SURA YA KUMI NA TATU
NAMNA YA KUMSIFU NA
KUMWABUDU MUNGU
Tumejifunza mambo mengi sana yaliyokuhamasisha na yaliyokupiga deni uwe
kiumbe wa kumsifu na kumtukuza Mungu. Tunapomsifu mtu, huwa tunaelezea yale
ambayo yanamtofautisha na wengine. Hivyo basi, ufikapo katika muda wa kumsifu
na kumwabudu Mungu, ujue namna ya kuifanya sifa yako na ibada yako kwa usahihi.
Na ili kumpa
Mungu sifa na ibada, ni lazima na ni muhimu sana ujue mambo ambayo
yanamstahilisha Mungu wetu kusifiwa na kutukuzwa. Kwa kutumia sifa na tabia za
Mungu, utaweza kumsifu na kumwabudu vizuri. Hakuna kiumbe kingine chochote kinazo zile sifa kuu
tano za Mungu, isipokuwa yeye Mungu Jehova peke yake.
Kwahiyo, na hizo ndizo zinayomstahilisha yeye kusifiwa na viumbe wake.
Katika sura ya nane, tumeshajifunza mambo
yanayomstahilisha Mungu kupewa sifa. Kwakuwa sasa unayajua, basi tumia mambo
hayo uendapo mbele za Mungu katika katika ibada yako ili kumsifu na kumwabudu.
Unapomueleza Mungu sifa zake na tabia zake (vile alivyo) hapo unakuwa unamsifu
na kumwabudu.
Tofauti ya kusifu na kuabudu
Naomba urudie kuisoma sura ya kwanza ya kitabu hiki, ambapo
nimefundisha vizuri maana ya kumshukuru Mungu, kumsifu Mungu na kumwabudu
Mungu. Hii itakusaidia kutofautisha mambo haya kwa nia ya kuyaelewa au
kuyaelezea kwa mtu mwingine. Nilisema hivi,
Ibaba ni kitendo cha mtu kumtukuza, kumhimidi,
kumwinua, kumwadhimisha, kumshukuru na kumheshimu Mungu kwa vile alivyo na kwa
yale aliyoyatenda. (Appreciation and admiration for who God is and
for what He has done).
Lakini haya mambo matatu, yanayofanana sana na si rahisi sana kuyatenganisha
kimaelezo au kivitendo.
Lakini tuendapo
mbele za Mungu kwa ibada, iwe ni chumbani kwako au sebuleni kwako au kwenye
gari lako au kanisani kwako, kusifu na kuabudu na kushukuru, ni mambo
yanayofanyika kwa kuingliana sana. Sio sheria kwamba, hautakiwi kuchanganya
sifa na kuabudu na kushukuru, hapana. Hebu soma tena sura ya kwanza vizuri.
Kati ya mengi, nilisema hivi;
Haya mambo matatu, kusifu, kushukuru na kuabudu, ni mambo yanayofanana sana. Inaweza
ikawa vigumu kidogo kuyatenganisha kimaelezo au kivitendo. Ni ngumu kidogo,
kufanya kimoja pasipo wenzake, kwasababu ni mambo yanayokwenda kwa pamoja sana.
Lakini kwa tafsiri zake, yako hivi;
1. Kumshukuru Mungu;- Ni ile hali ya
kumueleza Mungu jinsi tunavyothamini (Appreciate and Admire) wema wake, fadhili zake na baraka zake katika maisha yetu.
2. Kumsifu Mungu; - Ni kumueleza Mungu juu ya matendo
yake makuu na ya ajabu aliyoyafanya.
Au ni kuwaeleza wengine kuhusu matendo makuu ya Mungu
aliyoyafanya katika maisha yetu au kwa watu wengine.
3. Kumwabudu Mungu; - Ni kumueleza Mungu tukuzo zetu, heshima yetu na
upendo wetu kwake kwasababu ya uzuri wa tabia zake kwetu.
(Credentials and Characters).
Kwahiyo, tuendapo mbele za Mungu kwa ibada, iwe ni chumbani kwako au
sebuleni kwako au kwenye gari lako au kanisani kwako, ili kumsifu na kumwabudu
na kumshukuru Mungu, uwe huru kujimimina mbele za Mungu kwa kufanya vyote
vitatu, kwa namna moyo wako utakavyokuwa unaongozwa na Roho Mtakatifu. Vyote
vitatu vinatengeneza ibada takatifu kwa Mungu.
Katika sura
inayokuja, nimefundisha vizuri namna ya kuingia katika ibada na hata kupenya na
kufika katika chumba cha ndani kabisa cha uwepo na utukufu wa Mungu; ili
unapokwenda mbele za Mungu wetu, uweze
kukutana na nguvu zake katika utukufu wake.
Lakini hapa chini nimeziweka kwa ufupi ili kukukumbusha. Na pia
nimekuongezea na mambo mengine yanayotakiwa katika kumsifu na kumtukuza Mungu.
Kwahiyo, utengapo muda wa kukaa mbele za Mungu wetu kwa ibada, msifu na
kumtukuza Mungu kwa mambo yafuatayo,
1.
Mtukuze Mungu kwa Sifa
zake za Uungu (ambazo hakuna mwingine aliye nazo) Kwamba;
a) Jehova ni Mungu wa Milele
b) Jehova ni Mungu Mtakatifu
c) Jehova ni Mungu Aliye kila mahali
d) Jehova ni Mungu Anayejua mambo
yote
e) Jehova ni Mungu Aliye na nguvu
zote na
anaweza kufanya mambo yote kabisa.
Nimezielezea vizuri hizi sifa za Uungu, katika
sura ya kwanza. Hizi ni baadhi tu ya sifa za Mungu, sio zote. Kwa hivyo basi,
pamoja na namna nyingine ambazo utajifunza kumsifu na kumwabudu Mungu, hebu uwe
unamsifu Mungu kwa mambo haya au kwa sifa zake hizi pia.
Msifu Mungu kwa;
2.
Kwasababu ya Tabia zake
3. Kwasababu ya Matendo yake ya Ajabu
4.
Kwasababu ya Fadhili
nyingi na kuu mno
5. Kwasababu ya Ahadi zake kubwa za thamani
2. Mtukuze Mungu kwa Tabia zake
Neno la Mungu, linatuonyesha jinsi ambavyo Mungu
wetu ana tabia na kawaida nyingi nzuri ambazo kwa hizo, tunavutiwa na tunapigwa
deni kumsifu na kumwabudu. Kwa mfano ; Biblia inasema kwamba, Mungu wetu
amejaa Upendo, usio na mwisho. Ni Mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, sifa
yake ni kuwa na rehema daima. Soma mistari ifuatayo, ili uone zaidi. Lakini
kwasababu ya sifa hizi (Tabia zake), tunapigwa deni kumsifu na kumwabudu.
*Zaburi 103:8, Kutoka 34 :6,
*Efeso 3 :18-19, Daniel 9 :4, Ufunuo
19 :11
3. Mtukuze Mungu kwa Matendo yake ya ajabu.
Mungu wetu ni Mungu aliyefanya mambo ambayo hakuna
tena, awezaye kufanya. Kwa mfano; ndiye aliyeziumba na kuzitundika sayari zote
za ulimwengu huu, bila minyororo wala nguzo. Mungu wetu ndiye anayesababisha
mioyo yetu inadunda, bile kuwekewa betrii wala chaji (charge). Au ni lini
ulichomeka moyo wako katika soketi ya umeme kama unavyochomeka simu yako ili kupata
umeme?
Nina uhakika, hakuna mtu anayefanya hivyo.
Sasa unadhani moyo wako unadundaje? Hizo ni kazi za ajabu za Mungu wetu.na
hakuna mtu awezaye kuzifanya. Kwasababu ya matendo yake ya ajabu, Mungu wetu
anastahili kusifiwa na kutukuzwa. Soma mistari ifuatayo kwa umakini. Utaweza
kuona kwa uchache, jinsi maandiko yanavyoeleza juu ya matendo makuu ya Mungu.
Haya ni maelezo ya watu wa Mungu ambao kwa kumjua
Mungu, waliweza kueleza ukuu wake vizuri, ili na sisi tunaosoma maandiko yao,
tunajifunza juu ya ukuu wa Mungu, uweza wa Mungu na tabia za Mungu wetu. Soma
vizuri Kitabu cha Daniel 6:25-27,
Nehemia 9:6, Zaburi
147:1-18, na Zaburi sura ya 136:4-26
4. Mtukuze Mungu
kwa Fadhili zake.
Mungu wetu ni Mungu atupaye baraka na fadhili
nyingi kila siku. Fikiri wema ambao Mungu amekufanyia maishani mwako, na hata
katika siku ya leo tu. Kuna vingi ametupa ambavyo wengi walitamani, lakini
hawakupewa. Uhai, afya, ulinzi, rehema, chakula, fedha, shule, simu, gari,
nyumba, ajira, mke, mume, watoto, na hata wazazi.
Sio kila mtu bado ana wazazi. Na wengine wamezaliwa hawajawahi kuwajua
wazazi wao. Kwakweli fadhili na baraka za Mungu ni nyingi sana; ukiamua
kuziorodhesha, utakesha. Sasa, kwa fadhili zote hizi alizotujalia, basi Mungu
wetu anstahili kusifiwa.
*Zaburi
103:1-5, Zaburi 107:21, 2Nyakati 20:21
5.
Mtukuze Mungu
kwa Ahadi zake.
Ni Mungu aliyetuahidi watu wake, mambo mengi sana mazuri. Ametupa ahadi
kubwa mno na za thamani sana. Ni ahadi za kutupa baraka, heshima na utajiri.
Kwa ahadi hizi pia, anastahili kusifiwa *
2Petro 1:3-4, Efeso 1:3-4, Kumbu 4:4-8
Kwa ufupi, hivi ndivyo unavyotakiwa kumsifu na kumwabudu Mungu. Kadri
unavyoanza kufanya hivi kwa vitendo, utaendelea kujifunza kufanya huduma hii
ipasavyo, nawe utajikuta unakutana na nguvu za Mungu kwa namna ya tofauti
maishani mwako.
MSIFU MUNGU
KWA MAJINA YAKE.
Majina ya Mungu, hueleza sifa za Mungu, Tabia za
Mungu au Matendo ya Mungu. Mfano; Wayahudi wanamwita Mungu El-Shaddai. Ni neno lenye
majina mawili ndani yake. ‘El’ maana yake Mungu, na ‘Shaddai’ lenye maana itokanayo na
neno ‘Shad’
yaani Titi (Ziwa) la mama
anyonyeshaye. Kutokana na ukweli kwamba, titi/ziwa la
mama anyonyeshaye, linampa mtoto mchanga kila kitu anchohitaji. Maziwa ya mama
yake, humpa mtoto kila kitu mtoto anachohitaji. Ndani ya maziwa kuna vitamini,
protini, wanga, mafuta, madini, maji, na kila kitu mtoto anachohitaji. Maziwa
ya mama, yanamtosheleza mtoto kwa kila kitu. Hivyo, Waisraeli
wanapomwita Mungu El-Shaddai, wanamaanisha kuwa, kama ziwa linavyo mtosheleza mtoto, vivyo hivyo, Mungu
ni ‘Mtoshelezi’ kwetu.
Halleluyah! Hivyo, kila jina la Mungu, linabeba
aidha Sifa yake au Tabia yake au Matendo yake. Ndio maana Mfalme Daudi anasema
“Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu … Mpeni Bwana utukufu kwa jina lake. Mwabuduni Bwana kwa
uzuri wa utakatifu.” (Zab 29:1-2) Msifuni Bwana kwa kuwa Bwana ni mwema, Liimbieni Jina lake, kwakuwa
lapendeza.(Zaburi 135:3).
Na Bwana Yesu alitufundisha kuanza sala namna
hii;
Baba
yetu uliye mbinguni, jina lako
tukutuzwe, hakafu Ufalme wako uje hapa duniani.
Kwahiyo, unaweza pia kumsifu Bwana kwa majina yake. Majina ya Mungu, hueleza aidha sifa za Mungu au tabia
za Mungu au Matendo makuu ya Mungu. Yafuatayo hapa
chini, ni baadhi ya majina ya Mungu kwa lugha ya Kiebrania, yatakayokusaidia
kumsifu, kumwabudu na kumshukuru Mungu.
MAJINA YA MUNGU
Jina la Mungu Maana yake Mstari wa Biblia
1.
Adonai - Mungu Mwenye enzi yote - Mwa
15:2-8, Kut 6:2-3
2.
El-Ohim - Mungu
Muumbaji - Mwa
33:20, Kol 1:16-17
3.
El-Elyon - Mungu Aliye juu
zaidi - Mwa14:18, Dan 4:34
4.
El-Gibbor - Mungu
Mwenye Nguvu - Isa 9:6,
Zab 147:5
5.
El-Hai - Mungu
Aliye Hai/Anaishi - Josh 3:10,
1Sam17:26
6.
El-Olam - Mungu wa Milele - Ufu 4:8,
Kut 3:14
7.
El-Roi - Mungu Aonaye
kila kitu - Mith 15:3, Zab 32:8
8.
El-Shaddai - Mungu
Mtoshelezi - Mdo 17:28, Kumb 8:4
9.
Jehovah - Ajitegemeaye
kuwepo -Kut 6:2-8, Mdo 17:24-25
10.
Jehovah Shalom -Mungu Amani yetu - Amu 6:22-24
11.
Jehovah
Rapha -
Mungu Atuponyaye
- Kut 15:26
12.
Jehovah
Jireh -
Mungu Mtoaji wetu - Mwa 22:
8, 14
13.
Jehovah Nissi - Mungu Ushindi wetu - Kut 14:13-14
14.
Jehovah Saboath - Bwana wa Majeshi -
Malaki 3:7
15.
Jehovah Shammah - Bwana ni Aliyepo -
Kut 3:14
16.
Jehovah Rohi - Bwana
ni Mchungaji wangu - Zab
23:1
17.
Jehovah Tsidkenu - Bwana ni Haki yetu -
Yer 23:6
18.
Jehovah Mekaddishem - Bwana Atutakasaye - Kut
31:13
Namna za
kumshukuru, kumsifu, na kumwabudu Mungu wetu.
Kwahiyo, katika maisha yetu sisi, kama waumini,
tunatakiwa kumpa Mungu wetu ibada, (kumshukuru, kumsifu na kumwabudu) kwasababu ya mambo yote hayo
niliyoyataja. Tunatakiwa kumtukuza Mungu kwasababu ya sifa zake, na kwasababu
ya tabia zake, na matendo yake na fadhili zake na ahadi zake kwetu.
Sasa basi, hapa chini, nimekuwekea njia
kuu tatu ambazo unaweza kumsifu na kumtukuza Mungu kwazo. Utengapo muda wa
kwenda mbele za Mungu, unaweza kutuia njiia kuu zifuatazo; Kumtukuza Mungu kwa,
- Kumwimbia nyimbo za
kumsifu na kuwabudu
- Kumweleza au
kusimulia kwa maneno
- Kumtolea Mungu sadaka
na dhabihu
Wako katika kazi ya Mungu
Mwl. Mgisa Mtebe
+255 713 497
654
mgisamtebe@ yahoo.com
www.mgisamtebe.com
SOMO JEMA SANA,LINAFUNGUA MILANGO,KUNA NGUVU KUBWA KATIKA KUSIFU
JibuFutaMwalimu, Mungu akubariki sana. Nilikuwa na haja sana ya kuelewa mambo haya na ama kwa hakika nimepata kitu. Roho Mtakatifu azidi kukufunulia mambo mengi zaidi kwa ajili ya watu wake.
JibuFutaKristo akutunze.
Nimejifunza kitu.asante sana mwalimu
JibuFutavitabu kama vipo kuhusu hili somo nipo tayar kununua nipo morogoro
JibuFutaAmen..nmejifunza sana kupitia kitabu hiki..Mungu akubariki Mwalimu
JibuFutaSomo zuri sana nimebarikiwa
JibuFutaMwalimu - Mungu akubariki sana na endelee kukuongoza na kukuongeza katika Neno. Nimejifunza sana
JibuFuta