Mwaka
1997 tulipokea barua na simu nyingi toka kwa watu wa Mungu mbalimbali
wakihitaji maombi kwa ajili ya matatizo yaliyokuwa yanawasumbua katika maeneo
ya kifedha. Wengine biashara na kazi zao vilikuwa haviendi vizuri -
nakadhalika.
Tulikaa na jambo hili katika maombi. Tarehe 24 Septemba 1997 saa kumi na nusu
asubuhi tukiwa katika maombi Bwana Yesu alisema nasi katika mioyo yetu ujumbe
ufuatao ambao tunaamini utakusaidia hata wewe. Bwana Yesu alituambia hivi:
roho ya mpinga Kristo ndiyo iliyoshambulia mafanikio ya
kifedha katika watu wangu,
Imeelekeza mashambulizi katika mafanikio ya roho zao (na nafsi zao) maana
nimesema mtafanikiwa katika mambo yote kwa kadri roho zenu zifanikiwavyo,
Kufanikikiwa kwa roho zenu kunategemea kufanikiwa kwa nafsi zenu. Mtafanikiwa
katika roho zenu kwa kadri nafsi zenu zifanikiwavyo, na matokeo yataonekana
katika mambo yote
Nafsi zenu zifanikiwavyo zinategemea utendaji wenu wa Neno langu. Ikiwa
utendaji wenu wa Neno ukiwa hafifu, na kufanikiwa kwa nafsi zenu kunakuwa
hafifu. Kufanikiwa kwa nafsi zenu kukuwa hafifu na kufanikiwa kwa roho zenu
kunakuwa hafifu, kwa hiyo kufanikiwa katika mambo yote kunakuwa hafifu pia.
Ndiyo maana nasema roho ya mpinga Kristo imeelekeza mashambulizi yake katika
kupinga, kuzuia, na kuchelewesha mafanikio yenu katika roho na nafsi zenu.
Lakini mnaweza kushinda kwa kusimama katika Neno langu ambalo ni upanga wa Roho
mikononi mwenu.
Nimesema katika Yoshua 1:8 ya kuwa mtafanikiwa ikiwa mambo matatu yatafanyika
juu ya Neno langu:
(a) Lisiondoke kinywani mwenu
(b) Mlitafakari wakati wote
(c) Na kudumu kulitenda
Sasa angalia mmesimamaje katika maeneo hayo matatu. Maana hizo ni mbinu za
kulitumia Neno langu kama silaha ya kumshinda adui
Mkisimama katika Neno langu ninavyotaka mtavuna mafanikio sana kwa wakati wangu
msipozimia na kukata tamaa katika mioyo yenu.
roho ya mpinga Kristo inawakatisha tamaa kwa kuwaangaliza matokeo ya upungufu
mlionao badala ya kuangalia ahadi zangu na matokeo yake.
Kwa kadri mnavyoangalia matokeo ya upungufu mlionao, ndivyo mnavyozidi
kutafakari juu ya upungufu mlionao. Kwa kadri mnavyozidi kutafakari juu ya
upungufu mlionao, ndivyo mnavyozidi kukiri na kushuhudia upungufu mlionao na
matokeo yake.
Kumbuka mnayafunga mafanikio yenu kwa maneno ya vinywa vyenu yanayotoka katika
nafsi zisizotafakari ahadi zangu na matokeo yake.
Mimi si mtu hata niseme uongo. Nililolisema katika Neno langu nimesema nitalitimiliza.
Napenda kufanikiwa kwenu kuliko nyinyi mnavyopenda kufanikiwa kwa watoto wenu.
Msikubali adui ayumbishe macho yenu na mioyo yenu isione uaminifu wangu.
Mkisimama katika neno langu na kupigana hivyo vita vizuri vya imani mlivyo
navyo;
- mtashangilia ushindi wakati kuta hazijaanguka bado,
- mtatangaza ushindi wakati bado upinzani wa adui umesimama,
- mtaona mafanikio wakati bado mmezungukwa na upungufu,
Kumbuka neno langu linatangaza ushindi katika roho kwanza kabla ya haujaonekana
kwa nje. Ndicho kilimchomsaidia Ibrahimu wakati anasubiri mtoto wake. Na ndicho
kilichonisaidia na mimi pale masalabani - nilishangilia ushindi dhidi ya adui
hata kabla sijafufuka. Daudi naye aliuona ushindi wakati bado Goliati amesimama
mbele yake.
Kila mtu atakuja kwangu na kuuliza nimpe Neno la kusimamia katika vita alivyo
nayo. Hamuwezi kushinda pasipo Neno.
Haya ndiyo machache tuliyoyapokea kutoka kwa Bwana Yesu tulipofanya maombi ya
kuuliza kwa nini watu wengi wa Mungu wamekuwa hawafanikiwi vizuri katika eneo
la fedha. Ingawa Bwana alisema nasi mwaka 1997 tunaamini bado ujumbe una nguvu
ndani yake ya kukusaidia. Tafakari maneno ya ujumbe huu, weka katika matendo
yaliyomo - na Mungu atakusaidia!
Ahsante,
Mwl.
Christopher Mwakasege
Post A Comment:
0 comments so far,add yours