Je, unafikiri mume au mke wako ni mgumu kuishi naye? Je, unamcha mungu kuliko kujipendeza mwenyewe? Abigaili hakuwa na kanisa. Abigaili hakuwa na Biblia. Abigaili hakuwa amebatizwa na Roho Mtakatifu. Lakini basi kinyume chake, Abigaili alikuwa na mume tu aliyekuwa hana adabu, tena mwovu, tena mkorofi, aliyeitwa Nabali.

Lakini Abigaili ALIMCHA Mungu. Na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso.

Katika 1 Samweli 25 tunasoma juu ya Nabali. Kondoo na mbuzi wa Nabali walikuwa na usalama wakati wote walipokaa chini ya ulinzi wa watumishi wa Daudi. Baadaye Daudi alipoomba Nabali awape watumishi wake msaada wa vyakula, Nabali akawatukana tu. Mara moja Daudi aliamua kumwua Nabali – lakini mtumishi mmoja wa Nabali aliweza kumwambia Abigaili mambo hayo.

Alifanyaje Abigaili? Je, alifurahia tukio hilo? Je, aliwaza, “Hii sasa ni fursa yangu kwa Mungu ya kuniondoa toka kwa mume huyu! Sasa nitakuwa huru kutokana na mume huyu mkorofi! Bado mimi ni mrembo – kwa nini niolewe na mume kama huyu? Abigaili alifanyaje sasa ili awe huru kutokana na mume wake mwovu? Hakuna chochote! Yeye hakupaswa kusema wala kufanya lolote lile! Yeye angeweza kutulia TU pale na kumwacha Daudi aje pamoja na watu wake kumwua mumewe Nabali! Na wewe ungefanyaje?

Lakini Abigaili ALIMCHA Mungu! Hakujipendeza. Hakujitumikia. Alitaka kumpendeza Mungu na kumtumikia! Hakujifikiria yeye mwenyewe, au ajiokoe mwenyewe kutokana na hali hiyo ngumu. Hapana. Yeye alifikiria tu kumsaidia Daudi asilete hukumu juu yake kwa kujilipiza kisasi mwenyewe na kumwua mumewe. Alimwamini Mungu. Kwa hiyo alinyenyekea chini ya mikono ya Mungu na hakufikiri juu ya faraja yake mwenyewe au hali yake ngumu wala hakutafuta njia ya kutoroka kutoka katika mazingira yake ngumu. Na wewe?

Aliamini kuwa kila kitu kilikuwa mikononi mwake Mungu, na kwamba iwapo mumewe inampasa kufa, basi huo ulikuwa ni wakati wake Mungu mwenyewe na wala sio kwa mkono wa mwanadamu.

Hivyo Abigaili alifanyaje? Yeye aliandaa zawadi ya vyakula kwa ajili ya Daudi na hao watu wake Daudi alioandamana nao. Abigael akaondoka na kumfuatilia Daudi hukohuko njiani, “Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, … akainama mpaka nchi. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, JUU YANGU MIMI NA UWE UOVU; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.”

Kumbe, Abigaili alikuwa yu radhi kuyatoa maisha yake kwa ajili ya mumewe mwovu! Kwa kuwa alimwamini Mungu, alitaka kumwokoa mumewe, na pia Daudi mwenyewe kutokana na hali ya kujilipiza kisasi. Abigaili hakujitafutia mlango au njia ya kutoka ili awe huru kutokana kwa mumewe mwovu. Na wewe?

Aliamini kuwa kila kitu kilikuwa mikononi mwake Mungu. Ndoa yake ili kuwa mikononi mwa Mungu. Na alikataa kufanya cho chote kubadilisha hali hiyo ya maisha yake!

Je, mumeo au mkeo ni mtu mgumu sana hata unafikiri ungeshindwa kuendelea kuishi naye? Jaribu kufikiria hali ilikuwaje kwa mwanamke kuishi na mume kama Nabali!

Je, wewe ni mwamini? Je, unayo Biblia? Je, unakiamini kilichoandikwa ndani ya Biblia? Unampenda Mungu na unaamini kuwa yeye yuko pamoja nawe katika mazingira yoyote yale? Je, unatafuta kumpendeza yeye au kujipendeza wewe mwenyewe?

Je, umepatwa na ubaridi au ugumu dhidi ya mumeo au mkeo kwa sababu unajisikia kuwa yeye ni mtu mgumu? Je, unamshughulikia kwa dharau na chuki? Yawezekana unataka kuniambia, “Lakini…” Lakini nini? Unataka kusemaje hapa? Unatakaje kujipa haki wewe mwenyewe – hapa hatuongelei juu ya dhambi kubwa, lakini ni kuhusu kile unachokifanya pale unapojisikia kuwa mumeo au mke wako ni mtu mgumu kwako.

Je, unatafuta njia ya kuikwepa hali unayoipitia kuliko kuitafuta njia ya Mungu katika hali hiyo? Yesu ndiyo njia. Tabia yake ndiyo njia na uzima. Kama umeingiwa na ubaridi au umekuwa mgumu juu ya mumeo au mke wako, na ikiwa wewe ni mkristo, usimlaumu – sio mapenzi ya Mungu kwako uwe baridi au mgumu bali huo ni uchaguzi wako mwenyewe. Usimlaumu MTU yeyote. Utubu badala ya kuuachilia moyo wako uwe mgumu. Jinyenyekeze mwenyewe chini ya mkono wa Mungu wenye nguvu na upokee neema izidiyo – ambayo itakubadilisha WEWE kwanza, na kisha umpende mumeo, mpende mkeo.

Abigaili hakuwa na Biblia isemayo kuwa, “mke ajinyenyekeze kwa mumewe”, wala hakuwa na Biblia inayosema, “waume wapendeni wake zenu”. Hakuwa na Biblia inayowaambia waumini wanaojikuta kwenye hali ngumu, , ‘Neema yangu YAKUTOSHA; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu.’ (2 Wakor. 12:9). Je, wewe unaamini mstari huu? Je utalipokea neno hili? Abigaili aliishi maisha ya namna hiyo. Je, wewe unaamini kuwa mume wako au mkeo ni mtu mgumu mno au ni mgumu kupita kiasi kwako? Lakini sikiliza neno la Mungu lisemavyo, “Lakini hutujalia sisi neema ILIYOZIDI; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.” (Yakobo 4:6).

Ikiwa utapungukiwa na neema ya Mungu katika mahusiano yako, waweza kupata sababu toka katika mistari hii ya neno ka Mungu.

Waweza kujisomea vitabu vingi vihusuvyo ndoa, waweza pia kwenda kuhudhuria semina nyingi zihusuzo ndoa, lakini kama humwendei Mungu na kujinyenyekeza mwenyewe mbele zake kwanza, hakuna hata jambo moja kati ya hayo ufanyayo yatakayo kusaidia.

Daudi alimwambia Abigaeli, ‘ubarikiwe wewe’! Nawe pia utabarikiwa, na utafanyika kuwa baraka kwa wengine nyumbani mwako ikiwa unampenda Kristo na kumtumikia kuliko kujipendeza mwenyewe tu, ikiwa unamfuata Yeye na ‘kuipoteza nafisi yako’ kwa ajili Yake kuliko kujaribu kujiokoa maisha yako kwa kujaribu kuikimbia hali ngumu au kulalamika kuhusu hali hiyo, na kuwa mgumu na mwenye uchungu.

Kumfuata Kristo Yesu na kujikana mwenyewe kutayafanya “machungu” kuwa “matamu” katika maisha yetu. “Kujitwika msalaba wako” haimaanishi kubeba mzigo nzito! Inamaanisha kujikana mwenyewe na kumchagua Yesu na njia yake, na huku kunaleta MABADILIKO katika maisha yako. Kama neno la Mungu linavyosema, “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito”, na tena, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni NIRA YANGU, mjifunze KWANGU; kwa kuwa mimi ni MPOLE na MNYENYEKEVU wa moyo; nanyi mtapata RAHA nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni LAINI, na mzigo wangu ni MWEPESI. (1 Yoh. 5:3; Mathayo 11:28-30).

Abigaeli hakujaribu kumbadilisha mumewe, alikabidhi uhai wake mikononi mwa Mungu na alikuwa anaridhia hukumu ya mumewe imwangukie yeye. Ikiwa Abigael angeweza kufanya hayo na kuwa kama hivyo nyakati za Agano la Kale, je, haitupasi sisi kuonyesha hata upendo mkuu na dhabihu katika mahusiano yetu sisi kwa sisi – sisi ambao tumeipokea neema na upendo wa Mungu kupitia Yesu Kristo ili kwamba uzima wake upate kudhihirishwa katika maisha yetu.

Inawezekana kabisa neno hilo siyo neno kwa wote, hata hivyo inawezekana ni neno kwa wengine.

Mungu alibariki neno lake kwa mioyo yetu.
 © David Stamen 2019 somabiblia.com

Share To:
Magpress

Bila jina

Kwa Moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na Maagizo yako. Moyoni mwangu nimeliweka Neno lako Nisije nikakutenda dhambi. (Zaburi 119:10-11).

Post A Comment:

0 comments so far,add yours