Tangu unapoomba sala
ile ya kumpokea BWANA YESU awe Bwana na mwokozi wa maisha yako (sala ya toba),
kuna mambo mengi yanatokea maishani mwako, ila huwezi ukayaona kwa macho, yote
yanafanyika katika ulimwengu wa roho ambayo macho ya kawaida hayawezi kuona.
Kwanza historia yako yote ya nyuma inafutwa na unaanza maisha mapya pamoja
na Mungu, “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe
kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya ” (2korintho 5:17).
Imeandikwa wazi
kabisa katika kitabu cha Waefeso 2:19 ya kuwa; “Basi tangu sasa ninyi
si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa
nyumbani mwake Mungu”.
Unapata neema hii ya
Mungu, na sasa unakuwa raia wa Mbinguni – biblia inakuambia tangu sasa wewe si
mgeni wala mpitaji katika Ufalme wa Mungu – bali wewe ni mwenyeji pamoja na
watakatifu wengi waliomo katika nyumba ya Mungu!
Nia ya Roho Mtakatifu
kukupa nafasi ya kusoma ukurasa huu, ni kukufahamisha angalau kwa kiasi fulani
juu ya umuhimu wa kutubu dhambi zako, na kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na
Mwokozi wako.
Ukisoma ukurasa huu
utakusaidia kujua kitu gani kinatokea unapo mpokea Bwana Yesu na mambo muhimu
ya kufanya katika maisha hayo mapya ya Ufalme wa Mungu.
Matokeo ya Kumpokea
Bwana Yesu
-
Unasamehewa dhambi zako zote!
“Na ninyi mlipokuwa
mmekufa kwa sababu ya makosa yenu…. Aliwafanya hai pamoja naye, akiisha
kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki
kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea
msalabani …” (Wakolosai 2:13,14).
“Tukiziungama dhambi
zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha
na udhalimu wote” (1Yohana 1:9).
-
Unahamishwa toka katika ufalme wa shetani na
kuingizwa katika Ufalme wa Mungu.
“Naye alituokoa
katika nguvu za giza, na akatuhamisha na kutuingiza katika
Ufalme wa mwana wa pendo lake;” Wakolosai 1:13.
Kuna falme mbili
zinazopingana na kila mtu ni raia katika mojawapo wa falme hizi. Kuokoka ni
kuondolewa katika ufalme wa giza (shetani) na kuhamishiwa katika Ufalme
wa Mungu. Unakubali kutubu na kumwelekea Mungu si tu unasamehewa
dhambi lakini pia unahamishwa na kuingizwa katika Ufalme wa Bwana Yesu (mwana
wa pendo la Mungu) ukiwa katika Ufalme wa Mungu huna haja tena na msaada wa shetani
katika maisha yako. Hirizi, utabiri wa nyota, mazindiko, ibada za mizimu na
ibada za kimila huvihitaji tena. Ulipotubu umebadili msimamo na mwelekeo wako
hivyo unaviondoa vitu hivi katika maisha yako maana wewe si raia wa ufalme wa
shetani hata kautii na kuutumikia. Yesu ndiye mfalme wako na anawajibika
kukulinda.
- Jina
lako linaandikwa mbinguni!
“…furahini kwa sababu
majina yenu yameandikwa mbinguni” (Luka 10:20).
“Yeye ashindaye
atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha
uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake”
(Ufunuo 3:5).
-
Unakuwa mwanfunzi wa Yesu.
“Basi enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana,
na Roho mtakatifu.” Mathayo 28:19
- Unakuwa
kiumbe kipya!
“Hata imekuwa, mtu
akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa
mapya” (2Wakorintho 5:17).
“Lakini mimi, hasha,
nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo,
ambao kwa huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu
kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiri, bali kiumbe kipya” (Wagalatia 6:14,15).
“Mvue kwa habari ya
mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye
kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu, mkavae utu mpya ulioumbwa
kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli” (Waefeso 4:22-24).
-
Umekuwa mtoto wa Mungu!
“Bali wote
waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio
jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa
mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu (Yohana 1:12,13).
“Tazameni, ni pendo
la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo…
Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini
twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama
alivyo” (1Yohana 1:1,2).
-
Malaika wanakuzunguka hata kama huwaoni!
“Je! hao wote
(malaika) si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale watakaorithi wokovu?
(Waebrania 1:14).
“Kwa kuwa atakuagizia
malaika zake wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, usije
ukajikwaa mguu wako katika jiwe” (Zaburi 91:11,12)
-
Unakuwa makao ya Kristo na Mungu!
“Yesu akajibu,
akamwambia, mtu akinipenda atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi
tutakuja kwake, na kufanya makao kwake” (Yohana 14:23)
“Nimesulibiwa pamoja
na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na
uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye
alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu” (Wagalatia 2:20).
“Katika yeye ninyi
nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho” (Waefeso 2:22).
-
Roho Mtakatifu yumo ndani yako sasa!
“Lakini, ikiwa Roho
wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua
Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa
roho wake anayekaa ndani yenu” (Warumi 8:11).
“Au hamjui ya kuwa
miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu?
(1Wakorintho 6:19).
-
Una mamlaka juu ya shetani na kazi zake tangu sasa!
“Tazama, nimewapa
amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru”
(Luka 10:19)
“Na ishara hii
zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo …. Wataweka mikono yao
juu ya wagonjwa, nao watapata afya” (Marko 16:17,18).
“Basi mtiini Mungu.
Mpingeni shetani, naye atawakimbia” (Yakobo 4:7).
-
Utafufuliwa au kunyakuliwa Yesu akija kulichukua
kanisa maana unao uzima wa milele!
“Yeye aliye naye
Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima” (1Yohana
5:12).
“Kwa sababu Bwana
mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu,
na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha
sisi tulio hai tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki
Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele” (1Wathesalonike 4:16,17).
“Huo ndio ufufuo wa
kwanza. Heri na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu
ya hao mauti ya pili haina nguvu …. (Ufunuo 20:6
- Unahesabiwa haki
na Mungu.
Kuhesabiwa haki maana
yake ni kuonekana kuwa huna hatia mbele za Mungu. Huna kesi, hivyo una kibali
mbele zake.
“kwa kuwa wote
wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, wanahesabiwa haki bure kwa
neema Yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. Yeye ambaye Mungu
alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu Yake. Alifanya
hivi ili kuonyesha haki Yake, kwa sababu kwa ustahimili Wake aliziachilia zile
dhambi zilizotangulia kufanywa. Alifanya hivyo ili kuonyesha haki Yake wakati
huu, ili Yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini
Yesu.” Warumi 3:23-26.
Haya ni baadhi tu ya
maneno mengi mazuri ambayo yamo katika biblia yanayoeleza kilichotokea
ulipookoka. Nakupa ushauri ya kuwa uyasome mara kwa mara pamoja na mengine
yaliyomo katika biblia ili upate kujijua wewe sasa ni nani mbele za Mungu
na za shetani baada ya kuokoka.
Post A Comment:
0 comments so far,add yours