata wakati wa hali ngumu kiuchumi kwa upande wako – bado zidi
kudumu katika maombi.
JE! MAFANIKIO YAKO
KIFEDHA YANA MATATIZO?
Mwaka 1997 tulipokea barua na simu nyingi toka kwa watu wa Mungu mbalimbali
wakihitaji maombi kwa ajili ya matatizo yaliyokuwa yanawasumbua katika maeneo
ya kifedha. Wengine biashara na kazi zao vilikuwa haviendi vizuri -
nakadhalika.
Tulikaa na
jambo hili katika maombi. Tarehe 24 Septemba 1997 saa kumi na nusu asubuhi
tukiwa katika maombi Bwana Yesu alisema nasi katika mioyo yetu ujumbe ufuatao
ambao tunaamini utakusaidia hata wewe. Bwana Yesu alituambia hivi:
· roho
ya mpinga Kristo ndiyo iliyoshambulia mafanikio ya kifedha katika watu
wangu,
· Imeelekeza
mashambulizi katika mafanikio ya roho zao (na nafsi zao) maana nimesema
mtafanikiwa katika mambo yote kwa kadri roho zenu zifanikiwavyo,
· Kufanikikiwa
kwa roho zenu kunategemea kufanikiwa kwa nafsi zenu. Mtafanikiwa katika roho
zenu kwa kadri nafsi zenu zifanikiwavyo, na matokeo yataonekana katika mambo
yote
· Nafsi
zenu zifanikiwavyo zinategemea utendaji wenu wa Neno langu. Ikiwa utendaji wenu
wa Neno ukiwa hafifu, na kufanikiwa kwa nafsi zenu kunakuwa hafifu. Kufanikiwa
kwa nafsi zenu kukuwa hafifu na kufanikiwa kwa roho zenu kunakuwa hafifu, kwa
hiyo kufanikiwa katika mambo yote kunakuwa hafifu pia.
· Ndiyo
maana nasema roho ya mpinga Kristo imeelekeza mashambulizi yake katika kupinga,
kuzuia, na kuchelewesha mafanikio yenu katika roho na nafsi zenu.
· Lakini
mnaweza kushinda kwa kusimama katika Neno langu ambalo ni upanga wa Roho
mikononi mwenu.
· Nimesema
katika Yoshua 1:8 ya kuwa mtafanikiwa ikiwa mambo matatu yatafanyika juu ya
Neno langu:
(a) Lisiondoke kinywani mwenu
(b) Mlitafakari wakati wote
(c) Na kudumu kulitenda
· Sasa
angalia mmesimamaje katika maeneo hayo matatu. Maana hizo ni mbinu za kulitumia
Neno langu kama silaha ya kumshinda adui
· Mkisimama
katika Neno langu ninavyotaka mtavuna mafanikio sana kwa wakati wangu
msipozimia na kukata tamaa katika mioyo yenu.
· roho
ya mpinga Kristo inawakatisha tamaa kwa kuwaangaliza matokeo ya upungufu
mlionao badala ya kuangalia ahadi zangu na matokeo yake.
· Kwa
kadri mnavyoangalia matokeo ya upungufu mlionao, ndivyo mnavyozidi kutafakari
juu ya upungufu mlionao. Kwa kadri mnavyozidi kutafakari juu ya upungufu
mlionao, ndivyo mnavyozidi kukiri na kushuhudia upungufu mlionao na matokeo
yake.
· Kumbuka
mnayafunga mafanikio yenu kwa maneno ya vinywa vyenu yanayotoka katika nafsi
zisizotafakari ahadi zangu na matokeo yake.
· Mimi
si mtu hata niseme uongo. Nililolisema katika Neno langu nimesema
nitalitimiliza. Napenda kufanikiwa kwenu kuliko nyinyi mnavyopenda kufanikiwa
kwa watoto wenu. Msikubali adui ayumbishe macho yenu na mioyo yenu isione
uaminifu wangu.
· Mkisimama
katika neno langu na kupigana hivyo vita vizuri vya imani mlivyo navyo;
- mtashangilia ushindi wakati kuta hazijaanguka bado,
- mtatangaza ushindi wakati bado upinzani wa adui umesimama,
- mtaona mafanikio wakati bado mmezungukwa na upungufu,
· Kumbuka
neno langu linatangaza ushindi katika roho kwanza kabla ya haujaonekana kwa
nje. Ndicho kilimchomsaidia Ibrahimu wakati anasubiri mtoto wake. Na ndicho
kilichonisaidia na mimi pale masalabani - nilishangilia ushindi dhidi ya adui
hata kabla sijafufuka. Daudi naye aliuona ushindi wakati bado Goliati amesimama
mbele yake.
Kila mtu atakuja kwangu na kuuliza nimpe Neno la kusimamia katika vita alivyo
nayo. Hamuwezi kushinda pasipo Neno.
Haya ndiyo machache tuliyoyapokea kutoka kwa Bwana Yesu tulipofanya maombi ya
kuuliza kwa nini watu wengi wa Mungu wamekuwa hawafanikiwi vizuri katika eneo
la fedha. Ingawa Bwana alisema nasi mwaka 1997 tunaamini bado ujumbe una nguvu
ndani yake ya kukusaidia. Tafakari maneno ya ujumbe huu, weka katika matendo
yaliyomo - na Mungu atakusaidia!
Ahsante,
Christopher na Diana Mwakasege
Post A Comment:
0 comments so far,add yours