Paulo anafundisha: ‘Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.’ (Waefeso 6:10-12).

Kwa hiyo, ndugu zangu, tufanyaje? Tuombe dhidi ya ‘falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.’? Hapana! Paulo hasemi hivyo! Kwa kweli. Hakuna mahali mmoja katika Biblia ambapo tunasoma kwamba hata muumini mmoja katika maombi yake anaomba juu ya shetani, falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, na juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Hata Danieli hakuomba juu ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho, yeye aliomba kwa ajili ya kazi ya Mungu na watu wa Mungu tu! (Soma Danieli 10. Yule aliyeongea na Danieli alimjulisha kuhusu vita vya kipekee juu ya mkuu wa ufalme wa Uajemi na kuhusu msaada wa Mikaeli, lakini Danieli mwenyewe hakuwa ameomba juu ya mambo haya na wala hakutaja mambo haya katika maombi yake!)

Kwa kweli Bwana Yesu alitoa pepo na hivyo watumishi wake wanaweza kufanya hivyo. Hilo ni jambo jingine kabisa! Lakini hamna hata mstari mmoja ambao unafundisha tuombe dhidi ya ‘falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho’ na wala hamna mfano hata mmojawapo wa muumini aliyewahi kufanya hivyo. Sasa fundisho la mtume Paulo ni lipi juu ya ‘kushindana kwetu’? Anasema:

‘Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu…’ Kwa nini anasema hivyo? Je, ili tupate kuomba dhidi ya ‘falme na mamlala? Hapana!  Paulo anaendelea kueleza, ili ‘mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi SIMAMENI, hali mmejifunga KWELI viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa roho ambao ni neno la Mungu.’ Mafundisho ya Paulo juu ya ‘vita vya kiroho’ inahusu mwenendo wetu wa kiroho, yaani, jinsi ya kusimama katika haki na imani! Kama Yakobo pia anafundisha, ‘Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.’ (Yak.4:7).
 Pia na kama Paulo anafundisha kwenye 2 Wakor.10:3-5, ‘Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;’ Unaona? Vita vyo kiroho kwa msingi vinahusu ‘kuangusha’ mawazo ambayo shetani anataka kuchochea moyoni mwetu yajiinuayo juu ya elimu ya Mungu! Ili kupinga hayo, Paulo anasema ‘silaha za vita vyetu zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome’. Silaha hizo zinazingatia, ‘ngao ya imani’ na ‘upanga wa Roho’.

Tukisimama imara kwa imani katika Bwana ndipo tunaweza kuomba. Je, tuombe dhidi ya falme na mamlaka nkd? Hapana! Paulo anafundisha kwa wazi, ‘kudumu katika kuwaombea watakatifu wote…’. Basi, anafundisha tusimame imara katika Bwana ili tuweze kuomba kwa ajili ya WATAKATIFU wote – yaani, kwa waumini wote katika Kristo – na kwa ajili ya kazi ya Mungu.

Je, ni Paulo tu anayetufundisha tuwaombeeni watakatifu wote? Hapana.

Yesu aliomba, “Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako.” Kumbe! Mzigo wa Bwana Yesu katika maombi yake ulikuwa (na unaendelea kuwa) kwa ajili ya watu wake, kwa ajili ya watakatifu! Alisema kwa wazi, “siombei ulimwenguni”. Je, Bwana Yesu aliwaombea wengine? Ndiyo.  “Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao (Yoh. 17:9,20,21). Aliwaombea waumini na wao watakaoamini! Je, katika maombi yetu, tunaongozwa na Neno la Mungu, na Roho Mtakatifu?

Unaona? Bwana Yesu hamshambulii shetani kwa maneno katika maombi Yake! Yesu alijaribiwa na shetani jangwani kwa siku arobaini. Sasa, ni muhimu sana kuelewa yale yaliyoyaandikwa kwa wazi wakati Yesu alipokuwepo jangwani.
Shetani alipokuja kumjaribu Yesu, ni wazi Bwana Yesu hakujaribu ‘kufunga’ nguvu za shetani; Yesu hakupaza sauti yake au kupiga kelele ili kumfukuza shetani atoke jangwani! Hapana! Aliishi, alisimama kwa Neno la Mungu tu! Shetani alikuja kuchochea kutokuamini juu ya upendo wa Mungu na uwezo wa Mungu mioyoni mwetu kwa maneno kama haya: ‘Je, Mungu wako yupo wapi? Je, anakupenda kwa kweli? Kwa nini Mungu alikuacha katika mahitaji yako? Angalia mazingira yako na niambie uwezo wa Mungu upo wapi? Kama wewe ni Mwana wa Mungu, fanya hivi au hivi!’ Ibilisi alikuja kwake Yesu na alitaka kuchochea mawazo kama hayo, na ibilisi atakuja kwako na mawazo hayo kuchochea kutokuamini ili usiamini upendo na uwezo wa Mungu. Hivyo ni vita vya kiroho! Tufanye nini katika vita vya kiroho? Na tufanye vile vile Yesu alivyofanya! Alisimama kwa Neno la Mungu!

“Imeandikwa….imeandikwa……imeandikwa!” ‘Upanga wa Roho’ haimaanishi kupiga kelele na kumshambulia shetani kwa hasira na maneno ya kumfukuza aondoke! Yesu hakufanya hivyo. Aliishi kwa neno la Mungu, ‘Imeandikwa, mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu’.

Lakini katika maombi Yake, Yesu anawaombea watu wa Mungu, kama ilivyoandikwa,

“Kwa hiyo anaweza kuwaokoa kabisa wale wanaomjia Mungu kupitia Kwake, kwa sababu Yeye ADUMU DAIMA KUOMBA KWA AJILI YAO.” (Waebr.7:25). Sikiliza juu ya huduma ya Yesu Kristo,

“Kristo Yesu ndiye aliyekufa, naam, zaidi ya hayo, ndiye aliyefufuka kutoka kwa wafu, YUKO MKONO WA KUUME WA MUNGU, NAYE NDIYE ANAYETUOMBEA.” (Warumi 8:34).

Kuhani mkuu katika Agano la Kale alibeba nini mabegani na kifuani mwake? Mungu aliagiza…

“Chukua mawe mawili ya shohamu na uchore juu yake majina ya wana wa Israeli, kufuatana na walivyozaliwa, majina sita katika jiwe moja na mengine sita katika jiwe jingine. Yachore majina ya wana wa Israeli juu ya hayo mawe mawili kama vile sonara anavyochonga mhuri. Kisha uyatie hayo mawe katika vijalizo vya dhahabu na uvifungie juu ya vipande vya mabega ya kisibau yawe kama mawe ya kumbukumbu ya wana wa Israeli. Aroni atavaa majina hayo mabegani mwake kama kumbukumbu mbele za BWANA.”

“Fanyiza kifuko cha kifuani kwa ajili ya kufanya maamuzi, kazi ya fundi stadi. Kitengeneze kama kile kisibau: cha nyuzi za dhahabu, buluu, za zambarau na za rangi nyekundu, cha kitani safi iliyosokotwa. Yote yatiwe kwenye vijalizo vya dhahabu. Patakuwa na mawe kumi na mawili, moja kwa kila jina la wana wa Israeli, kila moja lichorwe kama muhuri likiwa na jina la moja ya makabila kumi na mawili ya Israeli….Wakati wo wote Aroni aingiapo Mahali Patakatifu, atakuwa na yale majina ya wana wa Israeli moyoni mwake juu ya kile kifuko cha kifuani cha uamuzi kama kumbukumbu ya kudumu mbele ya BWANA. (Kutoka 28:9-29).

Unaona, kwa maagizo ya Mungu, kuhani mkuu alibeba jina la watu wa Mungu mabegani na kifuani mbele ya Mungu wakati wote! Aidha, Mungu aliagiza wachore majina ya watu wa Israeli juu ya vito VYA THAMANI sana! Kuhani mkuu alibeba watu wa Mungu karibu sana kwa moyo wake! Aliwabeba mabegani mwake. Sasa, Yesu ni kuhani mkuu wetu! Sisi tu wa thamani Kwake! Anatubeba karibu na moyo Wake na anatuombea mbele ya Mungu! Jambo la ajabu! Inaonekanaje kwako na kwangu katika maisha ya maombi yetu?

Zaidi ya hayo tunaona kwamba Roho Mtakatifu anatuombea,

“Kadhalika… Roho mwenyewe HUTUOMBEA kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa HUWAOMBEA WATAKATIFU kama apendavyo Mungu.” (Warumi 8:26,27).

Kumbe! Roho Mtakatifu alituongoza kuwaombea watakatifu, yaani, waumini, watu wa Mungu.

Na sisi, katika maombi yetu na katika ‘vita vya kiroho’, je, tunaelekezwa kuombe kwa ajili ya nini au nani? Neno la Mungu husema kwa wazi, “kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika KUWAOMBEA WATAKATIFU WOTE.”(Waefeso 6:18).

Tunapaswa kuwaombea wataktifu wote katika Roho. Je, mtume Paulo aliomba kwa ajili ya watakatifu? Ndiyo. “Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo, SIKU ZOTE TUKIWAOMBEA…Kwa sababu hiyo sisi nasi, … HATUACHI kufanya maombi na dua KWA AJILI YENU, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni.” (Wakol.1:3, 9).

Ni wazi tunaweza na tunapaswa kuomba kwa ajili ya mambo mengine, kwa mfano:

“Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka…” Kwa nini? Paulo anatujulisha, “tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu.” (1 Tim.2:1,2).

Paulo aliwaombea ndugu zake kwa jinsi ya mwili, yaani, Wayahudi, ili waokolewe, “Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe.” (Warumi 10:1). Ni wazi tunaweza kuwaombea wengine ili waokolewe.

Ni vema kuomba kwa ajili ya kazi ya Mungu na kwa ajili ya watumishi Wake,

“Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu.” (2Wathes.3:1)

“Mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo.” (Wakol.4:3)

Yesu anawaombea waumini. Roho Mtakatifu anawaombea waumini. Paulo aliwaombea waumini sikuzote. Na sisi tumeambiwa kuwaombea watakatifu kila wakati katika Roho. Kwa ujumla, haya ni mafundisho hasa ya Agano Jipya na yanawakilisha mzigo wa maombi ya watakatifu. Pamoja na hayo tunafundishwa kuomba kwa ajili ya kazi ya Mungu na watumishi Wake pia ili wengine waokolewe.

Sasa, tunaongozwa na nini katika maombi yetu? Kwa neno la Mungu? Kwa Roho Mtakatifu? Au kwa habari ya magazeti, redio na televisheni? Au inatupendeza kuomba dhidi ya ‘falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.’? Lakini Paulo hufundisha kwamba siyo jambo kusali dhidi ya mambo haya – ni jambo kusimama kwa imani na haki wakati shetani anapojaribu kutuangusha katika maisha ya kiroho yetu. Tusimame imara katika imani ILI TUWEZE KUWAOMBEA WATU WA MUNGU!

——————————————————————————-

“Sala zako na sadaka zako kwa wahitaji zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.” (Mat.10:2-4)

 Maneno ya ajabu! Ungependa kuwa na ushuhuda kama huo mbele ya Mungu? Malaika alisema maneno haya kwake Kornelio ambaye alikuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia. Kornelio hakuwa mhubiri wala mtume wala mchungaji wala nabii wala mwinjilisti! Alikuwa mtu wa kawaida tu. Alikuwa na kazi na familia. Kama jemadari hakika alikuwa na majukumu na shughuli nyingi! Lakini alimwomba Mungu daima! Alichukua muda kuwa peke yake kuomba mbele ya Mungu. Mambo ya kila siku hayakumzuia kwenda mbele ya Mungu kuomba!

Kornelio hakujulikana ulimwenguni lakini alijulikana mbinguni! Ni bora kabisa kujulikana mbinguni kuliko duniani! Je, tunapendelea tujulikane mbele ya watu, duniani, au tujulikane mbinguni, mbele ya Mungu? Usijibu kwa haraka swali hili! Usijibu ovyoovyo! Bali, tunavyoishi ni jibu!

Je, ninajitenga mwenyewe na wengine kwa ajili ya hamu yangu niwe na Mungu tu? Je, kwa kusudi na kwa mkazo tunachukua muda kuwa peke yetu pamoja na Mungu? Je, na tunafanya hivyo siyo kana kwamba ni jambo la kulazimishwa, lakini kwa sababu tumampenda Bwana na astahili tuutafute uso Wake na tujitoe maisha yetu! Je, kwa makusudi na kwa mkazo tunachukua muda kumwomba Mungu kupitia Yesu Kristo kwa ajili ya watu wake na kazi yake? Na je, tunasema sala kana kwamba ingekuwa orodha ya mahitji tu? Au tunao uhusiano na Mungu wa kina, na maombi na maneno yetu mbele ya Mungu yanatokana na uhusiano huo huo? Je, tunachukua muda kujitenga na mambo yote ya ulimwengu huo ili kumwabudu Mungu, kumpenda tu, kumsifu tu, bila kutafuta kitu kingine cho chote kwa ajili yetu? Je, unachoshwa kuwa na Bwana hata nusu saa? Kama tunakwenda mbele ya Bwana kuomba kwa ajili ya mahitaji tu, basi tutakuwa hatuelewi vizuri tabia ya wokovu wetu katika Kristo Yesu. Watu wengi sana hupenda kuimba kanisani na kuongoza sifa na ibada. Siyo nidyo, jamani? Sasa je, unamsifu Bwana na kumsujudu peke yako mahali pa siri ya maisha yako pia? Kama hapana, kwa nini? ‘Mahali pa siri’ ni kwa mfano chumba chako, au porini, au bustani. Haidhuru. Muhimu ni mahali ambapo upo peke yako mbele ya Mwokozi wako tu – mbele ya macho ya Mungu na siyo ya watu!

Kwa msingi thamani ya maisha yangu hayatokani na jinsi nilivyo au jinsi naishavyo mbele ya watu! Bali yanatokana na jinsi nilivyo na jinsi naishavyo mbele ya Mungu, mahali pa siri ya maisha yangu ambapo Mungu tu ananiona! “Sala zako… zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.” Kama ukipenda kuwa mtu wa Mungu kweli kweli, lazima uwe na ‘mahali pa siri’ katika maisha yako ya kila siku – pale ambapo Mungu tu anakuona, pale ambapo unamtumikia Mungu tu, peke yako, ambapo hakuna mtu ye yote mwingine akuonaye au ajuaye unalofanya kwa siri! (Mtt.6:4-7; 16-18).

Kwa upande moja, tufanyalo kwa siri ni muhumiu kuliko tufanyalo mbele ya watu! Tunafanyeje kwa siri katika maisha yetu? Je, tunamngojea Mungu, tunautafuta Uso Wake, tumsifu, tumpende, tumsujudu na kumwomba kwa ajili ya watu wake na kazi yake? Je, tunatafuta ile sifa itokayo kwa Mungu na siyo kwa watu? Je, tunajitoa maisha yetu kwake mahali pa siri ili tuwe bila hasira, uchungu, wivu, chuki, malalamiko na manung’nuniko na badaka yake tuwe harufu nzuri ya manukato ya Kristo mbele ya Mungu? (2 Wakor.2:15).

“Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu.” (Ufunuo 5:8). Biblia inatufundisha kwamba maombi yetu ni kama uvumba mbele Kiti cha Enzi! Huo ndio ukweli wa maana sana! Hebu tufikiri ukweli huo ili uchochee mioyo yetu tuombe!  Kumbuka, malaika alisema, “Sala zako na sadaka zako kwa wahitaji zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.”

Unafanya nini kwa siri? Unaangalia nini kwa siri? Unafanya mambo yale ambayo yakusababishe ukue katika Kristo, katika utakatifu, katika imani na katika maisha ya maombi – au mambo yale  yanayoharibu maisha yako ya kiroho na hata ya mwili? Maisha yetu ya siri, yaani faraghani, lazima yawe matakatifu.

Wahubiri na wachungaji wengine hupaza sauti sana wanapohubiri wakifikiri hiyo inawakilisha nguvu ya Bwana! Hapana. Wengi kwa sababu ya upungufu wa nguvu ya kiroho katika huduma yao wanapiga kelele wanapohubiri! Nguvu ya huduma yetu inatokana na mahali pa siri (mbele ya Mungu) katika maisha yetu! Ni kweli, huduma inategemea na mwito pia, lakini hata hivyo ni lazima kujitenga kwa ajili ya mwito huo kama Petro alivyosema, “sisi tutatumia muda wetu mrefu kuomba na kulihudumia lile neno.’’ (Mat.6:4).

Na hata mtume Paulo hakupiga mbio kufanya kazi ya Mungu kwa maono yake yenyewe! Alitumikia Bwana kwanza na kuwatumikia watu wa Mungu kanisani kabla ya kwenda kufanya kazi ya mtume! Matendo 13:1,2 inatufundisha jambo la maana sana:

“Katika kanisa huko Antiokia ya Shamu walikuwako manabii na walimu, yaani: Barnaba …na Sauli. Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalumu niliyowaitia.”

Unaona, Paulo hakujitukuza wala hakutazamia watu wamtambue au kumpokea kama mtume muhimu! Alikataa kufanya mapenzi yake yenyewe, na alikataa kufanya kazi ya Mungu kutokana na hamu yake, akili yake au uwezo wake wenyewe. Alibaki kwa unyenyekevu katika kanisa moja kuwahudumia watu wa Mungu, lakini msingi wa maisha yake ulikuwa kuchukua muda kumwabadu Bwana na kufunga mbele Yake mpaka Mungu Mwenyewe alimwita kufanya kazi ya mtume! Hamna watu wa Mungu wengi kama Paulo! Wengine wamalizapo Shule ye Biblia wanafikiri wametayarishwa kufanya huduma ya mchungaji. Hilo ni wazo lisilo na maana! Shule ya Biblia ya kweli ni MAISHA. Ni lazima kujifunza njia za Bwana katika maisha ya kila siku! Wachungaji na wahuburi kadhaa (au hata wengi) hawana kitu cha kiroho kuwaambia washirika kwa sababu wanakosa kuchukua muda kuwa peke yao mbele ya Bwana –  “sisi tutatumia muda wetu mrefu kuomba na kulihudumia lile neno.” Kanisa ambalo linao mchungaji wa namna hiyo, hubarikiwa! Watu kama hawa wanawalisha watu wa Mungu na maneno ambayo wanayoyapata kutoka kwake Bwana wakati wanaposali mbele Yake na kuutafuta uso Wake! Wanajitoa kabisa kwake Bwana na wanamngojea. Wengine wanahubiri mawazo ya kibinadamu tu au mambo mapya yanayotoka Ulaya au Amerika! Wanachukua muda kujenga huduma yao badala ya kumtafuta kwenye mahali pa siri.

Kwa sababu mtume Paulo aliishi maisha yake mbele ya Bwana na siyo mbele ya watu, kumbe, alijulikana mbinguni na hata katika ulimwenguni wa kiroho. Tunasoma, “Basi baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga huku na huko wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Yesu juu ya wale wenye pepo, walikuwa wakisema, ‘Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, na kuamuru utoke.’ Palikuwa na wana saba wa mtu mmoja Myahudi jina lake Skewa, aliyekuwa kiongozi wa makuhani, ambao walikuwa wanafanya hivyo. Lakini pepo mchafu akawajibu, ‘Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani? Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote …”. (Mat.19:13-16). Tunaona watu wanatumia jina la Bwana bila kumjua Yesu. Paulo alijulikana na Mungu, alijulikana na pepo, na alijulikana na watu! Kama tunafanya kazi ya Mungu ni lazima tujitenge na mambo ya kila siku na kuchukue muda kuwa mbele ya Bwana tujitoeeni kwake katika maombi na kumwabudu, na siyo kujaribu kutimiza ‘maono’ au ‘ndoto’ zetu wenyewe!

“Kornelio Yeye alikuwa mcha Mungu pamoja na wote wa nyumbani mwake, aliwapa watu sadaka nyingi na kumwomba Mungu daima. Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono wazi wazi malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!” Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?”


“Sala zako na sadaka zako kwa wahitaji zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.”  (Mat.10:2-4


Share To:
Magpress

Calvin Petro

Kwa Moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na Maagizo yako. Moyoni mwangu nimeliweka Neno lako Nisije nikakutenda dhambi. (Zaburi 119:10-11).

Post A Comment:

0 comments so far,add yours