Nawasalimu kwa jina la Yesu . Leo
katika nyanja hii ya vijana, nimeona ni vema tukashirikishana kuhusu suala la ‘kufikiri
kabla ya kuoa au kuolewa’.
Siku moja katika kusoma Biblia
nilikutana na mstari ufuatao, nakusahuri uusome kwa umakini. Biblia katika 1Wakorinto
7:8-9 inasema “Lakini nawaambia wale, wasiooa bado na wajane, Ni
heri wakae kama mimi nilivyo, lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni
afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa”.
Baada ya kuusoma mstari huu niliingia
katika tafakuri nzito sana ambayo mwishowe ilinipeleka kuandaa somo hili,
kwamba ni vema ukafikiri vizuri kabla ya kuchuka uamuzi wa kuoa au kuolewa.
Unajua malezi, dini, madhehebu yetu,
wazazi, mila na desturi vinachangia kwa kiwango kikubwa sana kuhusu utaratibu
wa kuanzia mtu kupata mke au mume mpaka watakapofunga ndoa. Kila kundi lina
mfumo na utaratibu wake ambao lingependa vijana waufuate ili kuhakikisha wanaoa
na kuolewa kwa kile ambacho kila kundi linaona na kuamini kwamba huo ndio
uataratibu mzuri kufuatwa.
Namshukuru Mungu kwa kuwa nami nimeoa,
ingawa vitu vingi sana Bwana alikuwa ananifundisha vinavyohusu ndoa hata kabla
sijaoa. Nakubaliana na dhana kwamba ili uweze kuwa Mwalimu mzuri kwenye nyanja
fulani basi ni lazima au ni vema wewe mwenyewe ukawa umepitia kwanza kwenye
nyanja hiyo. Lengo ikiwa sio tu ufundishe ‘theory’ bali pia utufundishe na
uzoefu wako binafsi kwenye eneo hilo. Licha ya kukubaliana na dhana hii, kwangu
binafsi haikuwa hivyo, maana kuna mambo mengi ambayo, Bwana Yesu, alikuwa
ananifundisha yanayohusu ndoa hata kabla sijaoa.
Kwa kifupi ndoa ni shule au darasa
ambalo wanandoa wanatakiwa kukaa chini na kujifunza kila siku namna ya kuishi
humo ndani ili kuweza kuishi maisha ambayo Mungu amewakusudia.
Kutokana na mifumo ya baadhi ya
makanisa yetu, si vijana wengi ambao wanafundishwa kwa undani kuhusu maamuzi
haya makubwa. Wengi wao wameingia kimwili na kujikuta wakijutia na kulaumu kwa
nini nilimuoa au kuolewa na huyu kijana. Nasema haya kwa kuwa nimekutana
na wanandoa wengi wa aina hii, na nataka nikuambie kama Biblia ingetoa mwanya
wa wanandoa kuachana na kuoa au kuolewa na mtu mwingine, wapendwa wengi sana
walioko kwenye ndoa wangefanya hivyo na wengine wasingekubali kuolewa au kuoa
tena.
Unajua kwa nini?
Ni kwa sababu si vijana wengi wenye
ufahamu wa kutosha juu ya aina ya maamuzi wanayotaka kuyachukua. Kwa hiyo
katika somo hili nimeona vema niandike mambo manne ya msingi ambayo naamini
yataongeza na kupanua ufahamu wako ili kukusaidia kufikiri kwanza kabla ya
kufanya maamuzi haya makubwa;
- Si
kila ndoa inayofungwa imeunganishwa na Mungu, kwa kuwa ndoa ni kiungo cha
muhimu kwa Mungu na Shetani pia.
Kuanzia mwaka 2005, Mungu alinipa
kibali cha kuanza kufundisha na pia kushauri juu ya mambo kadhaa kuhusu
wanandoa. Tangu wakati huo hadi sasa nimekutana na baadhi ya wanandoa ambao
wanajuta kwa nini walikubali kuoa au kuolewa. Wanaishi kwenye ndoa kwa sababu
tu ya watoto na pia kwa hofu kwamba endapo kama wataachana jamii na watu
wanaowazunguka hawatawaelewa.
Ni vizuri ukafahamu kwamba si kila
ndoa inayofungwa ni ya mapenzi ya Mungu, hata kama imefungwa kanisani. Biblia
inaposema kilichounganishwa na Mungu, mwanadamu asikitenganishe, katika nafasi
ya kwanza maana yake iwe ndoa ambayo Mungu ndiyo aliyehusika katika kuanzisha
mahusiano na kuwaongoza hao watu kuishi pamoja. Wakati Mungu anatafuta
kuhakikisha watu wake wanaoana katika mapenzi yake na Shetani naye anapambana
kuhakikisha watu wanaoana katika hila (mapenzi) zake.
Shetani amefanikiwa kwa kiwango kikubwa
sana kuvuruga wanandoa wengi na kuwafanya waishi maisha tofauti na yale ambayo
Mungu aliwakusudia. Ni kwa sababu hii ndio maana Paulo aliwaambia Wakorinto
‘Lakini nawaambia wale, wasiooa bado na wajane, Ni heri wakae kama mimi
nilivyo, lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni afadhali kuoa
kuliko kuwaka tamaa’. Paulo aliona shida, maudhi ya wandugu walioko kwenye ndoa
tokana na migogoro aliyokuwa akikutana nayo.
Fahamu kwamba ni furaha kubwa kwenye
ufalme wa giza mtu anapooa au kuolewa kinyume cha mapenzi ya Mungu. Hii ni kwa
sababu Shetani anajua akifanikiwa kukushawishi ukaoa kinyume na mapenzi ya
Mungu, ameharibu ‘future’ yako na kile ambacho Mungu alikusudia ukifanye hapa
duniani. Kumbuka suala sio kuoa au kuolewa tu, bali ni kuingia kwenye ndoa
ambayo itakuwezesha kulitumika shauri la Bwana katika kizazi chako. Hivyo kabla
hujaamua nani uishi naye hakikisha unamshirikisha Mungu akuongoze kumpata
mwenzi sahihi.
- Unapaswa
kuoa au kulewa katika mapenzi ya Mungu
Naam kuoa au kuolewa katika mapenzi ya
Mungu ni changamoto nyingine kubwa kwa vijana wa kizazi cha leo. Naam hili ni
eneo ambalo Mungu yupo makini sana kufuatilia nani atakuwa mwenzi wako wa
maisha. Na upande wa pili nao, Shetani anapigana kwa juhudi kubwa ili kuvuruga
kusudi la Mungu kupitia mtu au watu.
Ni vizuri ukafahamu kwamba
unapotaka kufanya maamuzi ya kutaka kuoa au kuolewa, Shetani naye ataleta
mawazo (mapenzi) yake ndani yako juu ya nani anafaa zaidi kuwa mwenzi
wako maisha. Lengo lake ni kuhakikisha anakuunganisha na mtu ambaye anajua
kwa huyo atakumaliza kiroho na kihuduma kabisa. Suala sio kuwazuia msiende
kanisani, bali ni kuhakikisha kile ambacho ungefanya kwa kuwa na mtu sahihi
hakifanikiwi. Ukitaka kujua ukweli wa jambo hili, muulize Mchungaji wako, kesi
nyingi anazokutana nazo kanisani kwake zinahusu nini, naamini atakujibu
kimapana. Ni jukumu lako kuwa makini kufuatilia unatii wazo la nani, Mungu au
Shetani?
- Vigezo
vya kimwili ni silaha kubwa ya uharibifu
Vigezo vya kimwili ni moja ya silaha
kubwa ambazo Shetani anazitumia kuwavuruga watu wengi waweze kuoa au kuolewa
nje ya mapenzi ya Mungu kwao. Jifunze kufukiri na kutafsiri mambo au makusudi
kama Mungu anavyotazama na kutafsiri. Na uwezo wa kufanya hili utaupata kwenye
neno lake tu. Kwako mwanaume Mungu anapokupa mke anakupa Mlinzi na msaidizi. Na
kwa mwanamke Mungu anakuwa amekupa kichwa. Ni muhimu sana kuchunga ni msaidizi,
mlinzi au kichwa gani unataka kiunganishwe na maisha yako kwa njia ya ndoa.
- Ndoa
ni wajibu mkubwa
Ndani ya ndoa kuna wajibu mkubwa sana
unaokusubiri kama baba au mama. Ndani ya ndoa muda na uhuru wako unabanwa na
mwenzi wako. Ndoa inabana pia muda wa kuwa na Mungu wako. Na kwa wengi kwa
kutaka kuwapendeza zaidi waume au wake zao, wamefarakana na Mungu, kwa sababu
wamewapa waume au wake zao hata nafasi na muda wa Mungu kwenye maisha yao.
Usiingie ndani ya ndoa kwa fikra za
uapnde mmoja. Naam ndoa ni wito wa mapungufu na uvumilivu ambao ni lazima uwe
tayari kuchukuliana na mwenzi wako katika mapungufu yake. Kuna vitu hamtaweza
kufanana na kwa sababu ya mapungufu yaliyopo kwa kila mmoja unapaswa
kutafakari kuhusu majukumu yanayokuja kwako kama mwanandoa, hekima na busara
katika kuzikabili changamoto za ndoa, kama vile kuzaa au kutokuzaa,
kutokujiweza katika masuala ya unyumba, matumizi ya fedha, tabia za mwenzi wako
nk.
Haya ni mambo ya kuhakikisha
unayaombea mapema ili kujenga msingi imara utakapoingia kwenye ndoa yako.
Lakini nikutie moyo kwamba endapo utaoa au kuolewa katika mapenzi ya Mungu,
yeye ni mwaminifu, atakuunganisha na mtu ambaye katika changamoto mtakazokutana
nazo hazitawakwamisha wala kuwafanya mjute. Bali endapo Shetani ndiye ataongoza
maamuzi yako, ni majuto makubwa sana (asomaye na afahamu).
Mungu akubariki, naamini ujumbe huu
umeongezea mambo ya kutafakari na kuzingatia kabla ya kufanya uamuzi wa kuoa au
kuolewa.
Post A Comment:
0 comments so far,add yours