MSAMAHA
Tukisoma kitabu cha WAEFESO 4:31,32 tunaona Biblia Takatifu
inasema kwamba:
"Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano
yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa
ninyi, wenye huruma, MKASAMEHEANE kama na Mungu katika Kristo
ALIVYOWASAMEHE ninyi." (Efe 4:31,32)
Je! Nini maana ya neno MSAMAHA na kuna faida zipi katika
KUSAMEHE; na kwa nini tunapaswa KUSAMEHE?
MSAMAHA:
Neno “MSAMAHA” ni neno jepesi kulitamka lakini ni pana sana katika
maana. Nisemapo "NI NENO JEPESI KULITAMKA" ninamaanisha kulitamka tu
kwa kawaida na katika hali ya kawaida tu pasipo kukosewa, lakini kwa watu
wengi; neno MSAMAHA ni neno gumu sana kulitamka toka rohoni mwao
hususani pindi wanapokosewa. Nilifanya utafiti juu ya hili neno nikagundua zipo
siri kubwa sana katika KUSAMEHE ambazo Shetani apendi watu
wazifahamu.
Tukirudi kwenye neno “SAMEHE” maana yake ni: Kukoma / kuacha kuhisi hasira juu
ya mtu ambaye amekuumiza, kakukwaza au kakuudhi; Pia, kukoma / kuacha kuhisi
hasira juu yako wewe mwenyewe (kuto kujichukia).
Neno MSAMAHA, kwa maana nyepesi linamaanisha kama ifuatavyo;
Þ Kutolipiza kisasi japokuwa unayo haki ya kulipiza kisasi.
Þ Ni tendo la imani na tena la hiari kwa kuwa unayo sababu, uwezo,
na haki ya kulipiza kisasi kutokana na yale uliyo umizwa.
Je! Unafahamu ni kwa nini watu wengi ni wagumu KUSAMEHE?
Watu wengi hushindwa kusamehe kwa sababu hawana Roho Mtakatifu
ndani yao; kwamba, wameruhusu maisha yao kutawaliwa na Shetani.
Dhana hiyo inao ukweli mkubwa ndani yake na pia wapo watu wajiitao watumishi wa
Mungu lakini nao wanashindwa KUSAMEHE. Si kwamba tu tunasamehe ili na sisi
tupate kusamehewa; La, si hivyo tu, bali zipo faida nyingi sana zipatikanazo
kwenye KUSAMEHE.
Siku zote mtu anapokosewa, ndani yake anazaa UCHUNGU, asipokuwa makini nao
UCHUNGU unazaa CHUKI, na pia hasipojiadhari hiyo CHUKI inazaa HASIRA. Na hapo
ndipo Shetani anapata mlango wa kumwingia mtu. Vitu hivyo vitatu; yaani,
UCHUNGU, CHUKI na HASIRA mara zote huandamana. Usipoweza kuudhibiti UCHUNGU,
unakuwa unaweka wazi mlango wa Shetani kukutawala.
Mtu kuokoka haimaanishi ndiyo mwisho wa makwazo na majaribu mbalimbali, bali
tambua unapo mpokea Yesu Kristo awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako unakuwa
umetangaza vita dhidi ya Shetani na majeshi yake ya pepo waovu. Shetani
atajaribu kukuingia moja kwa moja, lakini akishindwa, anatafuta mbinu ya
kumuingia mtu mwingine ili akukwaze; nawe ukikwazika ndipo Shetani anapata
nafasi ya kukuingia na kukutawala kupitia UCHUNGU, CHUKI, na HASIRA.
Tumeona mifano mingi ya watumishi wa Mungu walio anguka kiimani kwa kushindwa
KUSAMEHE; Huduma nyingi za kuhubiri Neno la Mungu zimekufa kwasababu ya
KUTOSAMEHE; Makanisa mengi yamevunjika na kutengana kwa sababu tu ya
KUTOSAMEHE; Ndoa nyingi na uchumba mwingi umevunjika kwasababu ya KUTOSAMEHE;
Makampuni mengi yamevunjika kwa sababu ya KUTOKUSAMEHE, utaona mkurugenzi
amekwazana na meneja alafu kampuni inapoteza muelekeo, utendaji unakuwa mbovu
na hatimae kampuni inakufa. Yote hayo unaweza kukuta chanzo chake ni
KUTOSAMEHE.
Siku zote unapokwazika Shetani anakuwa anakuletea hati ya mashtaka kwenye
mawazo yako; utasikia siuti ikikwambia;
"YAANI FULANI AKUFANYIE HIVI
KABISA ALAFU UMSAMEHE? HAPANA !!! LAZIMA UMKOMESHE. HAIWEZEKANI UMSAMEHE HIVI
HIVI TU WAKATI AMEKUPA HASARA YOTE HII.”
Ndipo nawe waweza ukajikuta
yanakuingia akilini na ukaanza kusema: “Kweli; HAIWEZEKANI KABISA, TENA YAANI,
ATANITAMBUA MIMI NI NANI."
Utaona Shetani anakukumbushia tukio jinsi ulivyo tendewa.
Utasikia ushauri mwingisana ndani ya fahamu zako. Tena maneno hayo
yanaweza kukupa UCHUNGU sanakiasi cha kushindwa kula, na hata ukatokwa na
machozi. Na akili ya mwanadamu ni rahisi kunasa mabaya kuliko mema; ni rahisi
kukumbuka mabaya kuliko mema; hapo ndipo Shetani huchukulia point endapo
usipokuwa makini.
Ukimruhusu Shetani katika akili zako; ndipo utajikuta
ukimtazama aliyekukwaza ni mtu wa karibu sananawe, ambae ulitegemea
angekuwa msaada kwako lakini amekurudisha nyuma na kuuumiza sana moyo
wako. Hauna raha, amani wala matumaini yoyote yale. Yawezekana akawa ni rafiki
yako wa karibu sana amesababisha ufukuze kazi kwa kosa ambalo
hukulifanya. Kweli inauma sana; inaleta huzuni na uchungu ukiwaza utafanya
nini na wale wanaokutegemea. Inaumiza sana.
Kwa wakati huo, ukijitizama uwezo wa kumdhuru unao, sababu ya kumdhuru unayo,
na nia ya kumdhuru unayo. Na kila mtu unaemsimulia anakwambia:
"Mbona wewe mjinga hivyo? Ingekuwa ni mimi, kamwe siwezi
kumlazia damu huyo, lazima angenitambua."
Kwa wakati huo moyo wako umejaa UCHUNGU, CHUKI na HASIRA. Lakini
kwa mbali saaaana, unasikia sauti ndani ya moyo wako ikisema: MSAMEHE.
Nadhani ata wewe waweza kutambua ni jinsi gani ilivyo vigumu kuitii hiyo sauti
isemayo SAMEHE kwa kuwa ukitazama ni kweli umeonewa, uwezo wa kulipa kisasi
unao, na hata ukilipa kisasi au kudhuru wapo watu watakaosema "Kwa kweli
umefanya vizuri kumkomesha. Ilimpasa hivyo."
Na kama ukitenda jambo baya juu yake; fahamu kwamba hiyo imetokana na
wewe kuruhusu UCHUNGU ukutawale. Wengine hufikia hata hatua ya kujinyonga.
Mawazo yatakujia; “Yaani fulani kabisa azini na mke wangu ! Tena fulani ni
rafiki yangu kabisa ! Hapana. Lazima nimkomeshe.”
Hayo yote chanzo chake ni UCHUNU uliouruhusu uingie ndani ya
nafsi (akili) yako. Tumeona Biblia Takatifu inatuambia kwamba: "Uchungu
wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu..." (Efe
4:31) Sasa; je! Nini maana ya neno UCHUNGU? Nivigumu kupambana na adui kama hatumfahamu
adui yetu UCHUNGU ni nani.
UCHUNGU:
Kwa maana nyepesi neno UCHUNGU maana yake ni hii:
Þ Ni hali ya kutokuwa na furaha, kujawa hasira zilizotokana na
kutendewa mabaya.
Þ Ni hali ya kuhisi huzuni nzito ambayo wakati mwingine inaweza
kuchangamana na maumivu makali katika fahamu za mtu, ambayo yaweza kusababisha
mwili kunyong'onyea na kusababisha akili kupoteza uwezo wa kufikiri vizuri.
Mara nyingi UCHUNGU husababisha akili kushindwa kufanya kazi
ipasavyo. Hiyo ndiyo maana halisi ya neno uchungu. Zifuatazo ni athali za
kutosamehe;
MADHARA YA KUTOSAMEHE:
i/: KUHARIBU AFYA YAKO.
Kama nilivyojifunza hapo awali; UCHUNGU husababisha huzuni
nzito. Hii huzuni inapomwingia mtu, huleta maumivu makali katika fahamu za mtu;
Uwezo wa mtu wa kufikiri vizuri hupotea, na wakati mwingine huyu mtu anakuwa kama vile
amedumaa akili. Unaweza hata ukamwuliza: “Jina lako ni nani?” Lakini mtu huyo
badala ya kukujibu akabaki anakushangaa tu.
Uchungu unapomwingia sana mtu unaweza kumfanya apoteze hamu ya kula.
Atahisi kila aina ya chakula kwake ni kibaya, atahisi vyakula vyote kwake
havina radha. Na hata akijilazimisha kula ataona kama chakula ni
kigumu kumezea. Matokeo yake, afya inaanza kuzorota na mwili unaanza
kunyong'onyea. Ndipo chanzo cha madonda ya tumbo. Uchungu utokanao kwa hasira
husababisha mwili uweze kuzalisha sumu ambayo inaleta madhara katika afya yako.
Pia, UCHUNGU husababisha mtu kuwa na
mawazo yenye maswali yasiyo na majibu kwa wepesi; na tena tumaini huonekana kama vile
limepotea kabisa. Uchungu huo ukidumu kwa muda mrefu husababisha mwili
kutengeneza sumu itakayoharibu ule ute mwepesi unaopatikana katikati ya mifupa
(Synovial fluid) pamoja na kuharibu afya yako kwa ujumla (Bila shaka hapa
madaktari wananielewa vizuri.) UCHUNGU huo ukizidi kupita kiasi, mwili wa mtu
huyo huonekana umekakamaa kakamaa sana. Na kwa kiasi kikubwa afya ya mtu
huyu huanza kuharibika hatua baada ya hatua. Mwili wake hunyong'onyea na akili
zake hushindwa kufanya kazi vizuri, hupoteza kumbukumbu na utambuzi wa mambo
mbali mbali na kumfanya mtu afanye maamuzi ya pupa yanayompeleka kwenye hasara
kubwa zaidi badala ya kuleta suluhu la matatizo yake.
Hivyo basi; Athali ya pili ya
KUTOSAMEHE ni kama ifuatavyo:
ii/: KUTENGWA NA WATU.
KUTOKUSAMEHE kunasababisha GHADHABU na HASIRA. Na hivi vyote
hutokea pale unaposhindwa KUUDHIBITI UCHUNGU USIKUTAWALE. Mlango mkubwa wa
DHAMBI huanzia pale mtu anaposhindwa kudhibiti UCHUNGU. Kwa hiyo; UCHUNGU
unapomtawala mtu, uchungu huo unazaa kitu kinachoitwa CHUKI. Ndani ya hii chuki
ndimo kunakaa GHADHABU. GHADHABU ni hali ya mtu kuwa na maamuzi ya pupa pasipo
kujali madhara yake. Hali hiyo yaweza kumfanya mtu kuwa na majibu ya mkato
mkato, kutopenda kuulizwa ulizwa; humfanya mtu kuwa na hali ya UGOMVI mara kwa
mara, kutopenda kuwa na subira (anataka afanyiwe vitu kwa haraka haraka la
sivyo ananuna na kutoa maneno machafu, na wakati mwingine anakuwa na tabia ya
kuzira). Katika hatua hii ndipo kunazaliwa kitu kiitwacho HASIRA. HASIRA
umfanya mtu kuchukua maamuzi pasipo kujali. Mtu huyo kwa wakati huo anakuwa
hatarinisana kuingiliwa na Shetani. Endapo asipodhibiti hiyo hasira
yawezekana Shetani akamwendesha kama jinsi Shetani apendavyo. Hapo
ndipo utaona MAGOMVI, MATUSI na KILA AINA YA UBAYA vinadhihirika kwa mtu huyo.
Tena anafanya pasipo hata kujali. Mtu hukirihusu hasira ikutawale utakuwa
umempa Shetani kibali cha kukutawala. Biblia Takatifu inasema kwamba:
"Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira nyingi; Wala
usiende na mtu wa ghadhabu nyingi; Usije ukajifunza njia zake; Na kujipatia
nafsi yako mtego." (MITHALI 22:24-25).
Mtego huo hutoka kwa Shetani ili akuingize
dhambini. Hivyo basi; matokeo ya hasira ni
KUTENGWA NA WATU. Kwa kuwa mtu huyo hufanya maamuzi bila kutumia akili, hekima
wala busara.
Neno la Mungu linapotuambia: "UCHUNGU WOTE NA GHADHABU NA
HASIRA NA KELELE NA MATUKANO YAONDOKE KWENU, PAMOJA NA KILA NAMNA YA
UBAYA.." Mungu anatutaka vitu hivyo viondoke kwetu kwa ajili ya faida yetu
wenyewe. Lakini ukishindwa kuvidhibiti, matokeo yake utafikia hatua itakayokupa
hasara kimwili na kiroho pia.
Na ufahamu kwamba; MTU KUSHINDWA KUDHIBITI
UCHUNGU USIMTAWALE kunaweza kuwa CHANZO CHA MABAYA NA DHAMBI KUTOKEA. Ndiyo
maana utaweza kuona mtu amegombana na mke wake nyumbani alafu anaondoka na
hasira zake kisha unasikia amegongwa na gari barabarani.
Sasa jiulize, kusamehe
ni kwa ajili ya faida kwa Mungu au kwako wewe mwenyewe? Au yawezekana
umedhurumiwa pesa zako na wafanya biashara wenzako kisha ukaingia ofisini mwako
umejaa hasira, wateja wanapokuja wewe unawajibu vibaya; Je, biashara yako ikifa
utamlaumu Mungu, Shetani au lawama ni juu yako wewe uliyeshindwa KUZUIA HUO
UCHUNGU? Dawa ya kuushinda uchungu ni KUSAMEHE; hakuna tiba nyingine zaidi ya
KUSAME.
Ni kitu cha kushangaza hata watu wadunia wanataka kuwazidi akili baadhi
ya watu wa Mungu. Katika accountance kuna kitu kinaitwa Bad Debt Account. Yaani
ni deni lililoshindikana kulipwa aidha kwa kudhurumiwa au mdeni amekufa au
kufirisika. Wahasibu hufungua account hiyo ambayo ni ishara ya kusamehe deni
lililoshindikana kulipwa, kisha wanafanya mikakati mipya ya kusawazisha pengo hilo.
Sasa je! Kuna tatizo gani linalowafanya watu wa Mungu washindwe KUSAMEHE?
Nikifungua Biblia kwenye kitabu cha WAEFESO 4:26 Biblia inasema:
"Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na
UCHUNGU wenu bado haujawatoka." (Efe 4:26)
Unaona sasa; tatizo kubwa la watu ni kuruhusu UCHUNGU
KUWATAWALA. Tunapoambiwa "MWE NA HASIRA, ILA MSITENDE DHAMBI...” Kumbe
inawezekana kabisa mtu kupatwa na hasira kwa sababu makwazo na majaribu ni
mengi tuyapatayo kila siku, lakini tumeambiwa “MWE NA HASIRA LAKINI MSITENDE
DHAMBI”; na tena tunaambiwa “...JUA LISIZAME TUKIWA BADO NA UCHUNGU NDANI
YETU.” Tunalazimika KUSAMEHE kwa ajili ya faida yetu sisi wenyewe. Ndiyo
maana tukisoma WAEFESO 4:26 imeandikwa: "wala msimpe Ibilisi nafasi."
Hivyo basi, kumbe KUTAWALIWA NA UCHUNGU NI NJIA YA KUMPA
SHETANI NAFASI. Tunaposoma WAEFESO 5:17 tunaona imeandikwa:
"Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo
mapenzi ya Bwana". (Efe 5:17)
Bila shaka hadi hapo nimeeleweka vizuri. Sasa basi; Athali ya
tatu ya KUTOKUSAMEHE ni kama ifuatavyo:
iii/: MUNGU HATAKUSAMEHE DHAMBI ZAKO.
KUTOSAMEHE ni moja ya sababu ya KUTOSAMEHEWA. Neno DHAMBI, lina maana ya
kutenda kinyume na mapenzi ya Mungu. Dhambi ni kuvunja amri/sheria za Mungu.
Mtu atendapo DHAMBI anakuwa haumkosei mwanadamu bali umemkosea Mungu. Hivyo
basi, ni Mungu pekee ndiye awezaye KUKUSAMEHE. Kwa hiyo, Mungu hawezi
kukusamehe wakati wewe hautaki KUSAMEHE wenzako. Neno la Mungu linatuambia
kwamba:
"Nanyi, kila msimamapo na kusali, SAMEHENI, mkiwa na neno
juu ya mtu; ILI NA BABA YENU ALIYE MBINGUNI AWASAMEHE NA NINYI MAKOSA
YENU." (Marko 11:25)
Tukizidi pia kusoma ule mstari wa 26, tunaona Mungu anasisitiza
kwa kusema:
"Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni
hatawasamehe ninyi makosa yenu." (Marko 11:26)
Mungu ametuweka wazi kabisa; ENDAPO
KAMA SISI HATUSAMEHE, VIVYO HIVYO NA SISI HATUTASAMEHEWA. Sasa je! Ni nani
asiyetenda makosa au kumkwaza mwenzake kwa namna yoyote ile? Bila shaka hapa
jawabu ni HAKUNA. Kila mmoja wetu umkwaza mwenzake kwa namna fulani fulani. Kwa
hiyo hatupaswi kuruhusu UCHUNGU ututawale hata kidogo ili Shetani asipate
nafasi ndani yetu. Kwa kuwa sote huwa tunakoseana, ni lazima tusameheane ndipo
na sisi tupate kusamehewa na Mungu.
Madhara mengine ya kutosamehe ni haya
yafuatayo:
iv/: MUNGU HAPOKEI SADAKA ZAKO, NA WALA HAJIBU MAOMBI YAKO.
Nikifungua Biblia Takatifu kwenye kitabu cha MATHAYO 5:23,24
tunaona pameandikwa kwamba:
"Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka
ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu,
uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako."
Mungu huchukizwa na sadaka za mwenye dhambi. Sadaka za mtu
mwenye dhambi hazipokelewi mbele za Mungu. Ndiyo maana imeandikwa kuwa utii ni
bora kuliko dhabihu. Mungu si masikini hata ababaishwe kwa sadaka zako.
Tukisoma kitabu cha HOSEA 6:6 Mungu anasema:
"Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu
kuliko sadaka...",
Mungu hababaishwi na hako kasadaka kako. Mungu si masikini hadi
ababaishwe na uto tusadaka twako. Mungu anapenda sadaka za mtu mwenye moyo safi;
Ndiyo maana Biblia inasema kwenye MITHALI 21:3
"Kutenda haki na hukumu humpendeza BWANA kuliko kutoa
sadaka." (Mithali 21:3)
Mungu hupendezwa na moyo safi; ndiyo maana amesema
"...IACHE SADAKA YAKO MBELE YA MADHABAHU, UENDE ZAKO, UPATANE KWANZA NA
NDUGU YAKO, KISHA URUDI UITOE SADAKA YAKO." Kwahiyo, usipopatana
(sameheana) na yule mliyekoseana, hakika Mungu hatapokea sadaka zako. Hivyo
basi, KUTOSAMEHE umfanya mtu kukosa kibali mbele za Mungu. Naunapokosa kibali
kwa Mungu maana yake unakuwa haujampendeza Mungu, vivyo hivyo kwa maana nyepesi
unakuwa umetenda dhambi, kwa maana dhambi ni kutenda kinyume na mapenzi ya
Mungu.
Hivyo basi, ninapenda kuhitimisha somo hili kama ifuatavyo;
Biblia inasema kwenye kitabu cha WAEFESO 6:10,12
"Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza
wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za
Shetani."
Ninajua wapo watu ambao watauliza; Je, silaha za Mungu ni zipi?
Silaha kubwa kabisa kuliko zote ni NENO LA MUNGU lililomo ndani
ya Biblia Takatifu; neno hilo la Mungu linapaswa kukaa kwa wingi
ndani yako. Neno la Mungu likikaa kwa wingi ndani yako, ukilifanyia kazi na
kulishika, ndipo Roho Mtakatifu atakaa ndani yako na kukuongoza namna ya
kufanya. Pasipo Neno la Mungu, hatuwezi kuyajua mapenzi ya Mungu. Kwahiyo,
silaha kuu ni NENO LA MUNGU. Ndiyo maana tukisoma WAEFESO 6:14-17 imeandikwa:
"Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa
dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;
zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale
yote yenye moto ya yule mwovu..."
Sasa soma hapa kwa makini zaidi, "...Tena ipokeeni chapeo
ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu."
Siku zote Shetani anataka kuona watu wanapotea na kukosa baraka
za Mungu. Shetani analeta majaribu na makwazo mbalimbali ili watu waanguke na
kuiacha njia ya uzima; Shetani anataka watu wawe na uchungu ili wakose baraka
za Mungu. Hauwezi kusema umemsamehe mtu wakati bado unao uchungu moyoni mwako.
Biblia inasema hakuna dhambi ndogo wala dhambi kubwa, ni kwa sababu muongo na
muuaji wote hukumu yao ni kutupwa kwenye ziwa la moto na kupata humo
mateso ya milele yote. Vivyo hivyo yeye asiyesamehe wenzake hukumu yake ni ile
ile kwenye ziwa la moto sawa sawa na muuaji.
Nikisoma WAEFESO 6:12 imeandikwa
"Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama;
bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya
majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."
Ndugu zangu tuweni macho na makini sana, Shetani hapendi
kuona watu wanabarikiwa, hapendi kuona kazi ya Mungu inasonga mbele, na hapendi
kuona watu wanarithi uzima wa milele. SAMEHEANENI NA WALA UCHUNGU USIKAE
MIOYONI MWENU. Mwenyezi Mungu awabariki nyote mnaotendea kazi haya mliyojifunza
humu. Roho Mtakatifu awaongoze kwenye kweli yote, mbarikiwe katika jina la Yesu
Kristo. Amina.
Post A Comment:
0 comments so far,add yours