Je unaona kama mke wako hakuheshimu? Anahitaji upendo toka kwako. Je mume wako haonyeshi  upendo? Anahitaji heshima toka kwako.
Jinsi wewe na mwenzi wako mnavyotendeana kulingana na kila mmoja anavyohitaji, ndivyo jitihada zenu zitakapoleta matunda na kila mmoja atazidi kutiwa moyo kuendelea kutenda  mazuri kwa mwenzake na kupeelekea kuboresha ndoa yenu. Sasa ili kufanikisha hili kila mmoja wenu lazima ajue kuozungumza lugha ya upendo na heshima kwa mwenzake.
Zitazame tofauti zenu kama mtaji na sio tatizo
Tofauti kati yako na mwenzi wako haimaanishi kuwa mmoja wenu hayuko sahihi. Muombe Mungu aweze kukusaidia kuzikubali tofauti kati yenu na kukuwezesha kuzitumia kusaidiana na kufaidiana. Kumbuka mbele za Mungu wote ni sawa na mna thamani sana.
Muone mwenzi wako kuwa ni mtu mwenye nia njema
Kama mwanadamu mwingine mwenzi wako pia anaweza akafanya mambo yanayoonekana kama ubinafsi. Ni muhimu kuwa na imani kuwa mwenzi wako ana nia njema juu yako hata katika nyakati anaposhindwa kuonyesha upendo na heshima juu yako. Kumbuka kuwa ndani ya moyo wake mwenzi wako anakupenda na hapendi kukuudhi. Muombe Mungu akuwezeshe kumuona mwenzi wako kama yeye anavyomuona.
Chunga maneno yako
Maneno unayoongea yanaonyesha yaliyomo ndani ya moyo wako. Hivyo muombe Mungu aujaze moyo wako upendo na heshima kila siku, na muombe Roho mtakatifu kuifanya upya akili yako ili mawazo yako yawe mema yatakayokupelekea kuongea maneno mema yenye upendo. Kuwa mwangalifu nay ale unayoyasema kwa mwenzi wako na jinsi unavyoyachukulia yale mwenzi wako anayoyasema. Epuka kutumia maneno ambayo yatamuudhi mwenzi wako. Sikiliza kabla ya kujibu na fikiri kwanza kabya ya kuongea. Hakikisha unaongea kwa sauti nzuri ya upole na upendo na pia lugha ya mwili iwe ya upendo na upole pia. Nia kuongea maneno yanayojenga, ya kweli, yenye msamaha, ya kushukuru, ya kiMungu na yenye kutia moyo.
Tambua lugha ya mawasiliano ya mwenzi wako
Wanawake na wanaume wanatofauti kubwa sana ya lugha ya mawasiliano kati yao. Itambue lugha ya mawasiliano ya mwenzi wako, usiwe na hisia tu bali hakikisha unaielewa vyema ili kuepuka migogoro inayotokana na kutokuelewana au tafsiri isiyo sahihi. Sikiliza kwa makini, uliza pale unapokuwa na wasiwasi na azimia kujifunza na kuifahamu lugha ya mawasiliano ya mwrnzi wako. Kumbuka kutokuelewana kwa lugha ya mawasiliano na jinsi ya kuwasiliana hakumaanishi ndoa yenu ni mbaya, bali kunaonyesha tofauti ya matarajio na namna ya kuwasiliana. Jaribuni kwa pamoja kwa msaada wa Mungu kukabiliana na hali hii kwa upendo na maelewano.
Samehe
Tegemea msaada wa Mungu katika kukuwezesha kumsamehe mwenzi wako pale anapokukosea, mara zote. Kumbuka kuwa Mungu amekusamehe makosa yako na hivyo onyesha msamaha kwa mwenzi wako. Pale unapopata msamaha kwa mwenzi wako baada ya kumkosea tambua kuwa kuna uwezekano wa kuhitaji muda wa kuponya jeraha la moyo wake, kuwa muelewa na onyesha kuwa kweli umekubali kosa lako na upo tayari kurekebisha.
Timiza mahitaji ya muhimu ya mwenzi wako
Hakikisha unatumia uwezo wako kuhakikisha unatimiza mahitaji muhimu ya mke wako ya kuwa karibu naye, kuwa muwazi, kumuelewa, kumthamini, kumtunza na kumjali. Anahitaji uwe karibu naye katika hali zote, kuwa muwazi kwake na kushirikiana naye katika mawazo na mipango yako, kumsikiliza bila kujaribu kumbadilisha, kusuluhisha matatizo kwa pamoja, kumheshimu na kila wakati kumhakikishia upendo wako kwake.
Hakikisha unatumia uwezo wako kuhakikisha unatimiza mahitaji muhimu ya mume wako ya uongozi, mahusiano na kimwili. Tambua hitaji lake la kuongoza na usijaribu kuudharau uongozi wake, sikiliza kwa makini mawazo yake na ushauri, thamini hitaji lake la kuwa karibu na wewe na kuwa rafiki yake katika hali zote, na uwe tayari kwa hitaji la kimwili bila vipingamizi.
Tambua kuwa Mungu pekee ndiye anayeweza kutimiza kila hitaji la mwanadamu. Hivyo mwenzi wako anaposhindwa kutimiza baadhi ya mahitaji yako usikasirike wala  kuumia sana. Badala yake mwendee Mungu.
Angalia nia yako
Usitumie vitendo au lugha ya upendo na heshima kama njia ya kumfanya mwenzi wako kufanya kile unaachokitaka. Muombe Mungu akuwezeshe kuwa na nia safi kila wakati ili uweze kufanya jambo jema kwa nia njema na kwa wakati unaofaa, kumfurahisha Mungu na pia mwenzi wako. Onyesha upendo ha heshima kwa mwenzi wako bila kutarajia chochote kama malipo.
Chagua lililo jema bila kuangalia mwenzi wako anasema nini
Hata kama mwenzi wako haonyeshi ushirikiano kwa jitihada zako za kuonyesha upendo na heshima wewe endelea kufanya hivyo kwa moyo wa kupenda. Mungu atazilipa jitihada zako kwa kukubariki. Tamabua kuwa kwa kumwonyesha mwenzi wako upendo na heshima unakuwa unamtumikia Mungu na kumheshimu, hivyo endelea kufanya yaliyo mema bila kujali mwenzi wako anafanya nini. Mungu anaona na atabariki juhudi na jitihada zako.


Share To:
Magpress

Calvin Petro

Kwa Moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na Maagizo yako. Moyoni mwangu nimeliweka Neno lako Nisije nikakutenda dhambi. (Zaburi 119:10-11).

Post A Comment:

0 comments so far,add yours